• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Umuhimu wa kujiandaa na kujenga msingi thabiti wa ndoa katika dini

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Umuhimu wa kujiandaa na kujenga msingi thabiti wa ndoa katika dini

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo.

Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad Swallallahu ‘Alayhi Wasallam, Maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyama.

Katika kumuumba kwake mwanadamu, Mwenyezi Mungu aliweka utaratibu wa kuwepo mahusiano kati ya mume na mke, ili kuendeleza uzao kwa wanadamu, kuwaondolea upweke na kuwatunukia utulivu, faraja, huruma, mapenzi, upendo na ushirikiano.

“Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri,” Arruum 21.

Kutokana na umuhimu wa ndoa katika maisha ya mwanadamu, tumeona kuna haja ya kukumbushana, hasa vijana jinsi ya kujiandaa kwa maisha ya ndoa kabla ya kuoana.

Katika Uislamu inapofikia hatua ya kutaka kuoa au kuolewa, pande zote mbili hukabiliwa na mawazo mengi ni vipi atampata mchumba sahihi.

Tatizo kubwa ni katika kumchagua mwenza sahihi na mwenye sifa, ambaye utakapompata na kumuoa/kuolewa, atakuwa ndiye mshirika wako wa maisha.

Vilevile hutizamwa ni vigezo gani atumie muoaji au muolewa katika kufikia lengo lake la kumpata anayestahili na kukidhi haja.

Ikumbukwe kwamba pamoja na kwamba kuna dhana kwamba mwanamke hawezi kuchumbia na hana nafasi ya kuchagua mume anayetaka aolewe naye, ukweli ni kwamba kwa utashi wake mwanamke ana haki ya kumkubali au kumkataa mchumba anayekuja kwake.

Kusumbua

Kwa ujumla mambo ya ndoa huwasumbua watarajiwa huku kila mmoja akiwa na mitazamo tofauti katika chaguo.

Kila upande ukiwa umekua na kulelewa katika mazoea, desturi na tamaduni tofauti, mambo ambayo yana athari kwa namna moja au nyingine katika makuzi.

Baadhi ya wenye dhamira ya kuoa au kuolewa, wanakuwa hawafahamu wanahitaji mke au mume wa aina gani. Wakati mwingine wanajikuta wanaingia katika hamu ya kuwa katika ndoa, lakini bila kujua wanataka kuwa na wenza wa namna gani.

Wengine hujikuta wakijiingiza katika ndoa bila ya kuwa na ufahamu wa kutosha au taaluma yoyote inayohusiana na maisha hayo ya mahusiano na hatima yake hukosa uwezo wa kuziendesha ndoa zao.

Lakini pia wapo ambao hawana kabisa uelewa wa misingi ya kuoa na kuolewa zaidi ya kusukumwa na fikra finyu ya kutamani kuwa na mwenza kwa ajili ya kukidhi tu matamanio ya nafsi na hususan tendo la ndoa na kurahisishiwa baadhi ya majukumu kama vile kupika, usafi wa nyumba, kufua na kadhalika.

Wapo wanaotamani kuingia katika mahusiano ya ndoa kwa lengo moja tu, la kupata wepesi wa kupata mali na maisha ya anasa na starehe.

Kwa ujumla wengi wanaotaka kuoa au kuolewa, mara nyingi hawana fikra halisi na pana ya kusudio la ndoa. Si kidini si kimazingira.

Hata maandalizi katika kuliendea jambo hilo wakati mwingine hayafanyiki vya kutosha na kwa kiasi kikubwa. Uchaguzi wao hautizami sekta za msingi kama dini na maadili kwa ujumla wake.

Katika kufanya uchaguzi wa mtarajiwa, iwe ni mume au mke, kuna mambo mawili yanaweza kujitokeza, nayo ni kuwa na ndoa iliyojaa matarajio ya watarajiwa (kama yalikuwepo kabla) au kuwa na ndoa iliyokosa matarajio ya watarajiwa na hivyo mwisho wake kuwa ni balaa badala ya raha, dhiki badala ya faraja.

