• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Mpuuzeni Orengo kumpangia Ruto mabaya – Raila

Mpuuzeni Orengo kumpangia Ruto mabaya – Raila

Na JUSTUS WANGA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, hafurahishwi na mwandani wake seneta wa Siaya James Orengo, kufuatia matamshi yake ya hivi majuzi kwamba anapanga kuanza mchakato wa kumuondoa mamlakani Naibu Rais William Ruto.

Bw Odinga, anahisi kwamba matamshi hayo yanaweza kuathiri uhusiano baina yake na Rais Uhuru Kenyatta na inasemekana ameambia wabunge wa ODM kujitenga na matamshi ya Bw Orengo.

Bw Odinga, hasa ameghadhabishwa na matamshi ya Bw Orengo kuwa, yeye na Rais Kenyatta wako na mpango wa kisiri wa kisiasa, kufuatia muafaka wao wa Machi 9, 2018.

Siku moja tu baada ya Bw Orengo kutoboa kuhusu mpango huo, Bw Odinga alimtuma mwenyekiti wa ODM John Mbadi kufafanua ukweli wa mambo.

“Nataka kufafanua kwa uwazi na uhakika kuwa, ODM haijaunda muungano wowote na chama ama mtu yeyote. Maoni mengine yoyote ya kukinzana na haya yachukuliwe kuwa ya mtu binafsi,” Bw Mbadi alisema katika majengo ya bunge wiki mbili zilizopita.

Inasemekana Rais Kenyatta pia hakufurahishwa na matamshi ya seneta huyo, hasa aliposema kuwa alikutana naye kwa saa nne.

Matamshi hayo yalipandisha joto katika kambi ya Naibu Rais, ambapo wafuasi wake wanahisi ni Rais anayejaribu kumhujumu Dkt Ruto, kinyume na maelewano yao ya mbeleni kuwa angemuunga mkono baada ya kukamilisha muhula huu wa uongozi.

Ujumbe wa Bw Orengo umetoa fursa kwa Dkt Ruto na kambi yake kuendelea kukosoa muafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, wakisema ulilenga kuzuia Dkt Ruto kuingia ikulu.

Mahojiano na watu kadha ndani ya ODM yanaonyesha kuwa, kuna kuchanganyikiwa ndani ya chama hicho, wengine wakiamini kuwa Orengo alikuwa akizungumza kwa niaba ya Bw Odinga.

Mzozo huu ulianza mwaka jana ambapo kabla ya Rais Kenyatta kuzuru Nyanza, ilisemekana Orengo aliwaongoza viongozi wa eneo hilo kudai watu walioathiriwa wakati wa uchaguzi uliopita wafidiwe.

Bw Odinga alisemekana kutofurahishwa na wito huo, akisema haukuwa muda wa kujadili mambo hayo.

“Uhuru amekubali kufanya kazi nasi na mambo mengine kama haya yanaweza kusuluhishwa ndani kwa ndani si katika mikutano ya hadhara. Huu si wakati wa uanaharakati, tumejaribu hiyo njia na haikufanya kazi, kwanini tusijaribu mbinu nyingine,” mbunge ambaye hakutaka kutambulishwa alisema Bw Odinga alieleza viongozi wa eneo hilo Rais alipozuru huko.

Wandani wa karibu zaidi na Bw Odinga sasa wanamlaumu Bw Orengo kwa kuharibu mambo, baada ya Rais kukubali kushirikiana na upinzani.

Wabunge wa Nyanza sasa wameshauriwa kutojiunga na mrengo wa viongozi wanaomuunga Bw Orengo.

Baadhi ya viongozi wa ODM pia wamejitenga na matamshi ya Bw Orengo na wanaounga wito huo, wakisema hayafai kuhusishwa na chama.

Inasemekana kuwa Bw Odinga amemtaka Bw Orengo kumweleza sababu ya kusukuma ajenda ya kumng’atua Naibu Rais na atafaidika na nini.

You can share this post!

Faini ya Sh3 milioni mkulima akikataza serikali kukagua...

Pesa zinazonyang’anywa wafisadi zitumike kulipa...

adminleo