• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
KAULI YA MATUNDURA: Mchango wa Wachina katika makuzi ya Kiswahili

KAULI YA MATUNDURA: Mchango wa Wachina katika makuzi ya Kiswahili

Na BITUGI MATUNDURA

JUMA lililopita, mtaalamu – Dkt Caesar Jjingo wa Chuo Kikuu cha Makerere alizua mdahalo kwenye ukumbi wa WhatsApp wa CHAKITA Karatina 2019 – alipowauliza wanataaluma kwenye ulingo huo wampe mifano ya leksikoni au maneno ya Kichina yaliyoingia katika Kiswahili.

Swali lake lilichochewa na kauli ya Prof David P.B. Massamba – akipinga maoni ya Hamo Sassoon (1980) aliyedai kwamba asilimia 80 ya msamiati au leksikoni ya Kiswahili ni maneno ya Kibantu huku asilimia 20 ya msamiati wa Kiswahili ukitokana na asili ya Kiarabu.

Kwa mujibu wa Sassoon Chambacho Massamba, Kiswahili hakina maneno ya ‘mkopo’ kutoka kwa lugha nyingine isipokuwa Kiarabu.

Katika kitabu chake – Kiswahili ‘Origins And Bantu Divergence – Convergence Theory (2007)’, Massamba anasema kwamba tunajua kwa hakika kuwa Kiswahili kina maneno ‘mkopo’ kutoka kwa lugha nyingine kama vile Kireno, Kiingereza, Kituruki, Kiajemi, Kiibrania, Kifaransa, Kijerumani, Kijapani, Kilatini, Kigiriki, Kihispania na Kichina.

“Waswahili, kuna kitabu ambacho ninasoma kwa sasa. Mwandishi anasema Kiswahili kimetohoa/kuazima baadhi ya maneno kutoka kwenye Kichina, pasipo kutoa mifano ya baadhi ya maneno hayo. Je, kunaye anayeweza kukumbuka baadhi ya maneno hayo tafadhali?” akauliza Dkt Jjingo.

Nilipojikunakuna kichwa, sikuweza kukumbuka neno hata moja.

Mawazo yaliyonijia ni kwamba labda Massamba kakosea kukiorodhesha Kichina kwenye kundi moja na lugha zilizochangia sana leksikoni ya Kiswahili.

Kwa hakika, ni rahisi mno kutaja maneno yenye asili ya lugha hizo nyingine alizotaja Massamba yaliyoingia katika Kiswahili – isipokuwa Kichina.

Kwa hiyo, nilimjibu Dkt Jjingo kwamba Massamba si ‘Msahafu’ – kwamba asemalo ndilo hilo.

Mtaalamu wa Ushairi na Utamaduni wa Waswahili – Prof Kineene Wa Mutiso wa Chuo Kikuu cha Nairobi alisema kwamba, ingawa Wachina walitagusana na Waswahili kwa muda mrefu na hata kuwaoa, hawakuwaathiri sana.

Mifano ya maneno ya Kichina yaliyoingia katika Kiswahili aliyotoa Prof Wa Mutiso ni pamoja na ‘sinia’ na ‘chai’.

Nilipoangalia kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI) niligundua kwamba ingawa etimolojia ya neno ‘chai’ imefumbatwa na kamusi hiyo kuwa ni Kichina, etimolojia ya neno ‘sinia’ imeelezwa kuwa ya Kihindi.

Wataalamu walianza kudahili iwapo wanaleksikografia wa awali – wakiongozwa na akina Fredrick Johnson na Ludwig Krapf ‘walikosea’ katika kutambua etimolojia halisi ya baadhi ya maneno waliyoyakusanya na kuyaingiza katika kamusi.

Kadhalika, wataalamu walitanua fikra na kusema kwamba, kuna uwezekano neno la Kichina kuingia katika Kiswahili kupitia kwa Kihindi ikiwa kuna mtagusano wa watu wa jamii hizo.

Uchache wa maneno ya Kichina yaliyoingia katika Kiswahili ilishadidiwa na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Dkt Jjingo na Prof Massamba kwa njia ya WhatsApp.

“Je, unaweza kunipa baadi ya mifano ya maneno yaliyotoholewa kwenye Kichina?” akauliza Dkt Jjingo. “Neno linalonijia kwa haraka haraka ni ‘chai’,” akajibu Prof Massamba.

Muktadha huu unaonesha kwamba maneno ya Kichina yaliyoingia katika Kiswahili si mengi sana. Pekuapekua yangu ilionyesha kuwa mbali na ‘sinia’ na ‘chai’, kuna pia ‘chopstiki’ na ‘kung’fu’.

Fenomena ya ‘ukame’ wa maneno ya Kichina yaliyotoholewa na kuingizwa katika Kiswahili inapaswa kutuchochea kufanya utafiti zaidi kubaini sababu ya ‘utasa’ huo wa leksikoni – licha ya kwamba Waswahili walitagusana kwa ukuruba mno na Wachina.

Hata hivyo, Prof Kineene Wa Mutiso anahisi kwamba jawabu la hali hii limo kwenye hulka ya Wachina, Wakorea na Wajapani kutokuwa na mazoea ya kutagusana na watu wengine. Anawamithilisha na konokono, kasa na ambao popote waendapo, hubeba ‘nyumba zao’.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Justus Kyalo Muusya

MAPITIO YA TUNGO: ‘Pepo za Mizimu’ ni novela...

adminleo