• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Serikali yakana njaa imeua Wakenya, madaktari wataka uchunguzi ufanywe

Serikali yakana njaa imeua Wakenya, madaktari wataka uchunguzi ufanywe

MOHAMED AHMED Na AGGREY OMBOKI

SERIKALI ikiongozwa na Naibu Rais William Ruto, imesisitiza hakuna Mkenya yeyote aliyepoteza maisha kwa kukosa chakula.

Pia machifu wote ambao wamesambaza habari za vifo vinavyotokana na njaa wataadhibiwa vikali, akasema Dkt Ruto.

Maoni hayo yaliungwa mkono na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i akiongea kwenye Kameme FM Jumatano asubuhi na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa akihojiwa katika Citizen TV.

Vigogo hao wa serikali wamewalaumu wanasiasa, machifu na wanahabari kwa madai ya kueneza uvumi na kuzua taharuki.

Serikali inasisitiza waliokufa waliaga kutokana na magonjwa wala si njaa.

Kwa upande wao, madaktari wamependekeza uchunguzi ufanyike kujua kiini cha vifo hivyo.

Daktari Eric Njenga wa hospitali ya Aga Khan alisema badala ya majibizano kuna haja ya kuchunguza sababu ya vifo hivyo.

“Kuna haja ya kujua kilichoua watu hao. Maradhi kama ukimwi na saratani yanaweza kufanya watu kudhoofika. Njaa pia inaweza kusababisha hali hiyo,” akasema Dkt Njenga

Akiongea jijini Mombasa jana, Dkt Ruto alipinga ripoti kwenye vyombo vya habari kuwa watu zaidi ya 10 wamefariki kuhusiana na baa hilo huku akiwalaumu wale wanaotatizia juhudi za serikali kutekeleza mradi wa mabwawa, ambao alisema unalenga kupambanana na shida hiyo siku za usoni.

“Kumekuwa na taarifa nyingi za uwongo kuhusiana na yale yamekuwa yakitokea. Tumeambiwa kuwa watu 11 wamefariki lakini hilo sio kweli. Hakuna mtu yeyote ambaye amefariki, na sisi kama serikali tunafanya juhudi zote kuhakikisha kuwa hakuna mtu atafariki kwa sababu ya ukame,” akasema Dkt Ruto.

“Hakuna kifo chochote ambacho kimethibitishwa kusababishwa na njaa,” akasema Bw Wamalwa.

Walisema hayo huku Gavana John Lonyangapuo wa Pokot Magharibi akithibitisha kuwa watu wawili wamefariki katika eneo hilo.

MCA wa Silale, katika Kaunti ya Baringo, Bw Nelson Lotela naye alisisitiza kuwa kunao wakazi waliokufa: “Nashangaa kwa nini serikali inakanusha habari za watu kufa kwa njaa, ilhali sisi watu wa mashinani tuna ushahidi kuwa watu wanakufa kwa njaa.”

Wanahabari wa Taifa Leo waliokuwa mashinani katika maeneo ya Oropoi na Nawountos katika Kaunti ya Turkana mnamo Jumanne, walieleza kuwa wakazi wengi wamehama makwao kwenda kutafuta chakula, maji na malisho ya mifugo wao.

“Wazee wasio na uwezo wa kutembea ndio wameachwa nyumbani. Wengi wamedhoofika sana,” alisema mpiga picha Jared Nyataya.

Wanahabari hao pia walishuhudia msongamano mkubwa katika shule kutokana na kuwa hata watoto ambao hawahatimiza umri wa kwenda shuleni sasa wanaenda, ili waweze kupata chakula kinachopewa wanafunzi.

Dkt Ruto alisema machifu wote ambao wamefichua habari za vifo vinavyotokana na njaa kwenye vyombo vya habari, tayari wanahojiwa kuhusiana na madai hayo.

Naye Dkt Matiang’ia alisema chifu aliyefichua mara ya kwanza kuhusu watu kufa kwa sababu ya njaa alifutwa kazi kitambo. Hii ni licha ya kuwa chifu huyo, Jack Ronei wa kata ya Kositei, ameagizwa kufika makao makuu ya kamishna wa Baringo kuandikisha taarifa kuhusu taarifa alizotoa kwa wanahabari.

Dkt Ruto alisema hakuna uhaba wa chakula nchini, bali shida kuu ni kufikisha vyakula hivyo katika kile pembe ya nchi: “Hatuna uhaba wa chakula. Tupo na chakula cha kutosha. Tayari tunatekeleza juhudi tukishirikiana na washikadau kufikisha vyakula hivyo kila pembe ya nchi.”

“Suluhisho la kudumu ni ujenzi wa mabwawa ambayo sisi kama serikali tayari tumeanzisha mpango wa kujenga mabwawa 57 katika maeneo tofauti ya nchi,” akasema.

Alisema hata hivyo, ujenzi huo wa mabwawa umekumbwa na changamoto ikiwemo madai ya ufisadi: “Tuko na mabwawa ambayo tunataka kujenga lakini kama munavyojua kumekuwa na watu ambao wanatatiza malengo yetu ya kutekeleza mradi huo,” akaongeza.

Alisisitiza kuwa pesa za kujenga mabwawa ya Arror and Kimwarer hazijapotea na mradi utatekelezwa.

“Haiwezekani ati iwe serikali imepoteza Sh21 kwa mara moja. Hii serikali inaendeshwa na watu wanaojifahamu. Hii sio karata. Kisha mtu ananiuliza ni kwa nini ninataka kujua kuhusu mambo ya mabwawa. Lazima nijue kwa sababu mimi ndiye bosi mdogo wa kampuni hii inayoitwa Kenya,” akasema.

You can share this post!

AKILIMALI: Ukistaajabu ya kuku wa kienyeji basi hujui ya...

AKILIMALI: Mtambo wa kuangua mayai umeimarisha idadi ya kuku

adminleo