• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
SOKOMOKO: Penzi lianzapo kufa

SOKOMOKO: Penzi lianzapo kufa

KWANZA mawasiliano, kasi yake hupunguwa,
Hayawi masemezano, ja mwanzo yalivyokuwa,
Hata soga na vigano, hukoma pasi kujuwa,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

Pili ni mifarakano, hutokea kila mara,
Muda wote mivutano, ambayo haina dira,
Huwa shida mapatano, hii mbaya biashara,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

Tatu jambo la dharau, huanza kuonekana,
Kuonana mabahau, kwenye vitu viso mana,
Wakati kumbe walau, mwaweza eleweshana,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

Nne kuaminiana, huwa ni kitendawili,
Kwake bibi pia bwana, jambo hili ni la kweli,
Mitego hutegeana, ashikwe mwizi kamili,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

MFAUME HAMISI,
‘Mshairi Machinga’
Dar es Salaam, Tanzania

Nipe muda nifikiri

Eti mambo dijitali, hivyo ndivyo wasemavyo,
Na hakuna wanawali, hivyo ndivyo tu yalivyo,
Kitazama mara mbili, utapata ndivyo sivyo,
Nipe muda nifikiri, ziko wapi hizo siku?

Zama zile yamkini, banati walipendeza,
Vazi hadi miguuni, na nywele walilegeza,
Adabu walithamini, na katu hawakubeza
Urembo ungeamini, ni weusi ulokoza.

Ziko wapi hizo siku, walipotazama chini?
Wamekuwa ja chiriku, hasikizi ukineni,
Wanapenda tu udaku, hawajui samahani,
Wakishayala mabuku, utasema nao nini?

Hawa binti siku hizi, kama sumu yake swila,
Hawaheshimu wazazi, hata awe wa kabila,
Ndoa nazo hawawezi, hata kupika chakula,
Ni kweli hiki kizazi, chahitaji pia sala.

JAMES A OWUOR
Chuo Kikuu cha Kisii

Lugha ya mwana

Toto asemapo ‘n’nya’, nina humwamba ‘pupu’
Akamwondowa foronya, amwambe ‘susuu’
Tumbo linapomsinya, anaambiwa ‘luluu’
Lugha ya mtoto mchanga, hukolezwa na ninae.

Ninaye akimsonya, afanyapo makuruu
Humwambia mwana, n’nya haraka mumuu’
Wala hampi mwanya, amwamba ‘hebu nunuu’
Lugha ya mtoto mchanga, hukolezwa na ninae.

Mwana mchanga hupenya, popote wakati huu
Gesi ikimtekenya, tumbo likose nafuu
Ili asije tawanya, nina humwamba ‘susuu’
Lugha ya mtoto mchanga, hukolezwa na ninae.

Mwana wa mja si panya, amwaye kijuujuu,
Shuti nina humkanya, hali ipate suluu,
Humwambia toto ‘n’nya, chutama uchuuchuu’
Lugha ya mtoto mchanga, hukolezwa na ninae.

LUDOVICK MBOGHOLI
Al-Ustadh-Luqman
Ngariba Mlumbi (001)

Familia zote makiweni

Ningeweza kutabiri, kesho ningaitangaza,
Ndege hawangeabiri, mauti yangewasaza,
Ila sasa ni tiriri, waja tumewapoteza,
Familia makiweni, alopanga ni Manani.

Alopanga ni Manani, wino wake hufutiki,
Haulizwi kwa nini, kutwaa watu mbee za haki,
Tulobaki tusalini, tuambaani hamaki,
Familia makiweni, walokwenda maghufira.

Walokwenda maghufira, isiwapate adhabu,
Dua ndiyo bora sera, kuwaepushia tabu,
Ingawa kifo hukera, la mno huwa kutubu,
Familia makiweni, Mola ndiye nguzo njema.

FRANCIS MAINA MACHARIA
‘Bin Macharia’
Sacred Heart Mwakiwiwi Girls

Mapenzi asali chungu

Nimetoka kote ng’ambo, wenzangu hamjambo,
Nimewaletea mambo, na sisemi majigambo,
Niliishi kitambo, kabla kuja kiwambo,
Tahadhari hili jambo, mapenzi asali chungu.

Leo utaitwa ua, kesho witwe malaika,
Atafanya kunyanyua, ua liwe linanuka,
Polepole takuua, ubaki kwitwa mzuka,
Tahadhari hili jambo, mapenzi asali chungu.

Mla nawe hafi nawe, walinena jambo hili,
Leo atacheka nawe, na kukosha wako mwili,
Si wote wandani ewe, wengine wafuata mali,
Tahadhari hili jambo, mapenzi asali chungu.

Ni bora ukiridhia, nikikupa huu wosia,
Machozi utayatoa, mdudu kikuingia,
Sipotii tajifia, zitakuua hisia,
Tahadhari hili jambo, mapenzi asali chungu.

FAITH WAIRIMU WERU
Chuo Kikuu Cha Moi (Bewa Kuu)
Mchele wa chenga

Kila kitu napikia

Kuna vitu navipanga, msosi kujipikia,
Mchele ninautwanga, ili chenga kupatia,
Nile mikate ya wanga, ufundi kumiminia,
Chele la chenga pekee, halipiki kitumbua.

Nimekumbuka na keki, chenga waweza tumia,
Sukari ukiipaka, keki tamu wajilia,
Hapo hakuna mashaka, waweza kujitwangia,
Chele la chenga pekee, halipiki kitumbua.

Ukiuhitaji uji, mzuri tena murua,
Weka nazi na maji, chenga nazo watumia,
Muulize Baba Haji, utamu anaujua,
Chele la chenga pekee, halipiki kitumbua.

