• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
JAMVI: Handisheki ilivyoibua ubabe wa kisiasa baina ya Orengo na Mbadi

JAMVI: Handisheki ilivyoibua ubabe wa kisiasa baina ya Orengo na Mbadi

NA CECIL ODONGO

MATAMSHI ya Seneta wa Siaya James Orengo ambaye pia ni mwandani wa kinara wa ODM Raila Odinga, kwamba chama hicho kiko tayari kuunda muungano na kile cha Jubilee kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2022, yamezua vita vya ubabe kati yake na Mwenyekiti wa chama John Mbadi.

Seneta huyo akizungumza wakati wa kipindi cha Point Blank katika runinga ya KTN, alidai ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga unalenga kuimarisha uwezo wa kiongozi huyo wa ODM kuingia ikulu kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“ODM inaendea mamlaka ya kisiasa na tunaandaa mikutano hii macho yetu yakilenga uchaguzi wa 2022. Mamlaka haya yatakuja kutokana na ushirikiano kutoka ODM na chama cha Jubilee ambacho Rais Kenyatta anahusika pakubwa,” akasema Bw Orengo.

Hata hivyo, Bw Mbadi alikuwa wa kwanza kujitokeza kupinga madai ya Bw Orengo akisema chama hicho kitawasilisha mwaniaji wa urais kivyake 2022 na hakina ufahamu wowote wa kuwepo kwa mkataba fiche kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Ni mapema sana kwa mtu yeyote kudai anazungumza kwa niaba ya ODM na kudai chama kimeingia makubaliano na chama kingine au mtu binafsi. Chama kitakuwa na mwaniaji uchaguzi mkuu ujao ila bado hatujui wapinzani wetu wala miungano itakayoundwa,” Bw Mbadi akamjibu seneta huyo.

Hata hivyo, imebainika kwamba kiini cha uhasama kati ya Bw Orengo ambaye ni Kiongozi wa wachache kwenye Bunge la Seneti na Bw Mbadi ambaye anashikilia wadhifa huo katika Bunge la Kitaifa ni uwaniaji wa viti vya Ugavana vya Kaunti za Siaya na Homa Bay mtawalia.

Bw Mbadi ambaye amehudumu kama mbunge wa Suba Kusini tangu 2007, ametangaza hadharani kuwa yupo kwenye kiny’ang’anyiro cha kutwaa ugavana wa Homa Bay baada ya muda wa kuhudumu wa gavana wa sasa Cyprian Awiti kukamilika.

Ingawa, Bw Orengo hajatangaza waziwazi kuwa atakuwa debeni kumrithi Gavana wa sasa Cornel Rasanga Amoth, kumeibuka madai kwamba viongozi hao wawili wanapanga kubadilishana viti katika kaunti hiyo. Vilevile kumeibuka madai Bw Mbadi anampigia upatu Mbunge wa zamani wa Rarieda Nichols Gumbo kutwaa ugavana wa Siaya, jambo ambalo halifurahishi kambi ya Bw Orengo.

Ingawa hivyo, Bw Mbadi ameonekana kuingiwa na baridi kwenye azma yake baada ya aliyekuwa mwaniaji wa ugavana wa Homabay Joseph Oyugi Magwanga kuonyesha dalili za kurejea chamani baada ya kukihama na kusimama kama mwaniaji huru mwaka wa 2017.

Uvumi kuwa Bw Magwanga aliyedai kupokonywa ushindi wa kiti hicho yupo pua na mdomo kurejea ODM ulishamiri mwezi Februari alipojitokeza katika Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu kuungana na familia ya Bw Odinga katika hafla ya ukumbusho wa miaka 25 tangu kifo cha babake waziri huyo mkuu wa zamani marehemu Jaramogi Oginga Odinga.

Bw Magwanga vilevile anasifiwa kutokana na rekodi ya kupigiwa mfano ya maendeleo alipohudumu kama mbunge wa Kasipul na hilo lilidhihirika aliposhindwa pembamba na Bw Awiti kwa kura chache katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Hata hivyo, akizungumza na meza ya Jamvi , Bw Mbadi alikanusha kwamba uhusiano kati yake na Bw Orengo umeingia doa, akisisitiza kurejea kwa Bw Magwanga chamani hakumtishi kamwe.

