• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Raila sio rika lako, Mishi Mboko amwambia Murkomen

Raila sio rika lako, Mishi Mboko amwambia Murkomen

MOHAMED AHMED na CHARLES WANYORO

BAADHI ya viongozi wanaounga muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, wamewasuta viongozi wa karibu wa Naibu Rais William Ruto, dhidi ya kuhusisha siasa katika vita dhidi ya ufisadi.

Viongozi wa Meru waliwafokea baadhi ya viongozi wa chama cha Jubilee wanaopinga muungano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga huku mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko jana akimtahadharisha seneta wa Elgeyo-Marakwet, Kipchumba Murkomen dhidi ya kuliingiza jina la kinara wa ODM Raila Odinga, katika mazungumzo ya uchunguzi wa sakata hiyo.

Viongozi hao akiwemo waziri wa Biashara, Bw Peter Munya, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na mbunge wa Igembe Kaskazini, Bw Maoka Maore walisema kuwa muafaka wa viongozi hao wawili tayari umeleta matunda hususan katika vita dhidi ya ufisadi na kuleta nchi pamoja.

Walizungumza katika ibada ya wafu ya marehemu Mzee Samson M’Mucheke M’Maroo, katika shule ya msingi ya Keiya.

Bw Munya alisema kuwa si sawa kwa kiongozi yoyote yule kutaka kuvunja muungano huo kwa ajili ya matakwa yake ya siasa za 2022.

“Sasa tunalenga maendeleo na sio vile siasa za usoni zitakavyofanywa. Tulimaliza siasa hivi majuzi na bado ahadi zilizotelewa hazijamalizika kufikia wananchi. Hakuna kiti cha mtu, huwezi kusema unasukumwa nje ili usipate kiti fulani,” akasema Bw Munya.

Bw Maore alimshutumu Bw Ruto kwa kutuma viongozi wake kutoa cheche za maneno dhidi ya Bw Kinoti na Bw Odinga.

“Wale wanaopiga vita Bw Raila ama Bw Kinoti watambue kuwa wanampiga vita Rais Kenyatta. Kama watu wako wa karibu wanatoa cheche za maneno dhidi ya Rais Kenyatta ni lazima uwakanye. Rais Kenyatta anapaswa kuheshimiwa,” akasema Bw Maore.

Raila sio rika lako

Bi Mishi Mboko kwa upande wake alihoji ni kwa nini viongozi hao wameonekana kuingiwa na wasiwasi kuhusiana na uchunguzi huo.

“Kila mkisimama kwenye majukwaa mnazungumzia sakata hii na utaskia jina la Raila ndani. Mimi nataka kumwambia Murkomen aachane na Raila. Raila sio rika lake kwenye siasa wala umri,” akasema Bi Mboko katika kikao na wanahabari eneo la Mama Ngina.

Bi Mboko alisema inashangaza ni kwa nini viongozi wa eneo la Bonde la Ufa wamedai kulengwa kwenye sakata hiyo ilhali kumekuwa na sakata nyingi za ufisadi.

Alisema ni lazima Bw Murkomen ajitokeze mbele kwenye taasisi husika kueleza kile anachojua kuhusiana na sakata hiyo ya mabwawa.

“Sio kuzungumza kando kando, kama kuna kitu unajua kuhusiana na uchunguzi huo jitokeze mbele utuambie maana sisi kama Wakenya tunataka kuelewa kuhusiana na mabilioni hayo ya pesa yaliyopotea,” akasema Bi Mboko.

Alisema madai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinasukumwa na siasa ni mbinu ya kutaka Wakenya wasifuatilie kashfa hiyo ya mabwawa.

“Na hatutokubali kuona mkileta mbinu za kutaka Wakenya waachane na suala hili. Hatuwezi kuwacha siasa kuingizwa mahali pasipofaa. Kama mnataka siasa subirini 2022 na mtajua yale yaliopangwa lakini kwa sasa tunataka huduma kwa watu wetu ambazo haziwezi kupeanwa kama tutazungukwa na ufisadi,” akaongeza.

You can share this post!

Binamu ya Uhuru afagia kondoo wote sokoni

Pipeline na Prisons zaanza vizuri voliboli Cairo

adminleo