• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 1:25 PM
KIPWANI: ‘Mungu aliniepusha na penzi karaha…’

KIPWANI: ‘Mungu aliniepusha na penzi karaha…’

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WENYEWE wanasema mapenzi kizunguzungu na yakikupata ni kana kwamba kapagawa na pepo husikii la mwadhini ama la mchota maji msikitini.

Na hili pepo la huba halikumsaza Shua Ilazia maarufu Shua Alice kwani alipokuwa akiendelea kutia makali kipaji chake cha uimbaji alipendana na kijana mpiga kibodi kanisani huku akiwa na matumaini kuwa ndiye aatakuwa mwenza maishani.

Ila alikuja kugundua kwamba mpenzi wake huyo aliyempenda kwa dhati, hakuwa singo jinsi alivyodhania.

“Mola alinifungua macho na nikagundua yule kaka alikuwa na mke na familia na nikaamua kumuepuka,” asema.

Kibao chake cha kwanza Namgojea Bwana alikiachia 2013 kabla kusombwa na wimbi la mapenzi.

Hebu sema kweli, ushamuondoa moyoni?

Alice: Kabisa! Wajua Mungu ni wa maajabu. Alinifichulia siri kumhusu huyu jamaa na akanipa nguvu kumfuta kabisa moyoni na sasa nimeelekeza nguvu zangu zote kumtukuza.

Na je, ulimshukuru Mola kwa kukupa huo ufunuo?

Alice: Muda mfupi baada ya kutemana na yule kaka nilizindua kibao changu cha pili Mungu yu Mwema 2014 kama njia ya kumpa Mola shukrani kwa mema aliyonitendea.

Ngoma zako hizo zilipokelewa vyema?

Alice: Naam! Wajua natumia mitindo ya Rhumba na Bongo Fleva inayowakosha mashabiki hivyo ziliwavutia wengi. Na tangu hapo pia nimetoa vibao vyangu vingine vya Ana Heri, Yesu Yatsaa, Yambonya, Hakuna Mwingine, We give you Glory, Mzazi Wangu, Yesu ni Bwana na Yesu Umkuu.

Kati ya hizo ni ipi ambayo imeitikiwa zaidi?

Alice: Wimbo uliopendwa zaidi na mashabiki wa nyimbo za Injili ni ule wa Yesu Yatsaa ambapo hadi sasa umetizamwa mara 1000 kwenye YouTube. Kwa mimi msanii ninayeinukia, nahisi fahari kujua nina mashabiki kibao.

Ushatimiza matarajio yako au bado safari ndefu?

Alice: Bado ndio naanza. Nina matumaini makubwa ya kuwa mwanamuziki mtajika sawa na kina Martha Mwaipaja na Tumaini Akilimani wa Tanzania na Florence Andenyi wa hapa kwetu Kenya.

Mbona wasanii wafurika ulingo wa injili?

Alice: Sababu kubwa ni kuwa wengi wamgundua kuwa nyimbo za sifa ni kivutio kikubwa cha mashabiki sababu hazibagui hadhira si wadogo kwa wakubwa, vijana kwa wazee wote wamo ndani.

Una chochote unachowaandalia mashabiki kwa sasa?

Alice: Nina kibao ambacho kiko jikoni na nitakizindua hivi karibuni hivyo wasibanduke. Wakae mkao wa kusubiri na ninawahakikishia hawatajutia.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Penzi langu lote liko kwake, lakini ni...

KURUNZI YA PWANI: Wabunge 4 wasema 2022 Pwani itatoa...

adminleo