• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
WASONGA: Raila na Ruto ni maadui wa maendeleo ya Kenya

WASONGA: Raila na Ruto ni maadui wa maendeleo ya Kenya

Na CHARLES WASONGA

VITA vya maneno kati ya Naibu Rais William Ruto na wafuasi wake kwa upande mmoja, na Raila Odinga na wafuasi wake kwa upande mwingine ni ithibati tosha kwamba wawili hao ni maadui wa ustawi wa taifa hili.

Kwa hakika malumbano yao hayana manufaa yoyote kwa juhudi za kuleta umoja nchini, kubuni nafasi za kazi na mipango ya kuimarisha uchumi wa nchini kupitia utekelezaji wa ajenda nne kuu za maendeleo za serikali ya Jubilee.

Madai ya Dkt Ruto kwamba Bw Odinga anashirikiana na serikali kuvuruga mambo katika chama tawala cha Jubilee hayana mashiko, kwa sababu kiongozi huyo wa ODM hana uwezo na mamlaka ya kufanya hivyo.

Ukweli ni kwamba tangu mwanasiasa huyu mkongwe aliporidhiana kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9 mwaka jana, utulivu wa kisiasa umerejelea nchini.

Kwa mfano, maandamano ya kila mara ya wafuasi wa upinzani wakipinga hili au lile sasa yamegeuka kuwa historia.?Utulivu huu umepiga jeki sekta ya utalii kwani kulingana na takwimu za serikali, idadi ya watalii wanaozuru Kenya imepanda sawa na pesa za kigeni ambayo zimetimu Sh150 bilioni katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Serikali pia amekuwa ikitumia utulivu huu kuvutia wawakezaji, haswa kutoka nje, katika jitihada za kufanyika mpango wake wa kufanikisha ujenzi wa nyumba 500,000 za gharama nafuu katika kufikia mwaka wa 2022.

Kulingana na Waziri wa Uchukuzi na Miundo Msingi na Nyumba James Macharia, tayari zaidi ya wawekezaji 20 kutoka nje wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa nyumba nchini.

Kwa hivyo, ikiwa lengo kuu la Naibu Rais ni kufanikisha ajenda hii ya serikali anayoitumikia, basi hana budi kukoma kuingiza siasa katika muafaka kati ya bosi wake na Bw Odinga. Anapaswa kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi kwa kukoma kuingilia utendakazi Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

Na muhimu zaidi, Bw Ruto anafaa kuwashauri wafuasi wake, haswa wabunge, wakomeshe mtindo wa kumshambulia Bw Odinga na Rais Kenyatta kila mara katika mikutano ya hadhara. Ukweli kuhusu madai yao kwamba “handisheki” kati ya wawili hao ililenga kuzima ndoto ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu mnamo mwaka wa 2022 hauwezi kuthibitishwa wakati huu, kwani imesalia miaka mitatu na nusu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao.

Kwa hivyo, madai kama hayo hayachangii kwa njia yoyote katika utekelezaji wa ahadi chungu mzima ambazo serikali ya Jubilee ilitoa wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga na wafuasi wake sharti wasitishe kampeni za kumchafulia jina Dkt Ruto kila mara.

Huu mwenendo wa kumsawiri Naibu Rais kama kiongozi mfisadi na mnyakuzi wa mali ya umma hautachangia kwa vyovyote kupalilia umoja na maridhiano nchini.

Kiongozi huyu wa ODM anafaa kumheshimu Dkt Ruto ikiwa haja yake ni kufanikisha maazimio ambayo yako kwenye mwafaka kati yake na Rais Kenyatta, haswa azimio la kuliunganisha taifa.

Na endapo Bw Odinga ana ushahidi wowote wa kumhusisha, moja kwa moja, Naibu Rais na uporaji wa mali ya umma, jambo la busara kufanya ni kuuwasilisha kwa asasi husika wala sio kumhukumu Dkt Ruto katika hafla za mazishi.

Kwa hivyo ikiwa kweli wawili hawa ni washirika wa karibu wa Rais Kenyatta, wanavyodai kila mara, basi sharti wadhihirishe hilo kwa vitendo kwa kukoma kuonekena kuvuruga serikali kupitia malumbano ya kila mara.

[email protected]

You can share this post!

NCPB yatumia Sh6.8 bilioni kununua mahindi

TAHARIRI: Boinnet anaondoka bila kutimiza mengi

adminleo