• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Mashabiki wa Spurs wataka Wanyama atumie Liverpool ile roketi ya shuti aliyosukuma mwaka 2018

Mashabiki wa Spurs wataka Wanyama atumie Liverpool ile roketi ya shuti aliyosukuma mwaka 2018

Na GEOFFREY ANENE

JE, unakumbuka roketi ya shuti ambayo kiungo wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama alisukumia Liverpool msimu uliopita uwanjani Anfield mnamo Februari 4, 2018?

Mashabiki wa Spurs wanataka bao sawa na hilo kutoka kwa nahodha huyu wa timu ya Kenya klabu hizi zitakapokutana uwanjani humu hapo Machi 31, 2019.

Can we have another Victor rocket on Sunday please (Tunaweza kupata roketi nyingine kutoka kwa Victor mnamo Jumapili, tafadhali,” walisema kwenye mitandao ya kijamii mnamo Machi 30.

Ombi lao huenda likajibiwa na Wanyama ama la kwa sababu Spurs imekuwa ikifanya vibaya siku za hivi karibuni. Haijashinda mechi nne zake zilizopita ligini.

Pia, Liverpool ina rekodi nzuri sana dhidi ya Spurs ya ushindi 15, sare nane na kichapo kimoja katika mechi 24 zilizopita uwanjani Anfield.

Mara ya mwisho Spurs ililemea Liverpool uwanjani Anfield ilikuwa 2-0 mwezi Mei mwaka 2011. Spurs imeshinda mechi moja kati ya 12 zilizopita ligini dhidi ya Liverpool ikitoka sare mara nne na kupoteza saba.

Ililima Liverpool 4-1 uwanjani Wembley mwezi Oktoba 2017.

Mbali na takwimu hizi, wanyama hajakuwa fiti alivyokuwa msimu uliopita ama msimu uliotangulia kutokana na kusumbuliwa na jeraha. Alikuwa kwenye benchi Spurs ikizimwa 2-1 na waajiri wake wa zamani Southampton katika mechi iliyopita mnamo Machi 9. Hakucheza pia mechi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund ambayo Spurs ilishinda 1-0 Machi 5 nchini Ujerumani. Alikuwa kwenye benchi. Mechi ya mwisho alisakatia Spurs ilikuwa dhidi ya Arsenal ligini ambayo ilitamatika 1-1 akipumzishwa dakika ya 59.

Liverpool inajivunia karibu kikosi chake chote kuwa bila majeraha wakati huu tofauti na Spurs, ambayo inatarajiwa kuwakosa Eric Dier na Harry Winks, huku pia ikikabiliwa na hofu ya kumkosa Serge Aurier. Macho yote yatakuwa kwa wavamizi matata Salah na Sadio Mane (Liverpool) na Kane (Spurs).

Tuzo

Mnamo Machi 9, 2018, Wanyama alishinda tuzo ya goli bora la mwezi wa Februari mwaka 2018 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza. Hili ndilo bao mashabiki wanataka afunge tena Jumapili.

Bao hilo lilikuwa tamu kiasi cha kuwapiku mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2017 Mohamed Salah (Liverpool & Misri), Sergio Aguero (Manchester City & Argentina), Jose Izquierdo (Brighton & Hove Albion & Colombia), Adam Smith (Bournemouth & Uingereza) na Mario Lemina (Southampton & Gabon).

Alisukumia kipa Loris Karius kiki zito kutoka nje ya kisanduku ambalo Mjerumani huyo aliliona likiwa ndani ya wavu. Lilisaidia Spurs kutoka 2-2 dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield hapo Februari 4, 2018.

Katika mchuano huo, Wanyama alikuwa mchezaji wa akiba akiingia nafasi ya Mbelgiji Mousa Dembele dakika ya 79. Aliona lango dakika moja baadaye akiisawazishia Spurs 1-1.

Mabao yote ya Liverpool yalifungwa na Salah naye Kane akafunga bao lingine la Spurs.

You can share this post!

Pigo kwa Gor wachezaji 4 muhimu kukosa mechi ya Berkane

Mrengo wa Ruto wakaza kamba

adminleo