Sijasahau na wali, chenga nazo kutumia.
Weka nazi kwa umbali, utamu kuusikia.
Kwenye chenga sina swali, kila kitu napikia.
Chele la chenga pekee, halipiki kitumbua.

SULTAN SAID
‘Bongo Tata’
Vijibweni, Dar es Salaam

Yupi bora wa kupenda

Yangu kalamu meshika, mengi kuwaulizeni,
Ni nani wa kupendeka, naomba nielezeni,
Kwa mwongo nimeteseka, wa kupenda sibaini,
Wadau ninauliza, yupi bora wa kupenda.

Wengi tumechangamana, vipusa nimemanya,
Urembo waonekana, machoni wanikanganya,
Mnambie ubayana, msiwe wa kunidanganya,
Wadau ninauliza, yupi bora wa kupenda.

Wadau mnijuzeni, vipi na wapi nipate,
Asiye na afkani, mapenzi pasi kitete,
Maisha ya aushini, na yasiwe na ukete,
Wadau ninauliza, yupi bora wa kupenda.

Kaditama nimefika, lenu jibu nasubiri,
Kusubiri sitachoka, hadi nipate abiri,
Sitaweza kwaibika, hata nipewe udhiri,
Wadau ninauliza, yupi bora wa kupenda.

VINCENT OKWETSO
‘Malenga Chipukizi’
MMUST, Kakamega

Heri njema Bab Shali

Yeye kazaliwa leo, yule ndugu Bab Shali,
Ndipo mie Kipepeo, kwa kutunga sijafeli,
Natunga bila cheleo, kwa ndugu ninomjali,
Heri njema Bab Shali, sikuyo ya kuzaliwa.

Alinipa kichocheo, ndugu Mohammed Shali,
Keshatunga bila ndweo, nikabakia Aseli,
Ndiposa leo macheo, tungo ninalinakili,
Heri njema Bab Shali, sikuyo ya kuzaliwa.

Chereko bila pweleo, ipo kote kwelikweli,
Na tungo la mapokeo, laimbwa na kina Ali,
Kisha pale kwa mleo, ni sauti ya Aseli,
Heri njema Bab Shali, sikuyo ya kuzaliwa.

Twaandaa kitoweo, cha mbuzi halafu wali,
Kisha keki za kileo, twaandaa kikamili,
Usubiri matokeo, sio moja sio mbili,
Heri njema Bab Shali, sikuyo ya kuzaliwa.

BOAZ ASELI
‘Ustadh Kipepeo’
Kitale

Ukiachwa achika!

Yaweje wewe huchoki, kufuata kiso chako?
Ulivyo kupe hung’oki, wasema bado ni wako,
Nasema huambiliki, wayapuza macho yako,
Ukiachwa tu achika, usife tukakuzika.

Huchoki kumpigia, simu asozipokea,
Mlango kimbishia, kufuli nakuwekea,
Wengine wanaingia, huku we wajionea,
Ukiachwa tu achika, usife tukakuzika.

Mitandaoni wamwona, ana wengi wenye hali,
Hivyo wanavyoshikana, zieleweshe akili,
Sana umekondeana, huku wajua ukweli,
Ukiachwa tu achika, usife tukakuzika.

Hamnazo ni za nini, hizo unazojitia?
Utatendwa hadi lini, na mapenzi kujutia?
Hebu toka uvundoni, wapo wema nakwambia,
Ukiachwa tu achika, usife tukakuzika.

DENNIS SHONKO
‘Sonko’
Naivasha

Twaishi na wasiwasi

Watu wanaangamia, wanafa kila wakati,
Ni jamii tunalia, twaachwa na hatihati,
Sisi sote tunajua, hatuna kamwe kismati,
Kifo hakina huruma, twaishi na wasiwasi.

Marafiki wanakufa, wazazi wanatuacha,
Kimezidisha maafa, hadi akina galacha,
Kimebomoa na ufa, ni shida kunapokucha,
Kifo hakina huruma, twaishi na wasiwasi.

Wale tunaowaenzi, watuacha kwa huzuni,
Tunaishi kama panzi, mauko ndiyo kiini,
Chatenganisha wapenzi, watu wengi taabani,
Kifo hakina huruma, twaishi na wasiwasi.

Sisi sote tujipange, tusitekwe na machungu,
Kwa hivyo mniunge, tumekingwa na ukungu,
Hivyo basi msiringe, sisi viumbe vya Mungu,
Kifo hakina huruma, twaishi na wasiwasi.

LIONEL ASENA VIDONYI
‘Malenga Kitongojini’
Shule ya Upili ya Seeds

Mapenzi yamebadilika

Mahaba meadimika, vimesalia vilio,
Yaandamwa na wahaka, mapenzi ya hivi leo,
Sumu yamebadilika, twauwana hivi leo,
Jihadhari na mapenzi, yasije yakatuponza.

Chimbeni visima vyenu, mizinga pia chongeni,
Teka maji yalo yenu, ya wenyewe yaacheni,
Lango lilo wazi lenu, lofungika singieni,
Jihadhari na mapenzi, yasije yakatuponza.

Yamegeuka kinaya, mauko siyo mapenzi,
Kitokea la ubaya, jadili kama wapenzi,
Hasira kitu kibaya, metudhuru zote enzi,
Jihadhari na mapenzi, yasije yakatuponza.

Tamati sasa nafika, fuoni natia nanga,
Mtimani mebondeka, kwa mahaba ya upanga,
Ombi langu kwa rabuka, tukomboe kwalo janga,
Jihadhari na mapenzi, yasije yakatuponza.

MIKE SIMIYU
Naivasha

You can share this post!

Droo moto Ulaya Manchester United, Arsenal wakipangwa na...

SHANGAZI AKUJIBU: Dada ya mpenzi wangu ananipa umbea dhidi...

adminleo