• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Ujerumani kusafishia wakazi maji ya bahari

Ujerumani kusafishia wakazi maji ya bahari

NA KALUME KAZUNGU

WAFADHILI kutoka nchini Ujerumani wamezindua mradi wa kusafisha maji ya chumvi kutoka Bahari Hindi na kuyageuza safi kwa matumizi ya binadamu katika harakati za kukabiliana na tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji eneo la Mokowe, Kaunti ya Lamu.

Mradi huo uliogharimu kima cha Sh 4 milioni unalenga kusafisha takriban tani 15 za maji ya chumvi katika kila kipindi cha saa 24 kwa kuyasafisha na kuyawezesha kutumiwa na binadamu.

Mradi huo ulijengwa kwenye shule ya watoto wenye akili tahira iliyoko mjini Mokowe na mbali na kuwasaidia zaidi ya watoto 100 kwenye shule hiyo, mradi huo pia unanuiwa kuwapa maji safi wakazi wa vijiji vya Mokowe na viungani mwake.

Mamia ya wakazi eneo hilo wamekuwa wakitaabika kwa kukosa maji safi ya kunywa, hatua ambayo imechangia akina mama na wanafunzi kuandamana na wazazi wao hadi kwenye maeneo ya mbali wakitafuta maji.

Akihutubu wakati wa ufunguzi rasmi wa mradi huo, Mwakilishi wa wafadhili wa Ujerumani, Bw Ulf Hoffmeyer-Zlotnik alisema azma yao ni kuboresha maisha ya wakazi eneo hilo.

Alisema sehemu nyingi za Lamu zinakumbwa na uhaba wa maji na kwamba kuna haja ya wafadhili zaidi kujitokeza ili kukabiliana na tatizo hilo sugu.

“Mradi wa usafishaji maji umegharimu Sh 4 milioni. Maji yatakayosafishwa ni yale ya chumvi kutoka Bahari Hindi. Mradi utaweza kusafisha angalau tani 15 za maji kila muda wa saa 24. Furaha yetu ni kuona kwamba maisha ya wakazi wa Lamu yameboreshwa vilivyo,” akasema Bw Zlotnik.

Naye Gavana wa Lamu, Fahim Twaha aliwasifu wadau kutoka Ujerumani kwa kujitolea kwao katika kutatua tatizo la maji eneo la Mokowe.

Alisema kaunti iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuona kwamba tatizo la ukosefu wa maji kaunti ya Lamu linakabiliwa na kutatuliwa kikamilifu.

“Tunawashukuru wafadhili wa Ujerumani kwa kujitolea kwao kuanzisha mradi huu. Azma yetu ni kushirikiana na wafadhili zaidi ili kutatua tatizo la maji kwenye sehemu mbalimbali za Lamu,” akasema Bw Twaha.

You can share this post!

Kanisa ladai upangaji uzazi umelipunguzia waumini

Boinett alifaulu kwa mengi ila alifeli kumaliza ukatili wa...

adminleo