• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
USAFI: Jinsi ya kuzuia harufu mbaya kinywani

USAFI: Jinsi ya kuzuia harufu mbaya kinywani

Na MARGARET MAINA

[email protected]

HARUFU mbaya kinywani inaweza kuathiri maisha ya mtu kimahusiano kwa sababu anakuwa hana ujasiri wa kutagusana na kusemezana au kupiga gumzo na wenzake.

Chakula anachokula mtu kinaathiri hewa inayotoka kinywani. Harufu mbaya si ugonjwa wa kuambukiza.

Pia tatizo kubwa ni kwamba watu wenye harufu mbaya huenda pengine hawana habari kwamba wana harufu mbaya.

Harufu nyingi mbaya kinywani hutokana na vyakula vyenye asilia ya proteni.

Kutokuwa makini na usafi wa kinywa kama vile ubwete wa kupiga mswaki vizuri unafanya uchafu na bakteria hatari kusalia kinywani.

Maambukizi ya magonjwa kama vile fizi kutoka damu, mfumo wa upumuaji kuathirika vibaya na kisukari ni baadhi tu ya changamoto.

Baadhi tu ya visababishi ni kinywa kuwa kikavu kutokana na dawa (medications), uvutaji sigara, mazoea ya kunywa kahawa bila kusunza pamoja na ulaji wa vyakula vyenye viungo vikali kama vile vitunguu maji au saumu.

Ni rahisi sana kutambua harufu kutoka kwenye kinywa cha mtu mwingine.

Namna ya kujilinda na harufu mbaya mdomoni (tiba) 

Kula vyakula vyenye afya na vyakula ambavyo wakati unakula vinaweza kusafisha kinywa vizuri.

Kusafisha meno mara kwa mara kwa siku asubuhi na baada ya mlo wa usiku, unashauriwa kutumia kisafisha ulimi (tongue cleaner) kusafishia ulimi wako. Tumia bazooka (chewing gum) ambazo husaidia kuongeza kiasi cha mate kwenye kinywa kilichokauka.

Tumia dawa ya kusukutua mdomoni (mouthwash) kabla ya kulala usiku. Kuwa makini na afya ya kichwa chako kama vile kupiga mswaki vizuri, kuondoa mabaki ya vyakula kwenye meno na kumuona daktari kila unapoona una Matatizo ya meno au kinywa au kila baada ya miezi sita.

Kuhakikisha unakunywa maji ya kutosha kila siku angalau bilauri nane za maji.

Mwone daktari wako ukiona una tatizo la harufu mbaya kinywani.

Namna ya kujikinga na kuondoa harufu mbaya mdomoni

Watu wengi husumbuliwa na tatizo la kunuka mdomo bila hata kujijua hivyo kuwa kero kwa wenzao. Mara nyingi hali ya harufu mbaya kutoka kinywani husababishwa na uchafu wa kinywa na ulaji wa vyakula usiosahihi. Kizuri tu au angalau ni tatizo linalotibika.

Ni rahisi kulizuia na kuliondoa tatizo la kunuka kinywani iwapo utaamua kufuata kanuni za usafi wa kinywa na unywaji wa maji kwa kufuata kwa makini muongozo ufuatao:

Kupiga mswaki

Kitu cha kwanza kufanya ni kupiga mswaki kwa ukamilifu kila uamkapo asubuhi. Wakati wa kupiga mswaki, utatakiwa sio tu kusugua meno, lakini pia ulimi, sehemu ya katikati hadi karibu na koromeo kwa kusugua vizuri.

Vilevile kila uamkapo baada ya kulala mchana au jioni, hakikisha unapiga mswaki kwani bakteria wa kinywani hutawala kinywa kila ulalapo. Baada ya kupiga mswaki na kusugua ulimi hakikisha unasukutua kwa maji safi.

Kunywa maji mengi

Maji ni muhimu mwilini mwa binadamu. Unywaji wa maji ya kutosha kila siku utakusaidia kudhibiti na hatimaye kuondoa tatizo la kunuka mdomo. Unywaji wa maji mengi ni muhimu, hasa kwa wale watu wenye ugonjwa wa kukauka midomo.

Mara nyingi harufu itokayo kinywani, hutokea tumboni na sio kinywani pekee. Kama tumbo litakuwa chafu, hata kama utasafisha kinywa vizuri bado harufu mbaya inaweza kuendelea kutoka. Hivyo ni vizuri kushauriana na wataalamu wa kiafya kwa matokeo mazuri kabisa.

Kwa upande mwingine, ili kuzuia kinywa kunuka pale mdomo unapokuwa umekaukiwa na mate, ni vizuri kutafuna vitu kama bazooka (chewing gum) ili kuzalisha mate ambayo huhitajika katika kudhibiti bakteria.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nikiomba pesa sipewi, lakini...

AFYA: Kitunguu saumu kina faida zozote kiafya?

adminleo