• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KAULI YA WALIBORA: Ajabu ya kuonea fahari Kiswahili chenye mabaka!

KAULI YA WALIBORA: Ajabu ya kuonea fahari Kiswahili chenye mabaka!

Na KEN WALIBORA

NINI kitawafanya Wakenya wakizungumze Kiswahili sahihi na sanifu?

Hili swali linanitanza wala sijui jibu lake.

Kila nipitapo watu wanataja tarakimu au nambari kwa Kiingereza huku wakidai wanazungumza Kiswahili.

Sikiliza vituo vya redio uone. Kila watangazaji wakitaja tarakimu katika vituo vya Kiswahili, mathalani nambari ya simu au namnari ya usajili wa gari, zote wanazitaja aghalabu tarakimu kwa Kiingereza. Utawasikia wanasema zero, seven two two, zero two one… Wasikilize wafanyabiashara nao na wateja wao, aghalabu wanapopiga bei ya nguo, nafaka au chochote, aghalabu wanataja bei kwa Kiingereza ingawa wanadai wanazungumza Kiswahili. “Hii unauza how much?” “Hii ni five forty.”   Utawasikia wahudumu wa vituo vya mafuta nao wakisema kwamba nambari ya tili ya lipa na mpesa ni “one eight two five ten.”

Kwa hiyo, kwa hawa wasemaji hodari wa Kiswahili watu wanaotaja tarakimu kwa Kiswahili hasa kama mimi ama ni mahambe au wanazungumza lugha ya kigeni. “Ee?”  Huwa wananishangaa kila nikitaja nambari kwa Kiswahili. “Unasema nini?” Wanapigwa na kibuhuti kama walioona mvua ikinyesha bila ya kuwapo kwa mawingu. Je, ni kosa kufikia mkataa kwamba nambari au tarakimu za Kiswahili zinaendelea kuwa msamiati wa kigeni, msamiati usioeleweka? Je, kusema one ni bora zaidi kuliko kusema moja? Kuna fahari zaidi kusema five forty kuliko kusema mia tano hamsini? Mantiki ya kunogesha Kiswahili kwa tarakimu za Kiingereza bado haijaniingia akilini. Labda ni kwa sababu ya uzumbukuku wangu; zumbuku hapa nilipo sijui ngoma ipo wapi. Ila mpaka sasa sijasikia wasemaji mahiri wa Kiingereza wakipachika pachika tarakimu za Kiswahili ama Kiganda, Kisebei, Kimaragoli, Kichagga, Kihaya au Kiduruma katika mazungumzo yao. Naam, bado katika umri wangu wa makamo, sijawahi kumsikia msemaji asili wa Kiingereza akisema, “There were hamsini girls at the party” au “You need to buy motor bike worth sitini shillings.”

Vilevile sijawahi kuwasikia watu wa kwetu huku wakihamisha hamisha tarakimu za lugha moja asilia hadi kwa lugha nyingine. Mathalan ni muhali kumsikia msemaji wa Kikikuyu akisema “andu ario” kwa kuongeza neno “ario” la Kijaluo la tarakimu.

Hata hivyo, wanaisimu wanapaswa kutufumbua macho kuhusu vile maneno ya Kiarabu kama vile “thenashara”  kwa maana ya 12 yalivyoingia na kukita kambi (kauli iliyoshika sana siku hizi) katika kanzi ya maneno ya tarakimu za Kikikuyu.

Baadhi yetu tutakerwa na juhudi zozote za kuchanganya tarakimu za lugha zetu na lugha nyinginezo za huku kwa jumla. Ila ambavyo neno “thenashara” la Kiarabu limeshakubaliwa  katika Kikikuyu na  maneno “one, two, three,” ya Kiingereza yamebisha hodi na kufunguliwa milango katika Kiswahili, hatuna budi kujiuliza maswali chungu nzima.

Mbona maneno ya mbali yanatamanisha zaidi?

Na lini Kiswahili kitakuwa Kiswahili hasa? Mbona si kila mtu anakionea uchungu au kukerwa na kudhalilishwa kwa Kiswahili?

You can share this post!

Ndege mbili aina ya Boeing 737 MAX 8 zapiga abautani angani

Magavana sasa kusimamia uainishaji wa miji na manisipaa...

adminleo