• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:55 PM
Messi afungia Barcelona ‘hat trick’ ya 33 La Liga

Messi afungia Barcelona ‘hat trick’ ya 33 La Liga

Na MASHIRIKA

BARCELONA, UHISPANIA

LIONEL Messi alifunga mabao matatu katika ushindi wa 4-1 uliosajiliwa na Barcelona dhidi ya Real Betis kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mwishoni mwa wiki jana.

Mbali na kutawaliwa na kiu ya kulipiza kisasi dhidi ya Betis waliowazidi maarifa katika mchuano wa mkondo wa kwanza, Barcelona walikuwa na ulazima wa kufungua mwanya zaidi kileleni mwa jedwali.

Kikosi hicho ambacho kwa sasa kinanolewa na mkufunzi Ernesto Valverde kinaselelea kileleni kwa alama 66 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na Atletico Madrid ambao wanashikilia nafasi ya pili.

Fowadi Lionel Messi (kulia) wa Barcelona apiga mkwaju kufunga bao Machi 17, 2019, Barcelona ilipolipiza kisasi dhidi ya Real Betis uwanjani Benito Villamarin mjini Seville. Picha/ AFP

Real Madrid ambao wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya mkufunzi Zinedine Zidane, wanashikilia nafasi ya tatu 54, nane zaidi kuliko Getafe wanaofunga mduara wa nne-bora.

Bao jingine la Barcelona lilipachikwa wavuni na fowadi matata mzawa wa Uruguay, Luis Suarez kunako dakika ya 63.

Betis walifutiwa machozi mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Loren Moron.

Ilikuwa mara ya 33 kwa Messi kufunga jumla ya mabao matatu kutokana na mchuano mmoja akivalia jezi za Barcelona katika kampeni za La Liga.

Mvamizi huyo mzawa wa Argentina alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 18 kupitia mpira wa ikabu uliomzidi maarifa kipa Pau Lopez.

Chombo cha wageni chayumbishwa

Barcelona na Messi walikiyumbisha zaidi chombo cha wageni wao ambao waliwakomoa 4-3 ugani Nou Camp mnamo Novemba kwa kufunga mabao matatu ya haraka katika dakika za 45, 63 na 85 mtawalia.

Katika mechi nyinginezo za La Liga mnamo Jumapili, Eibar walitandikwa 2-1 na Real Valladolid huku Sevilla wakiwapokeza Espanyol kichapo cha 1-0. Valencia walilazimishiwa sare tasa na Getafe mbele ya mashabiki wao wa nyumbani nao Villarreal wakawapepeta Rayo Vallecano 3-1.

Mnamo Jumamosi, Gareth Bale na Isco waliwafungia waajiri wao Real mabao muhimu yaliyotosha kumwanzishia vyema kocha Zinedine Zidane awamu ya pili ya ukufunzi wake ugani Santiago Bernabeu.

Ushindi huo wa Real dhidi ya Celta Vigo mnamo Jumamosi uliwadumisha katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 54, mbili pekee nyuma ya Atletico Madrid.

Chini ya mkufunzi Diego Simeone, masaibu ya Atletico waliobanduliwa na Juventus kwenye kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wiki jana, yaliendelea zaidi. Kikosi hicho kilipepetwa 2-0 na Athletic Bilbao ambao walipaa hadi nafasi ya tisa kwa alama 37.

Isco aliyekosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Real chini ya kocha Santiago Solari aliyefutwa majuzi, aliwafungulia waajiri wake ukurasa wa mabao baada ya kushirikiana vilivyo na Karim Benzema kunako dakika ya 62.

Dakika 13 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa, Bale ambaye ni mzawa wa Wales aliyumbisha kabisa chombo cha wenyeji wao kwa kufunga bao la pili.

Kwa Zidane na kikosi chake cha Real ni kuhakikisha kwa sasa kinasajili ushindi katika takriban mechi zote zilizosalia ili kujikweza pazuri jedwalini mwishoni mwa msimu huu.

Hakika, kufikia sasa, matumaini ya Real ya kutia kapuni ubingwa wa taji lolote msimu huu yamedidimia sana hasa ikizingatiwa kwamba ni pengo la alama tisa ambalo kwa sasa linadumu kati yao na viongozi wa La Liga, Barcelona.

Wakinolewa na Solari ambaye alimrithi Julen Lopetegui aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu jana, Real walibanduliwa kwenye kipute cha Copa del Rey majuma machache kabla ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi kuwadengua kwenye kivumbi cha UEFA wiki jana.

Zidane alipoagana na Real yapata miezi 10 iliyopita, alikuwa amewashindia miamba hao mataji matatu ya UEFA na ufalme wa La Liga mara moja.

Real walitambishwa pia na Cristiano Ronaldo ambaye kwa sasa anavalia jezi za Juventus nchini Italia.

Mbali na Isco, wachezaji wengine wanaotazamiwa kuyafufua makali ya chini ya Zidane ni Marcelo, Bale na kipa Keylor Navas ambao kwa sasa wamerejeshwa katika kikosi cha kwanza.

Anapolenga kukisuka upya kikosi chake, Zidane amefichua azma ya kumsajili kiungo Raheem Sterling wa Manchester City mwishoni mwa msimu huu.

Kulingana naye, ujio wa Sterling utafufua pakubwa safu ya uvamizi ya timu hiyo ambayo imekosa makali tangu Ronaldo aondoke.

Real ambao wako radhi kumpa Zidane kiasi cha Sh42 bilioni ili awanie pia huduma za Neymar, Eden Hazard, Kylian Mbappe na Christian Eriksen.

You can share this post!

Gor kumjua Jumatano mpinzani wao wa nane-bora katika CAF

Everton wacharaza Chelsea na kuweka Sarri padogo Stamford

adminleo