• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
TZ yachoma samaki wenye sumu kutoka China huku Kenya ikizidi kununua

TZ yachoma samaki wenye sumu kutoka China huku Kenya ikizidi kununua

Na PETER MBURU

SERIKALI ya Tanzania Jumatatu iliteketeza shehena ya tani 11 za samaki kutoka Uchina, baada ya kudaiwa kuwa na sumu, ya kemikali za zebaki.

Katika zoezi lililosimamiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, shehena hiyo iliteketezwa katika eneo la dampo la pugu, Kinyamwezi, Jijini Dar Es Salaam.

Hatua hiyo ya kijasiri ya serikali ya Tanzania ilikuja wakati Kenya imeshindwa kuchukua hatua kama hiyo kuthibiti sekta ya uvuvi kutokana na samaki wanaotoka China, licha ya malalamishi ya muda mrefu kuwa viwango vyake vya ubora ni vya kutiliwa shaka.

Desemba mwaka 2018, uchunguzi uliofanywa na gazeti la The East African kuhusu samaki wa nchi hiyo ulionyesha kuwa wana madini ya chuma ambayo yana madhara kwa afya ya binadamu, baada ya samaki hao kununuliwa kutoka soko la Gikomba, Nairobi.

Samaki hao walipatikana kuwa na kemikali za zebaki, copper na arsenic, uchunguzi huo ulipofanywa.

Hii ilikuwa baada ya utafiti kufanywa Kenya na Tanzania na kuonyesha kuwa samaki wa kutoka China wanaliwa kwa viwango vikubwa katika mataifa haya mawili.

Samaki hao wamepata soko kutokana na bei yao ya chini, ikilinganishwa na wanaovuliwa humu nchini na wakipendelewa na watu wa mahoteli kutokana na bei yao ya chini.

Uchunguzi kwenye maabara katika chuo kikuu cha Nairobi ulionyesha samaki hao walikuwa na viwango vya chuma hizo, kumaanisha kuna uwezekano maji ambapo wanavuliwa yana kemikali hatari kwa afya.

“Matumizi ya muda mrefu ya samaki hawa yanaweza kuwa na athari mbaya kiafya,” Prof James Mbaria akasema.

Kenya imekuwa ikitegemea Uchina pakubwa ili kujiwezesha kushibisha soko la samaki, kiwango inachonunua kutoka taifa hilo la Asia kikizidi kukua hadi kufikia samaki wa Sh1.7 bilioni mnamo 2017.

Novemba 2018, Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufuku uingizaji wa samakiwa kutoka China nchini akidai kuwa walikuwa wakiua sekta ya uvuvi, lakini hatua hiyo ikabatilishwa miezi mitatu baadaye.

Lakini mnamo Februari 2019, idara ya uvuvi nchini ilisema iliamua kubatilisha hatua hiyo kufuatia upungufu wa chakula hicho sokoni.

Kenya imekuwa ikinunua takriban kilo 1.8 milioni za samaki kila mwezi kutoka Uchina, huku wanaovuliwa humu nchini wakiwa tani 135,000 kila mwaka, ikilinganishwa na kiwango kinacholiwa cha tani 500, 000.

Hadi sasa, Kenya imeshindwa kujikwamua kutoka kwa mtego wa China kuilisha samaki hawa ambao ni hatari kwa afya ya binadamu.

You can share this post!

Washukiwa wa ubakaji waachiliwa, korti yasema sura ya...

Ndege mbili aina ya Boeing 737 MAX 8 zapiga abautani angani

adminleo