“Vyombo vilifasiri visivyo usemi wangu kuhusu kauli niliyotoa kukanusha madai ya Seneta Orengo kwamba chama chetu kimeingia mkataba na Jubilee kuhusu uchaguzi wa mwaka wa 2022. Kama mwenyekiti na msemaji wa ODM, nilikuwa natoa msimamo wa chama na sina chuki na Bw Orengo kuhusu hilo, sisi ni marafiki sana,”

“Hata hivyo, kurejea kwa Bw Magwanga chamani hakunitishi kwa sababu ni haki yake ya kidemokrasia kusimama. Ukichunguza kwa makini, mimi ndiyo nimekuwa nikimrai Bw Magwanga arejee chamani na kama mwanasiasa wa miaka mingi niko tayari kukutana naye debeni. Mimi si mwoga na niko tayari kukabiliana naye akirudi chamani,” akasema Bw Mbadi.

Mbunge huyo wa Suba Kusini hata hivyo, alikanusha kuwa analenga kumhujumu marejeo ya Bw Magwanga kwenye chama hicho na kutumia nafasi yake ya uenyekiti kujivumisha kama mwaniaji anayeungwa mkono na Bw Odinga.

“Ndiyo najua kwamba kutwaa tiketi ya ODM ni kama kushinda uchaguzi eneo la Luo Nyanza lakini siogopi kushindana na mtu yeyote hata awe ni Bw Magwanga. Pia kumbuka Gavana wa Migori Okoth Obado alishinda kiti hicho mwaka wa 2013 bila kutumia ODM. Mimi niko uwanjani na nitapigania kiti hicho kama wengine,” akaongeza Bw Mbadi.

Kuonyesha kwa hali si hali ODM, Bw Orengo amekuwa akiongoza kampeni za kumpigia debe mwaniaji wa ODM kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ugenya huku Bw Mbadi, anayeshikilia wadhifa muhimu chamani akihepa kampeni hiyo.

Hata hivyo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anampuuza Bw Mbadi kama mwanasiasa anayemlenga Bw Orengo ili kujiinua kisiasa baada ya kugundua kwamba ana nafasi finyu ya kushinda kiti cha ugavana, Bw Magwanga akiwania.

Bw Andati anasema Bw Orengo ambaye pia ni wakili wa miaka mingi wa familia ya Bw Odinga, anajua anachokisema kwa sababu Rais Kenyatta au Bw Odinga hawajajitokeza kupinga kauli aliyoitoa kuhusu siri ya kushirikiana kwao.

“Ikiwa Bw Mbadi anataka kuchimba kaburi lake la kisiasa basi adhubutu kuonyeshana ubabe na Bw Orengo anayeaminiwa zaidi na kinara huyo wa ODM. Hafai kabisa kuhusisha wakili huyo na siasa za Homa Bay japo ukweli ni kwamba Bw Magwanga alimtoa gavana wa sasa kijasho wakati wa uchaguzi na kortini na ni wazi akirejea ODM basi Bw Mbadi huenda asitimize ndoto yake ya kuwa gavana,” akasema Bw Andati.

Mchanganuzi huyo hata hivyo, anadai Bw Orengo ndiye msema kweli kuhusu makubaliano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ikizingatiwa kwamba anawafahamu wawili hao na yupo karibu nao kuliko Bw Mbadi.

Hata hivyo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maseno, Dkt Tom Mboya anadai Rais Uhuru na Bw Odinga ndio wanaoweza kuelezea kilichoko kwenye makubaliano yao badala ya viongozi hao wawili wa ODM kutofautiana kuhusu mambo wasiyoyajua.

“Ukweli ulioko kwenye ‘handsheki’ ni Bw Odinga na Rais Uhuru wanaoweza kuelezea. Ingawa Bw Mbadi na Seneta Orengo wanatofautiana, hakuna kati yao anayeweza kusema anafahamu chochote kuhusu ushirikiano huo,” akasema Dkt Mboya.

You can share this post!

JAMVI: Wandani wa Ruto wamtaka amkabili Uhuru akigombea...

TAHARIRI: Mabilioni ya kazi gani kama watu wafa njaa?

adminleo