• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Kaunti zilizozembea kuwafaa wananchi zichunguzwe

TAHARIRI: Kaunti zilizozembea kuwafaa wananchi zichunguzwe

NA MHARIRI

RIPOTI ya Mkaguzi wa Matumizi ya Fedha za Umma inaonyesha Kaunti zilitumia mabilioni kwa mishahara na marupurupu, na chache katika maendeleo.

Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa matumizi hayo, ikifuatwa na kaunti za Kiambu, Nakuru, Bungoma, Meru, Machakos, Elgeyo Marakwet, Kisii na Mombasa. Isipokuwa Kisii na Elgeyo Marakwet, kaunti hizo nyingine zilikuwa na kiwango cha chini cha maendeleo.

Kwa upande mwingine, Kitui, Mandera na Narok zilifanya maendeleo makubwa hata baada ya kubana matumizi katika mishahara.

Takwimu hizi zinamkanganya Mkenya ambaye awali alionywa kuwa asichague wanasiasa kuongoza kaunti. Katika jopo hili, kuna mwanasiasa aliyekomaa, Bi Charity Ngilu, ambaye ameonyesha mfano wa kuigwa.

Gavana huyo wa Kitui ameonyesha kuwa hata akina mama wanaweza kufanya maendeleo makubwa wanapopewa nafasi ya kufanya kazi bila ya kuingiliwa. Ameboresha sekta ya Afya n ahata kilimo kimeimarika. Juhudi zake za kukabiliana na wakataji miji wanaochoma makaa pia zimeanza kuzaa matunda.

Lakini kuna kaunti ambazo zafaa kumulikwa kwa kutokuwa na kiwango cha maana cha maendeleo. Ripoti ya afisi ya Bw Edward Ouko inaonyesha kuwa Lamu na Kajiado hazijakuwa na maendeleo yoyote ya kupigiwa mfano.

Ni majuzi tu ambapo kaunti ya Kajiado ilikosa fursa ya kuandaa Sikukuu ya Madaraka Dei kwa kukosa uwanja. Sasa maadhimisho hayo yatakuwa katika kaunti jirani ya Narok.

Gavana Joseph Ole Lenku na mwenzake wa Lamu Fahim Twaha wanapaswa kuamka na kuwafanyia kazi wananchi, ikiwa takwimu za afisi ya Mkaguzi wa Fedha za Umma inasema kweli.

Bunge la Seneti linapaswa kuchukua hatua za haraka na kuchunguza kiini cha maendeleo kufanywa kwa kiwango cha chini mno katika kaunti hizo mbili.

Aidha, maseneta wana wajibu wa kuingilia kati uajiri usiostahili katika baadhi ya kaunti. Kwa mfano haieleweki kwa nini kaunti kama Turkana na Wajir zitumie pesa nyingi kulipa wafanyikazi.

Magavana wa kaunti zote 47 yafaa watambue kuwa walichaguliwa na wananchi sio eti kwa sababu wana elimu au maarifa kushinda wengine. Walipewa mamlaka hayo kwa sababu walishawishi wananchi kuwa wana uwezo wa kufanya maendeleo. Jukumu hilo ni muhimu kuliko kuairi watu wasiohitajika.

You can share this post!

MATHEKA: Suala la umri wa kushiriki ngono lijadiliwe kwa...

Huduma Namba si ile ‘666’ ya kishetani, Uhuru...

adminleo