Mtu anaweza kuoa au kuolewa na akafurahia uamuzi wake huo kwa jinsi ndoa ilivyotimiza matakwa ya kuitwa ndoa.

Lakini mwingine akajutia uamuzi wake kutokana na kukithiri maudhi mpaka kufika kuhasimiana na kuachana.

Ili kuepukana na hali hii, kuna haja ya kuwa na utaratibu mahususi kwa wazazi, wazee na viongozi wetu wa dini katika jamii yetu, kukuza mazoea ya kutoa mafunzo na miongozo kwa vijana na wetu ili kujaribu kutoa mwongozo kujaribu kuokoa janga hili la kasi ya kuharibika mahusiano ya ndoa, jambo ambalo Mwenyezi Mungu anasema linamchukiza sana.

Kwa mtazamo wangu, dini ndio mwongozo namba moja wa kujenga ustaarabu ya maisha ya mwanadamu.

Kwa maana hiyo kuna haja hasa kwa Waislamu, ukiacha zile hotuba za ndoa, kusisitizia thamani ya mafunzo ya dini katika kuliendea jambo hili.

Ifahamike tu kwamba msingi wa ndoa yoyote ile ni mafunzo ya dini.

Dini ndiye mwalimu wa maadili, dini ndiye mwalimu wa busara, dini ni mwalimu wa uvumilivu na subra, dini ndiyo ustaarabu wa maisha, dini ndiyo chanzo cha kumjua na kumtegemea Mwenyezi Mungu aliyetuumba ambaye ndiye mwenye dini yake na kaamuru wanadamu kuifuata ili kufaulu hapa duniani na kesho akhera.

Utulivu katika ndoa ni moja katika mambo muhimu yanayodumisha maisha ya ndoa kwa wanandoa.

Vijana wanaotarajia kutimiza suna hiyo wanatakiwa kufundishwa hilo na wawe na yakini na hilo.

Haina maana kosa kidogo tu, au kosa moja likamfanya mtu mara moja akakosa uvumilivu wa kutoa nafasi ya mwenzake kuonywa au kujirekebisha, yeye keshaamua.

Lakini umuhimu wa ndoa kwa kuoa wajane, wajakazi, maskini au mafukara, kuleta maana kwamba ndoa kunusu.

“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu”.

Ndoa huunganisha koo kufikia kuweza kurithiana kati ya mume na mke. Annisaa 12

Ndoa huzuia zinaa.

Ni jambo la msingi kwa kila mwanandoa au anayetarajia kuingia katika ndoa, afahamu kwamba ndoa ni kati ya riziki ambazo Mwenyezi Mungu amewapa waja wake.

Katika ndoa kuna wajibu, haki, majukumu na utaratibu wake katika maisha.

Kabla ya kuoa au kuolewa na kufunga ndoa, kuna haja ya kujiuliza kwa nini unaliendea jambo hilo. Hili ndilo swali la kwanza mhusika anapaswa kujiuliza moyoni na kupata majibu yake.

Ndoa humpa mtu heshima na katika jamii, kupata watoto, kutafuta sitara, kujenga familia bora, kuwaridhia wazazi wawili na kukidhi hamu za kijinsia.

Lakini wapo pia ambao kufikia maamuzi ya kuoa kwa kufuata marafiki, kusaidiana majukumu kama vile kupika na kuosha nguo, kusaidia ulezi wa wazazi, kupata mali na utajiri, kuepuka lawama na maudhi na kadhalika.

Ni lazima yawepo malengo ya kuoa kabla ya tendo lenyewe. Lakini malengo yenyewe lazima yawe sahihi na siyo ya kinafsi na ya matamanio tu.

Mtume (saw) amesema, “Mwanamke huolewa kwa mambo manne. Kwa (ajili ya) mali yake, kwa nasaba yake, kwa uzuri wake na kwa dini yake, basi mtafuteni mwenye dini (kwani) mikono yako itatakatika na michanga. (Bukhari na Muslim).

You can share this post!

DOMO KAYA: Riri anabisha, nani atamlaki?

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Kadri maafa mengi yanavyotokea...

adminleo