• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
SWAGG: John Legend

SWAGG: John Legend

Na THOMAS MATIKO

JOHN Rogers Stephens mzuri kama alivyo, mademu wengi watakuambia sio msanii wa kawaida.

Kwa hakika aliyempachika jina lake la stejini, John Legend alipatia mia fil mia kwa sababu daima atabakia kuwa lejendari kwa kile alichokifanya kwenye tasnia ya muziki na hasa Marekani.

John Legend ana kila sababu ya kuitwa ‘snack’ na wanawake wa kisasa hasa wa jijini Nairobi. Waulize utasikia.

Mwanamuziki John Legend atumbuiza Februari 19, 2019, Oakland, California. Picha/ AFP

Licha ya kuwa na umri wa miaka 40, jomba kajaliwa sura, sio sura tu, bali yenye mvuto.

Ana mwili mzuri alioweza kuudhibiti kwa mazoezi ya mara kwa mara na kama haitoshi ni mkali wa kutupia pamba hasa suti.

Lakini kikubwa hata zaidi, ni kipaji chake cha uimbaji.

Ana sauti zaidi ya ninga, pia ni produsa makini na vile vile ni mcheza ala hatari hasa piano.

Kwa utamu wote huu, ni kwa nini mahodari wote hawatadondokwa na mate?

Malezi

Alizaliwa miaka 40 iliyopita kule Ohio akiwa mmoja kati ya wana wanne wa fundi nguo Phyliss Elaine na mumewe mfanyakazi wa kiwandani, Ronald Lamar Stephens.

Kwa maelezo haya unapata picha ya mtu aliyelelewa katika maisha ya kawaida sana.

Alipoanza elimu yake, mamake ndiye mara nyingi alimpa darasa nyumbani.

Baadaye alijiunga na shule ya upili ya Springfield North na alipofuzu akiwa na miaka 16, alifanikiwa kupata udhamini wa kujiunga na Vyuo Vikuu vya Harvard, Georgetown na Morehouse College.

Hata hivyo aliishia kujiunga na Chuo Kikuu cha Pennsylvania alikosomea fasihi.

Sanaa

Akiwa na umri wa miaka minne, alianza kuimba kwenye kwaya ya kanisani. Alipata fursa ya kuanza kucheza piano akiwa na umri wa miaka saba.

Akiwa chuoni, alihudumu kama kiongozi wa kundi la muziki lililojulikana kama Counterparts.

Kama bendi, walirekodi nyimbo nyingi John akiwa vokalisiti mkuu. Umaarufu wake wa muziki chuoni ulikuwa na mchango mkubwa ambapo rafiki yake mmoja alimkutanisha na mwanamuziki maarufu Lauryn Hill.

Lauryn aliyemzidi umri kwa miaka mitatu, alimpa John kazi ya kucheza piano kwenye wimbo wake ‘Everything Is Everything’ kutoka kwa albamu yake The Miseducation of Lauryn Hill.

Hatua hii ilimfungulia njia na akaanza kupata shoo kibao kule Philadelphia na taratibu himaya yake ikapanuka na kufikia New York, Boston, Atlanta, Washington DC na hatimaye Marekani kwa ujumla.

Baada ya kufuzu Chuoni 1999, John alifanya kazi kama mtaalamu wa usimamizi katika kampuni ya Boston Consulting Group.

Pia alianza kujishughulisha na masuala ya kuprodusi muziki, kuandika na kurekodi. Alidondosha albamu yake ya kwanza John Legend (2000) na kuifuatisha na nyingine Live At Jimmy’s Uptown (2001).

Mwaka huu ndiyo alikutanishwa na rapa Kanye West aliyemsaini katika lebo yake na kumpa kazi ya kuwa mmoja wa wanabendi wake.

Ni wakati huu ambapo pia alipata jina lake la usanii John Legend alilopewa na mwanamashairi mashuhuri wa Kimarekani J.Ivy ambaye baada ya kuzisikiza kazi zake nyingi, alimwambia zilimkumbusha malejendari wa zamani.

Alianza kumwita John Legend, jina ambalo naye Kanye vilevile alilipenda na kulikoleza na hapo likaishia kudata. Kwa asilimia kubwa, ufanisi wake kimuziki umehusishwa na ushirikiano mwema na sapoti kubwa aliyopata kwa kutangamana na Kanye West ambaye tayari alikuwa maarufu na aliyemsaidia kumfungulia milango zaidi kupitia koneksheni zake kibao. Hii ndio sababu wamesalia kuwa washikaji wakubwa licha ya tofauti zao za kimitazamo hasa kuhusu siasa.

Mapenzi

Kwenye harakati zake za kisanii, 2007 alikutana na kichuna Chrissy Teigen aliyemtumia kama video vixen wa wimbo wake Stereo.

Ilipaswa kuwa kazi lakini mapenzi yakaota. Disemba 2011, Legend alimchumbia na kumwoa Septemba 2013 kwenye harusi iliyofanyika Como, Italia. Wimbo All of Me ulikuwa utunzi spesheli kwa Chrissy.

Walijaliwa mtoto wao wa kwanza binti Aprili 2016 na Januari mwaka jana wakapata mtoto wao wa pili wa kiume.

Mkwanja

Kwa makadirio anasemekana kuwa na mali isiyopungua thamani ya dola 45 milioni. Mkwanja wake kaupiga kupitia shoo zake, zingine zikiwa za kibinafsi alizoalikwa na kulipwa kuwatumbuiza watu mashuhuri duniani.

Pia ni kocha wa muziki katika kipindi cha ‘The Voice Coach’ ambapo karipotiwa kung’oka na kiasi kisichopungua dola 8 milioni kila mwaka.

Usisahau pia kutokana na mwonekano wake wa kishombe shombe, ameweza kuvutia dili kibao za kimatangazo zilizomlipa vizuri sana.

Mjengo
Pamoja na familia yake changa wanaishi kwenye mtaa wa kifahari wa Beverly Hills, California kwenye jumba alilonunua kwa dola 14 milioni.
Mjengo huo wenye vyumba vitano vikuu vya kulala na bafu nane, ulikuwa ukimilikiwa zamani na mwanamuziki staa Rihanna.

Usafiri

Kwa upande wa mikebe anayozunguka nayo mtaa, anamiliki kadhaa na kwa hadhi yake, sio vifaa vya kubahatisha.

Cadillac Escalade thamani yake Sh9.6 milioni, Chevrolet Impala (Sh3 milioni) na Lexus LS (Sh8.3 milioni), Tesla (Sh10 milioni) ni baadhi tu ya mikebe hiyo.

You can share this post!

AUNTY POLLY: Mama anibebesha mzigo wake, nisaidie

Waandamanaji Sudan wakaidi hali ya hatari

adminleo