• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
MARADHI: Uchungu wa kuwapoteza uwapendao

MARADHI: Uchungu wa kuwapoteza uwapendao

NA RICHARD MAOSI

CHARLES Maina mwenye miaka 69 kutoka eneo la Bahati, Kaunti ya Nakuru anakumbuka kama jana, uchungu wa kupoteza wake wawili na mama mzazi kwa kipindi cha muda mfupi.

Maina alizaliwa eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu mnamo 1952, akapata malezi ya mzazi mmoja, yeye pamoja na kaka yake ambaye kufikia sasa anaishi North Carolina, Marekani.

Kabla hajafikwa na matatizo, alikuwa na kazi nzuri, gari, mashamba na aliwekeza katika biashara lakini sasa anaishi katika ekari moja ya kipande cha ardhi!

Alianza taaluma ya ualimu 1972, Siriba Teachers College Maseno, na alipohitimu akaajiriwa jijini Nairobi.

Katika safari yake ya ualimu, alifunza shule za msingi za haiba kama vile Riruta Satellite, Dagorreti na Kirigo.

Bado akiwa mwalimu alifanya vyema katika michezo na kazi za sanaa ya maigizo jukwaani, ndipo akateuliwa kuwa katibu mkuu wa Muungano wa Michezo kwa Shule za Msingi na Taasisi nchini.

Katika nafasi hiyo, alikuwa na mchango mkubwa katika michezo barani Afrika hasa Afrika Mashariki, akiwahimiza wanafunzi kuzingatia vipawa.

Mzee Charles Maina akisimama kwenye makaburi ya wake zake katika eneo la Bahati, Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Aidha alifanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya dola, KDF na Kenya Prisons kama mshirikishi wa kufanikisha hafla zao za michezo akihudumu kama mkufunzi na kiongozi wa kutoa matangazo.

Mnamo 1986 alifungua shule ya kibinafsi kaunti ya Kisii akaibatiza jina Montessori, ambapo vilevile alisaidia kuchonga akili za wanafunzi ,mbali na kuwa shupavu katika michezo.

Lakini ghasia za uchaguzi 2007/2008, zilizima ndoto yake pale shule ya Montessori ilipovamiwa na kila kitu kuharibiwa.

Akiba yake yote iliteketea, akaamua kurejea Nakuru 2009, ili aweke upya misingi katika maisha yake.

“Nikiwa Nakuru mauti yalinyakua wake zangu kutokana na maradhi, mke wa kwanza aliaga 2010 kutokana na maradhi ya moyo, wa pili akapoteza maisha kutokana na saratani ya matiti 2011,” Maina alisema.

Anaungama kuwa wake zake walikuwa nguzo muhimu katika maisha yake, kumtuliza moyo hasa pale alipopoteza ajira.

Mzee Charles akionyesha picha za wanasiasa mashuhuri aliowahi kutangamana nao zamani akifanya kazi kwenye idara ya michezo nchini. Picha/ Richard Maosi

“Kinachoumiza moyo wake zangu walipoteza maisha muda ambao nilikuwa bado nawahitaji zaidi, wanisaidie kulea watoto wetu,”alisema.

Anasema mke wa kwanza aliaga baada ya kupigana na maradhi ya moyo, kwa jumla ya miaka mitano.

Wakati wa kifo chake, alikuwa mwalimu mkuu katika shule ya Msingi ya Kisii.

Mke wa pili alikuwa naibu mwalimu mkuu katika shule ya msingi ya Ol Donyo Mara Kabazi, Nakuru.

“Sikujua gharama kubwa ingehitajika kuwatibu wake zangu,kwa sababu sikuwahi pata, hamasisho kuhusu maradhi yasiyoweza kuambukizana,”aliongezea.

Kulingana na daktari moyo wa mke wa kwanza ulikuwa ukipanuka siku baada ya siku, na alihitaji upasuaji kurekebisha hali hiyo.

Aidha matibabu ya mke wa kwanza yalikuwa ghali mno, kiasi kwamba alilazimika kuuza mali yake yote ili apate pesa.

Lakini aliaga siku chache tu kabla ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Binti yake Charles Maina anayeugua maradhi ya kifafa. Yeye hutegemea kufanyiwa kila kitu. Picha/ Richard Maosi

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na, Kenya Cancer Statistics and National Strategies,kansa huchangia asilimia 7 ya vifo kote nchini ikifuatwa na maradhi mengine.

Adha mataifa yanayoendelea kama Kenya, ndio hupitia wakati mgumu kukabiliana na jinamizi la maradhi yasiyoweza kuambukiza.

