• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Mkataba wa Uhuru na Museveni utageuza Kenya mateka wa Uganda – Kuria

Mkataba wa Uhuru na Museveni utageuza Kenya mateka wa Uganda – Kuria

RUTH MBULA na SHABAN MAKOKHA

VIONGOZI kadhaa nchini wameeleza wasiwasi wao kuhusu makubaliano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Uganda, Rais Yoweri Museveni walipokutana Mombasa.

Viongozi hao wakiwemo Mbunge wa Gatundu, Bw Moses Kuria, aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echeza na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli walisema makubaliano ya wawili hao hasa kuhusu uagizaji wa sukari yatadhuru nchi hii.

Akizungumza alipokuwa Kaunti ya Nyamira jana, Bw Kuria alisema wakulima wa miwa watadhulumiwa endapo makubaliano hayo ya kuagiza kiwango kikubwa zaidi cha sukari kutoka Uganda yatatekelezwa.

Mbunge huyo alitoa wito kwa wabunge kutathmini upya suala hilo.

Akihutubia waumini katika Kanisa Katoliki la Mosamaro Masaba, Bw Kuria alisema wakulima wa Kenya watazidi kuumia huku serikali ikitazama.

Alikuwa ameandamana na Spika wa Seneti, Bw Ken Lusaka, Seneta wa Nyamira, Bw Okong’o Omogeni na Mbunge wa eneo hilo, Bw Vincent Kemosi.

“Tulikaa chini tukatia sahihi makubaliano. Makubaliano yote yanapendelea Uganda. Museveni ametutawala na huu ni wakati wa kusema ukweli,” akasema.

Kenya ilikubali kuagiza bidhaa zaidi kutoka Uganda kwa matumaini kwamba Uganda itatoa msimamo unaofaa kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR inayolenga kuunganisha mataifa hayo mawili.

Wakati wa ziara yake ya siku tatu, Rais Museveni alionekana kunufaika zaidi kwa taifa lake kuzidisha biashara humu nchini, hali iliyopelekea Wakenya kulalamikia jinsi serikali imekubali kudhulumiwa kirahisi.

Kenya ilikubali kuongeza kiwango cha sukari kinachoagizwa kutoka Uganda kutoka tani 36,000 hadi tani 90,000 mradi tu ithibitishwe sukari hiyo ilitengenezwa nchini humo.

Kenya pia iliondoa marufuku ya kuku kutoka Uganda na pia ikapeana ardhi Naivasha kwa taifa hilo kujenga bandari ya nchi kavu.

Bw Atwoli alimtaka Rais aelewe kwamba uamuzi aliofanya utadhuru viwanda vya humu nchini ambavyo tayari vinatatizika kuzalisha sukari.

You can share this post!

GSU na Prisons kujaribu kunyang’anya Waarabu taji...

Lloris akiri kuipa Liverpool ushindi

adminleo