• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Njaa: Wabunge wa ODM wamsuta Ruto

Njaa: Wabunge wa ODM wamsuta Ruto

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa upinzani wameitaka serikali ya kitaifa kuanzisha mikakati ya kudumu ya kukabiliana na ukame nchini huku wakimkashifu Naibu Rais William Ruto kwa kile wamekiita ni kupotosha Wakenya kuhusu idadi ya watu waliofariki kutokana na njaa.

Walisema ni aibu kwa serikali kudai kuwa kuna chakula cha kutosha nchini ilhali chakula hicho hakiwezi kuwafikia wananchi wanaokeketwa na makali ya njaa katika maeneo kame nchini.

“Mbona serikali isitumie magari na hata ndege kusafirisha mahindi kutoka kwetu Trans Nzoia na kuyapeleka hadi kaunti za Turkana, Baringo na maeneo mengine ambako wananchi wanakeketwa na njaa,” akauliza Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa Ijumaa kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Aliandamana na kiongozi wa wachache katika bungeni John Mbadi, Junet Mohamed (Suna Mashariki), Opiyo Wandayi (Ugunja), Lilian Gogo (Rangwe) miongoni mwa wengine.

Bw Mohamed alisema madai ya Dkt Ruto kwamba hamna mtu hata mmoja aliyefariki kutokana na njaa ni ishara tosha kuwa “hajutii masaibu yanayowapata Wakenya.”

“Kwa kudai kuwa  habari za watu kufa kutokana na njaa kuwa feki,  ilhali maafisa wa serikali kama vile machifu wamethibitisha hilo ni kielelezo cha kiongozi asiyeja na aliyekosa umakinifu,” akasema Mbunge huyo wa Suna Mashariki.

Kaunti zilizoathirika na njaa ni; Turkana, Samburu, Marsabit, Garissa, Isiolo, Mandera, Wajir, Baringo, Kilifi, Tana River, West Pokot, Makueni, Kajiado na Kwale.

Ingawa vyombo vya habari vimeripoti kwamba jumla ya watu 11 wamefariki kufikia sasa kutokana na makali ya njaa, Dkt Ruto alisema taarifa hizo sio sahihi na kwamba hamna Mkenya hata mmoja amekufa kutokana na njaa.

Shirika la Msalaba Mwekundi nchini (Kenya Red Cross) pia limetofautiana na kauli ya Dkt Ruto na kuungama kuwa kuna watu waliofariki kutokana na “maradhi yaliyotokana na njaa”.

You can share this post!

Manufaa ya kuendesha baiskeli

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya sera katika upangaji...

adminleo