• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
TAHARIRI: Ripoti ya ukaguzi Makueni yatia moyo

TAHARIRI: Ripoti ya ukaguzi Makueni yatia moyo

Na MHARIRI

BARAZA la Magavana nchini lilitangaza Alhamisi kwamba kwa mara ya kwanza tangu serikali za kaunti zianzishwe, serikali moja ya kaunti, ile ya Makueni imefaulu kumridhisha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu nchini Edward Ouko, kuhusu matumizi ya fedha.

Ripoti ya Mkaguzi ilipata kwamba mgao wote wa bajeti uliweza kutumika kwa miradi kama ilivyonakiliwa kwenye bajeti ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Kivutha Kibwana.

Ni sadfa kwamba haya yanajiri miaka michache tu baada ya jaribio la madiwani kuvunjilia mbali serikali hiyo kutokana na tofauti kati yao na gavana huyo, kiasi kwamba ni Rais Uhuru Kenyatta aliyeinusuru kwa kukatalia mbali kutia saini pendekezo la kuivunja, kumbe ingeondokea kuwa mfano bora katika utawala na usimamizi wa hela za mlipa ushuru.

Ni kinaya unapolinganisha ufanisi huu na kaunti zingine ambazo habari za ufujaji na uporaji wa mali ya umma zimekuwa kama kawaida, jambo linalotia doa imani ya Wakenya kuhusu ufaafu wa ugatuzi.

Habari za ‘usafi’ wa Kaunti ya Makueni zafaa kuwa njema kwa umma wote, na zaidi zafaa kurudisha imani kwamba udhibiti na hata ukabilianaji wa ufisadi wawezekana ikiwa kuna watu walio na nia njema na walio na uaminifu katika kuhudumia umma watasimama kidete na kuukabili kwa njia zote zile zilizopo.

Kimsingi, jambo hili lafaa kuzua mwamko mpya kwa Wakenya kukataa kukubali kwamba ubadhirifu na ufisadi ndio mkondo wa maisha kwa sababu ikiwa wote watarusha mikono na kukata tamaa katika vita dhidi ya ufisadi, je, kutakuwa na mustakabali kwa vizazi vijavyo?

Ni wajibu wa kila Mkenya kufuatilia utumizi wa fedha za umma katika kaunti yake na kujitokeza kupinga maovu yanayofanyika waziwazi ambayo mwishowe yatakuja kuharibu taifa.

Yastahili umma uache kupumbazwa na maisha ya bei ghali ya viongozi wao au kushangilia na kuvutiwa na viongozi ambao wanatumia pesa zilizotengwa kwa minajili ya maendeleo kwa ajili yao binafsi.

Yastahili Wakenya wahisi kujawa na hamaki na kukemea waziwazi pindi viongozi wawajuao wanapojihusisha na ubadhirifu wa mali ya umma.

Japo ni mapema kuilimbikizia sifa Makueni kama iliyopona ‘ugonjwa’ wa ubadhirifu, hatua yao kuweka historia ya kutopatwa na hatia ya ufujaji yatia moyo.

You can share this post!

Serikali yakiri wagonjwa na maiti zinazuiliwa hospitalini

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Wafahamu baadhi ya Salaf wenye utukufu

adminleo