• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Thamani ya Prof Magoha ni Sh250 milioni

Thamani ya Prof Magoha ni Sh250 milioni

Na CHARLES WASONGA

PROFESA George Magoha ambaye aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa Waziri wa Elimu anamiliki mali ya thamani ya Sh250 milioni, kulingana n stakabadhi alizowasilisha mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi.

Stakabadhi hizo ambazo zilichambuliwa na wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Spika Justin Muturi zinaonyesha kuwa mapato yake yanatoka katika uwekezaji wake katika miradi ya ujenzi wa nyumba, uchukuzi na upanzi wa miti.

Profesa Magoha pia alisema kuwa amekuwa akichuma mapato kutoka kwa kazi yake ya utabibu, haswa upasuaji.

Msomi huyo pia anamiliki nyumba kadha jijini Nairobi na Yala katika kaunti ya Siaya, magari kadha kati ya mali nyingine.

Profesa Magoha, ambaye alipigwa msasa na wabunge mnamo Alhamisi, alipendekezwa kwa wadhifa huo na Rais Uhuru Kenyatta na jina lake likawasilishwa bungeni mnamo Machi 6.

Aliwaambia wabunge kwamba maishani hajakuwa akivutiwa na haja ya kujichumia pesa nyingi, akitoa mfano wa kisa kimoja mnamo 1987 alipoacha kazi ya udaktari nchini Lagos, Nigeria ambapo alikuwa akipokea mshahara mkubwa kuja Kenya kupokea mshahara wa chini

“Niliacha mshahara wa Sh100,000 kwa mwezi nyakazi hizo kuja kuajiri kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) kwa mshahara wa Sh6,000,” Profesa Magoha aliwaambia wabunge.

Alihudumu kama Naibu Chansela wa UoN kati ya miaka ya 2005 na 2015.

Ikiwa uteuzi wake itaidhinishwa, Profesa Magoha atakabiliwa na kibarua kigumu cha kufanikinisha utekelezaji wa mtaala mpya wa masomo ambao ulianza Januari mwaka huu katika mazingira tatanishi.

You can share this post!

Sikumfuta kazi Matiang’i, asema Magoha

Mjadala bungeni kuhusu mayai milioni 33 kutoka Uchina

adminleo