• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
KINAYA: Jenerali Miguna Miguna atarudi Kenya akiwa shujaa wa Jubilee

KINAYA: Jenerali Miguna Miguna atarudi Kenya akiwa shujaa wa Jubilee

Na DOUGLAS MUTUA

Kwa ufupi:

  • Bwana Miguna aliyeondoshwa nchini akifanana na kinyago, atarejea kama shujaa na atapokelewa kama mheshimiwa
  • Paspoti ya ‘Jenerali Miguna Miguna’ imeraruliwa, ndiyo. Sikatai. Lakini itashonwa. Na nani? Walioirarua. Kwa nini? Anawatumikia
  • Sasa ‘Baba’ hamwamini ‘Jenerali Mwitu’ huyo kwa maana hajui kufunika kombe mwanaharamu apite
  • Utengano wa wakuu wa NASA ndiyo dua ya Jubilee.  Waliomtishia ‘Bwana Tikitimaji’ kutoka Ukambani akaogopa uapisho hawakukoma hapo

‘JENERALI’ wa National Resistance Movement (NRM) Kenya atarejea nchini kama shujaa wa Jubilee.

Ala! Vipi tena? Waliomfurusha nchini wameafikia malengo yao, sasa wanatabasamu kila wakati akitajwa. Hawana chuki naye.

Imekuwaje tena? Nyufa alizosababisha katika chungu kiitwacho National Super Alliance (NASA) zikipanuka zaidi na kitakuwa vigae.

Hivyo basi? Bwana huyo aliyeondoshwa nchini akifanana na kinyago – huku kavalia suti na sapatu – atarejea kama shujaa na atapokelewa kama mheshimiwa.

Aliyeondoshwa nchini na karatasi ya sandarusi mkononi kama aliyekwenda kwa ‘mama-mboga’ atabebewa mkoba na kusindikizwa hadi chumbani mwa watu mashuhuri katika uwanja wa ndege wa JKIA, Nairobi. Kwa maagizo ya nani? Usijali, wagombanao ndio wapatanao.

Waliompigania eti arejeshewe paspoti watakuwa watazamaji tu, sikwambii nusura wajinyonge, lakini hawatamfanyia chochote. Siasa ni mchezo wa wakora.

 

Paspoti itashonwa

Paspoti ya ‘Jenerali Miguna Miguna’ imeraruliwa, ndiyo. Sikatai. Lakini itashonwa. Na nani? Walioirarua. Kwa nini? Anawatumikia. Wanajua kushona matambara.

Iliyoraruliwa ni paspoti ya kawaida tu, kurasa 32, lakini atakayopewa itakuwa ya kidiplomasia, yenye kusara 48.

Kibaraka wa ‘Baba’ na ODM unanilaani na kusema hayo yote yanafanyika katika ulimwengu wangu wa kufikirika.

Labda una ukweli fulani, lakini chochote kinaweza kutokea. Anayenata pamoja kana kwamba kapandikizwa kwa gundi ni wewe mlalahoi msi kitu!

Haya ninayosema yanaweza kufanyika ghafla kama kupepesa jicho kwa maana ‘Baba’ amezeeka, anashauriwa na walafi wasiompenda mlafi mwenzao ‘Jenerali’.

Tatizo kuu ni kwamba anawasikiliza kikamilifu, hadi kiwango cha kumwambia ‘Jenerali’ afyate ulimi, naye haambiliki hasemezeki!

Nilijua tangu mwanzo kwamba ingekuwa vigumu kwa Miguna kuridhiana kikamilifu na kambi ya ‘Baba’. Wangeridhianaje ilhali wanaomzingira ‘Baba’ hawamwamini?

 

‘Jenerali mwitu’

Miguna mwenyewe ni domo-kaya; mwana wa Jaramogi alipomnong’onezea kwamba barobaro fulani kalishwa vitamutamu na Jubilee alianika yote mtandaoni.

Sasa ‘Baba’ hamwamini ‘Jenerali Mwitu’ huyo kwa maana hajui kufunika kombe mwanaharamu apite, anaoamini ni wajanja wanaotegea tu apumue za mwisho wamrithi.

Hofu ilitanda kotekote Miguna aliporejea katika kambi ya ‘Baba’ na uvumi ukaenea kwamba angemrithi kisiasa.

Watu waliomchukia na kumdharau walihoji hana ufuasi wowote, wakapiga mfano wa alipojaribu kuwania ugavana Nairobi akapata kura yake pekee, wakasema haiwezekani!

Lakini walishtuka ghaya ya kushtuka alipojitangaza ‘jenerali’ wa NRM na kuvutia wafuasi wa mbali na karibu.  Sasa waliyemdharau amekuwa tishio, ndiposa wanalilia maini yake.

 

Ni hatari

Tayari wamemsadikisha ‘Baba’ kwamba mtu huyo ni hatari, ‘Baba’ naye pasipo na kuchelewa akawaambia wafuasi wake wayapuuze matamshi ya Miguna, ni porojo.

Huo ni mgawanyiko, ikiwa si utengano wa hakika. Kila mkora wa Jubilee ameweka gunia zima la karanga mbele yake, anatafuna mojamoja huku akijionea sinema bila malipo.

Kumbuka tangu mwanzo utengano wa wakuu wa NASA ndiyo iliyokuwa dua ya Jubilee.  Waliomtishia ‘Bwana Tikitimaji’ kutoka Ukambani akaogopa uapisho hawakukoma hapo.

Utengano ukitokea kabisa NASA, wafuasi watamchukia ‘Baba’ kwa kutotumia nguvu mpya za Miguna kuvumisha vuguvugu lao.

Dua ya Jubilee kwamba ‘Baba’ atengwe itakuwa imejibiwa, wataandaa karamu kusherehekea. Ukialikwa utahudhuria?

 

Baruapepe: [email protected]

You can share this post!

Serikali yalemewa na gharama ya kutunza wafungwa, wale wa...

Agonga mumewe kwa mwiko sababu ya mlo

adminleo