• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Madai ya visa vya ubakaji yaongezeka Gatundu Kaskazini

Madai ya visa vya ubakaji yaongezeka Gatundu Kaskazini

Na LAWRENCE ONGARO

WANAWAKE wa kijiji cha Mutuma eneo la Gatundu Kaskazini wameungana pamoja kulalamikia hali mbaya na kuongezeka kwa visa vya ubakaji.

Wanawake waliozungumza na Taifa Leo na ambao hawakutaka kutajwa walidai ya kwamba kwa siku za hivi karibuni wameishi kwa hofu kuu wasijue la kufanya.

Walizidi kusema ya kwamba siku chache zilizopita mwanamke wa kutoka kijiji hicho, alivamiwa kwake usiku wa manane na wahuni wakamteka nyara na kumbaka mara kadha kabla ya kumdunga kisu.

“Hilo ni jambo hatari kwa wanawake na kwa hivyo serikali inastahili kuingilia kati. Tumejaribu kupiga ripoti kwa polisi lakini ni kama tunapoteza muda wetu bure. Hakuna anayetujali kabisa,” alisema mama mmoja aliyeongoza kikundi hicho na ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Walidai ya kwamba hata wakipeleka kesi zao kwa kituo cha polisi hakuna cha maana wanachoelezwa.

Wanawake hao wenye hasira wamedai kuwa siku chache zilizopita msichana wa shule; wa darasa la nane hasa, alinajisiwa na genge la wahuni  halafu baadaye wakamwacha kichakani akiwa hoi.

Wafululiza hadi kituoni

Wanawake hao waliacha shughuli zao zote za shambani na ufugaji na kufululiza hadi kwa afisa mkuu wa polisi ili kuwasilisha malalamishi yao.

Walidai polisi wa kituo cha Mutuma wakielezwa jambo la dharura wanapenda kupuuza kila mara.

“Wengi wao huonekana wakipiga doria lakini lengo lao kuu ni kuwahangaisha wakazi,”  alisema mkazi mmoja mwanamke ambaye alisema jina lake libanwe kwa sababu ya usalama wake.

Walisema kuwa eneo hilo kwa jumla halina usalama wowote ambapo wahalifu waliojihami huvamia maboma ya wanawake wajane na kuwabaka kisha kuwaacha na majeraha ya visu vilevile.

Wakazi hao walitaka maafisa wapya waletwe katika eneo hilo ili kuwe na mabadiliko fulani.

Afisa mpya wa polisi wa eneo hilo Bw Stephen Kirui alisema madai hayo yana uzito mkubwa ambapo ni vyema kuyatatua mara moja.

“Tayari nimeanza uchunguzi mkali ili kubainisha ukweli wa mambo. Polisi yeyote ambaye atapatikana kuwa amekuwa akizembea Kazini bila shaka atalazimika kubeba msalaba wake mwenyewe Siwezi vumilia utovu wa nidhamu,” alisema Bw Kirui.

You can share this post!

WAKILISHA: Asambaza teknolojia mashinani

Kocha Odera ataja chipukizi wa Chipu tayari kuwinda tiketi...

adminleo