• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 4:28 PM
Afueni Arsenal baada ya Lacazette kuruhusiwa kucheza dhidi ya Rennes

Afueni Arsenal baada ya Lacazette kuruhusiwa kucheza dhidi ya Rennes

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KLABU ya Arsenal imepata afueni baada ya mshambuliaji wao Alexandre Lacazette kuruhusiwa kucheza dhidi ya Rennes kwenye mechi ya Europa League leo Alhamisi usiku ugani Emirates.

Mfaransa huyo alikuwa amepigwa marufuku ya mechi tatu na UEFA baada ya kupewa kadi nyekundu wakati wa mechi ya awali dhidi ya klabu ya BATE Borisov mnamo Februari 2019 kwa kumpiga kumbo Aleksandar Filipovic katika hali ya kuhatarisha maisha yake.

Lacazette alikuwa ametumikia mechi mbili huku klabu ikisubiri uamuzi wa UEFA kuhusu rufaa waliowasilisha kumtetea.

Picha ya Februari 27, 2019, ya straika Alexandre Lacazette wa Arsenal asherehekea baada ya kufunga bao la tano la klabu yake ilipoikaribisha Bournemouth uwanjani Emirates, London. Picha/ AFP

Lakini sasa UEFA imethibitisha kwamba Arsenal imeshinda rufaa hiyo baada ya nyota huyo kutumikia mechi mbili na sasa yuko huru kuwachezea kuanzia leo Alhamisi.

Taarifa kutoka makao makuu ya UEFA ilisoma: “Rufaa iliyowasilishwa na Arsenal imekubaliwa, lakini shingo upande.”

Lacazette alikosa mechi ya marudiano ya 32 bora dhidi ya BATE Borisov iliyochezwa Februari 21, na ya mkondo wa kwanza ya 16 bora dhidi ya Rennes mnamo Machi 7 ambapo Arsenal walitandikwa 3-1.

Lacazette pamoja na Sokratis Papastathopoulos walitoa mchango mkubwa katika ushindi wao wa 2-0. Kadhalika, Henrikh Mkhitaryan atarejea leo baada ya kuikosa mechi hiyo ya mwishoni mwa wiki.

Hata hivyo, Hector Bellerin, Rob Holding na Danny Welbeck hawatakuwa kikosini kutokana na majeraha tofauti yanayowakabili.

Kwa upande mwingine, beki wa kulia Roman Danze na kiungo Rafik Guitane hawatacheza baada ya kuumia mwezi Oktoba.

Klabu ya Ufaransa

Hii itakuwa mara ya 26 kwa Arsenal kupangiwa kucheza na klabu ya Ufaransa, pia ikiwa ya 13 nyumbani, ambako wameweza kuibuka na ushindi mara tano katika mechi 12 zilizopita, huku wakishindwa tatu.

Mara ya kwanza Rennes kucheza na klabu kutoka Uingereza iliuwa mnamo 2001 walipokutana na Aston Villa katika nusu-fainali ya UEFA Intertoto Cup. Walishindwa kutokana na mabao ya ugenini baada ya kushinda mkondo wa kwanza huko Brittany.

Kufikia sasa, Arsenal wameenda mechi tano bila kushindwa katika ligi kuu ya EPL, ikiwemo sare ya 1-1 dhidi ya mahasimu wao, Spurs pamoja na ushindi wa 2-0 dhidi ya Manchester United.

Lakini kichapo cha 3-1 kutoka kwa Rennes katika mkondo wa kwanza kutawalazimu washinde kwa idadi kubwa ya mabao ili wasonge mbele.

Kwa upande mwingine, Rennes hawajashindwa katika mechi tano za karibuni katika mashindano tofauti na pia hawajashindwa katika michuano ya Ulaya tangu hatua ya makundi iliyoanza Novemba 2018.

Vikosi:

Arsenal

Cech, Maitland-Niles, Mustafi, Koscienly, Monreal, Torreira, Xhaka, Ramsey, Ozil, Aubameyang, na Iwobi.

Rennes

Koubek, Zeffane, Da Silva, Sitoe, Bensebaini, Sarr, Andre, Grenier, Ben Arfa, Bourigeaud, na Hunou.

You can share this post!

Agizo la Rais laleta tumaini na shaka kwa wanaspoti

NIPO KWA KAZI HII: Magoli ya CR7 yanusuru Juventus

adminleo