• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Chipukizi wa raga kupigania ubingwa wa Afrika Julai

Chipukizi wa raga kupigania ubingwa wa Afrika Julai

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za raga za wachezaji saba kila upande za chipukizi za Kenya zitawania ubingwa wa Afrika katika mashindano ya African Youth Games mnamo Julai 18-28, 2018.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Raga la Afrika (Rugby Africa), Kenya ni miongoni mwa mataifa 22 yaliyojiandikisha kushiriki makala haya ya tatu.

“Nashukuru kamati za kitaifa za Olimpiki za Afrika (ANOCA) kwa usaidizi wao wa katika usajili wa timu zitakazoshiriki mashindano ya chipukizi mwezi Julai. Ni kwa sababu yao tumeweza kupata ithibati kutoka kwa mataifa 22,” amesema Rais wa Rugby Africa, Abdelaziz Bougja. Mashindano haya yatahusisha wachezaji walio chini ya umri wa miaka 18.

Kenya ilizoa jumla ya medali 25 (saba za dhahabu, 11 za fedha na saba za shaba) katika makala ya mwaka 2014. Kutoka idadi hiyo ya medali, Kenya ilijishindia fedha katika raga ya wachezaji saba kila upande ya wavulana. Kenya ilizabwa 60-0 na Afrika Kusini katika fainali jijini Gaborone nchini Botswana.

Orodha ya mataifa yatakayoshiriki:

Timu za wavulana

Kenya, Algeria, Benin, Burkina Faso, Burundi, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ivory Coast, Madagascar, Mauritius, Morocco, Namibia, Sierra Leone, Afrika Kusini, Tunisia, Zambia na Zimbabwe.

Timu za wasichana

Kenya, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Madagascar, Morocco na Tunisia.

You can share this post!

Kipsang’ alenga tena kuvunja rekodi ya dunia kwenye...

Gor kumenyana na mahasidi wa Tunisia Klabu Bingwa Afrika

adminleo