Kansa ya matiti ikiongoza kwa asilimia 5,kisha ikifuatwa kwa karibu na ile ya kizazi.

Aidha uchunguzi unaonyesha baadhi ya wanawake, wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa kuliko wengine.

Ni wazi kuwa mambo yanayochangia seli za kansa, ni unywaji wa pombe kupita kiasi na historia ya kizazi cha mtu.

Mke wa pili wa mzee Maina alipoaga 2011, kutokana na saratani ya matiti, alisononeka sana.

“Mke wangu alikuwa amefikisha kiwango cha pili, na tulipogundua maradhi yalikuwa yameenea katika kila sehemu ya mwili wake. Nilijawa na huzuni moyoni,” aliongezea.

Anasema wakati wa kifo chake familia haikuwa imepoza makovu ya mke wa kwanza. Pia ilikuwa ikihangaika kukamilisha bili za hospitali ya mke wa kwanza.

Mzee Charles akielezea maisha ya upweke anayoishi tangu apoteze wake zake wawili. Picha/ Richard Maosi

Mke wa pili alipolazwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta, afya yake ilidhoofika kiasi cha kutatiza macho yake.

“Madaktari walitushauri kuwa ni upasuaji tu ungeokoa maisha yake, lakini hawakutupatia hakikisho kuwa angeishi tena. Mke wangu aliaga siku moja tu baada ya upasuaji,”alisema.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, (WHO) wagonjwa waliopoteza maisha yao kutokana na maradhi ya moyo walifikia 7,771 ambayo ni asilimia 2.71 ya vifo vyote vinavyoshuhudiwa.

Idadi ambayo ni 44.20 kwa idadi kila watu 100,000, hali ambayo inafanya Kenya kushikilia nambari 180 kote duniani.

Maradhi ya moyo husababishwa na kisukari, kuvuta sigara, kunywa pombe kupita kiasi, shinikizo la damu na msongo wa mawazo.

Aidha hali ya moyo wa mtu, inaweza kuchangia maradhi haya hasa pale inapopata changamoto ya kusukuma damu.

Kutibu maradhi ya moyo katika hospitali ya kibinafsi ni zaidi ya milioni moja, lakini kwenye hospitali ya Kenyatta hufikia 175,000.

Mnamo 2016 mzee Maina alipoteza mama mzazi kutokana na maradhi ya tumbo, hata kabla ya kupata faraja kwa kupoteza wake zake.

Hapa anaonyesha sehemu ambayo anajenga jumba la umma kuwahamasisha wakazi kuhusu changamoto za maisha. Picha/ Richard Maosi

Aliachiawa mtoto anayeugua maradhi ya kifafa, na watoto wengine wanane akiwa kama mama na baba.

Anasema kumtunza mwanaye mwenye umri wa miaka 45 anayeugua epileptic, kunampatia changamoto ikizingatiwa kuwa yeye hulazimika kumfanyia kila kitu.

“Hali ya mwanangu si nzuri,kwa sababu anahitaji uangalizi wa karibu jambo linalofanya nikwamishe shughuli zangu nyingi ikizingatiwa nimekuwa mzee,”Maina aliongeza.

Maina pia ameachiwa jukumu la kulea watoto wengine wawili mmoja akisomea katika shule ya upili ya Jomo Kenyatta Nakuru, na mwingine, katika taasisi ya kiufundi ya Eldoret.

Aidha anasema mtoto wa mke wa pili, anasomea uanahabari Chuo cha Multimedia University bewa kuu Rongai Nairobi.

Anasema wakati mwingine, yeye hulazimika kuingilia kati kama mzazi ili aweze kuwasaidia watoto wake ambao mpaka sasa hawajapata ajira ya kudumu.

Vifo vya wake zake wawili vilifanya afikiri upya, akaamua kuanzisha kituo cha kuhamasisha jamii kuhusu maswala mbalimbali yanayokabili jamii siku hizi.

Taifa Leo Dijitali ilipozuru makao yake, iligundua asilimia 70 ya jengo la kituo lilikuwa tayari kwa matumizi, hasa kutoa huduma kwa jamii.

Ametengeneza sehemu ya kuegesha magari, na mahali pa kukaribishia wageni ikizingatiwa hizi ni hatua zake za mwisho kumalizia mradi.

Maisha ya utulivu kilomita 17 kutoka mjini Nakuru ilitubainishia hali ya upweke anayopitia, lakini mzee Maina hajakata tamaa. Anapiga moyo konde kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.

You can share this post!

Zidane sawa na Del Bosque kwa makali – Casillas

Kocha wa KCB atamani kuepuka Gor ashinde Sportpesa Shield

adminleo