• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Matiang’i awakemea maafisa waliomuaibisha Lamu

Matiang’i awakemea maafisa waliomuaibisha Lamu

NA KALUME KAZUNGU

WAZIRI wa usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i Alhamisi aliwakemea watumishi wa umma eneo la Lamu kwa uvivu ambao ulipelekea yeye kuaibishwa hadharani na wananchi waliokuwa wakitoa malalamishi kuhusu utendakazi wa maafisa hao.

Wakati wa mkutano ulioandaliwa eneo la Mkunguni na kuhudhuriwa na Waziri Matiang’i, wananchi waliopewa fursa ya kuzungumza walichukua nafasi kumuomba Dkt Matiang’i kuwasaidia kutatua matatizo yanayowakumba ambapo mengine yalichangiwa na polisi na maafisa wa utawala eneo hilo.

Baadhi ya akina mama walitoa machozi wakati wakiwasilisha malalamishi kwa Bw Matiang’i.

Miongoni mwa malalamishi hayo ni ukiukaji wa haki za binadamu na dhuluma zinazoendelezwa na polisi dhidi ya wananchi wa Lamu, tatizo la ardhi, ikiwemo ukosefu wa hatimiliki, unajisi wa watoto na ubakaji, kupotezwa kwa vijana bila mpango na utepetevu wa polisi katika kukabiliana na matatizo punde wanaporipotiwa vituoni na wananchi.

Wakati aliposimama kuhutubia umma, Waziri Matiang’i alieleza kughadhabishwa kwake na malalamishi ya wakazi na akawanyoshea kidole cha lawama maafisa wa umma, ikiwemo polisi na wakuu wa utawala eneo hilo kwa kutowajibikia masuala yanayoathiri wananchi.

Alisema malalamishi yote yaliyowasilishwa na wananchi yalifaa kuwa yametatuliwa na wawakilishi wa serikali ya kitaifa walioko Lamu.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i akihutubia wakazi eneo la Mkunguni mjini Lamu Alhamisi. Ameamuru wavuvi zaidi ya 6000 wasajiliwe kwa njia ya kielektroniki na kuruhusiwa kuvua samaki usiku. Picha/ Kalume Kazungu

Alitaja maafisa hao kuwa wazembe, hatua ambayo katu hataruhusu iendelee.

“Hatuwezi tena kuvumilia uzembe kama huu. Ninakuja hapa mbele ya wananchi kuaibishwa kwa kuletewa malalamishi ambayo yangetatuliwa zamani hapa. Lazima kama watumishi wa umma tufanye kazi ambayo tumepewa. Hatuwezi kuacha wananchi kuhangaika bure wakitafuta huduma ilhali sisi tuko hapa na tunakula mishahara ambayo ni hawa wananchi wanatufadhili. Hilo ni jambo ambalo lafaa tulikemee. Iwe ni polisi, afisa wa utawala, sote lazima tufanye kazi vile tunapaswa,” akasema Bw Matiang’i.

Wakati wa hotuba yake, Bw Matiang’i aliwaita Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, Bw John Elungata, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono na Kamanda wa Polisi Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi na kuwaamuru kuhakikisha kuwa kufikia Jumatatu wanakuja pamoja na kuweka mkutano wa moja kwa moja na wananchi ili kupokesa malalamishi yao na kuyatatua.

“Ikiwa huwezi kazi, basi haina haja sisi tuendelee kukuweka hapa. Nataka kufikia Jumatatu wewe Mshirikishi wa Usalama Ukanda huu wa Pwani uje hapa Lamu kukutana na Kamishna na pia machifu wote wa hapa. Mwandae kikao na hawa wananchi ili watoe malalamishi yao kwenu na mtafute suluhu ya matatizo hayo,” akasema Bw Matiang’i.

Aliwataka wananchi kutoogopa kutoa shida zao kwa watumishi wa umma ili waweze kupaa suluhu ya haraka badala ya kusubiri hadi mawaziri waje mashinani.

Aidha aliwapongeza wakazi wa Lamu kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha maendeleo ya kitaifa yanaafikiwa eneo hilo.

Kwa upande wake aidha, Mshirikishi wa Usalama, Ukanda wa Pwani, Bw John Elungata, aliahidi kuwaleta karibu zaidi wananchi si wa Lamu tu bali kaunti zote sita za Pwani ili kuona kwamba suluhu inapatikana kwa matatizo yao.

“Sitaki kuwe na mwanya wowote kati ya maafisa wa umma na raia. Hii ndiyo sababu nikaamua kupeana nambari yangu ya simu ili ukiwa na lolote kuwa huru kunijulisha ili tusaidiane kutatua,” akasema Bw Elungata.

You can share this post!

Mchina aponea kifo baada ya kujidunga sindano ya juisi...

Aililia mahakama baada ya kutisha kumuua bawabu

adminleo