• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
KAULI YA WALIBORA: Prof Chimera hana mfano kwa kujitoa sabili kukuza lugha

KAULI YA WALIBORA: Prof Chimera hana mfano kwa kujitoa sabili kukuza lugha

Na KEN WALIBORA

NILIPANDA basi wiki iliyopita kuenda zangu Kilifi kuitika mwaliko wa wanafunzi wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Pwani.

Walikuwa wamenialika mwaka 2018 nikapanda basi hadi Athi River safari ikakorofishika nikarudi Nairobi.

Mto Athi ulikuwa umefurika na maji kuziba barabara.

Mara hii nilitaka kufika, ima fa ima na Mungu ni mkubwa nilifika salama u salimini katika mji wa Kilifi.

Naam, nilifika chuoni humo kulipa deni la kutofika kwangu mwaka 2018.

Nilipokewa kwa vilili na vigoma na viongozi wa chama wakiongozwa na Nicholas Onyango na Fatuma.

Walikesha wakinisubiri, nami nilifika alfajiri ambapo vijana wao walipaswa kuwa wanalala usingizi wa pono. Walikesha kwa ajili yangu.

Kama nilihofia kwamba watu wema walikuwa wamekwisha duniani, mapokezi ya vijana hao pwani yalinithibitishia kwamba si kweli.

Duniani bado wapo watu wema. Nilikaa kwenye kongomano lao kwa utuvu na kusikiliza jinsi wanavyowasilisha mada zao mbalimbali.

Ukiwasikiliza tu, unang’amua kwamba Kiswahili kina mustakabali mwema. Ni vijana waliohamasishwa wakahamisika, walioshajiishwa wakashajiika kukiendeleza Kiswahili.

Nilijawa na matumaini, fahari na furaha kwa kauli zao na namna walivyozitoa.

Hapo ikanijia fikira kwamba hawawezi kuwa na mwelekeo chanya na hamasa kiasi hicho bila kuelekezwa vyema.

Naye Prof Rocha Muzungu Chimera kwa kweli amekuwa nguzo na dira kwao.

Mwandishi huyu wa ‘Nyongo Mkalia Ini’, ‘Mnara Unawaka Moto’ na ‘Siri Sirini’, ni kielelezo chema cha namna ya kuwahamisha vijana kukipenda Kiswahili.

Niliona jinsi wanafunzi hao wanavyompenda mwalimu wao na kutangamana naye kama mzazi na mlezi wao halisi.

Kiasi cha kukukumbusha kwamba Prof Chimera alishirikiana na Prof Kimani Njogu kukiandika kitabu cha ‘Ufundishaji wa Fasihi ya Kiswahili’ kilichoibuka mshindi wa tuzo ya Noma kwa kuwa kitabu bora kote barani Afrika mnamo 2002.

Aidha, kitabu chake cha Kiswahili: ‘Past Present and Future Horizons’ kimeteuliwa kuwa miongoni mwa vitabu mia moja bora zaidi barani Afrika.

Riwaya ndefu zaidi

Aidha, huenda ikawa kwa majuzuu yake matatu ya ‘Siri Sirini’, Prof Chimera ndiye mwanariwaya aliyewahi kuandika riwaya ndefu zaidi barani Afrika.

Kwa hilo nampa mkono wa tahania.

Ila zaidi nampongeza kwa kutufinyangia kizazi kipya cha maashiki wa Kiswahili ambao nao wataendelea kutoa mchango wao katika kuchapua ukuzaji wa lugha hii adhimu.

Kama nilivyotaja katika hotuba yangu kwenye kongomano hilo, ni muhimu kwa Chuo Kikuu cha Pwani kuwa mstari wa mbele katika taaluma za Kiswahili hasa kutokana na historia na utamaduni na mahali kilipo kijiografia.

Ni muhimu kwa chuo hicho kufinyanga akina Rocha Chimera wengi wengine ili kutajirisha turathi zetu za Kiswahili.

Nionavyo mimi, vijana wanapaswa kuhamasishwa na kushajiishwa ipasavyo kama ambavyo juhudi za Prof Chimera zinavyobainisha bayana.

Tusijipe shughuli nyingi mno, tusijipurukushe mno kiasi cha kwamba hatuna muda kabisa wa kuwapa shime vijana katika safari zao za maisha. Hilo ndilo funzo nililotoka nalo Pwani.

“Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara”

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Job Mokaya

KAULI YA MATUNDURA: Mpya kabisa! Kamusi Pevu ya Kiswahili...

adminleo