• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
UHALIFU KISAUNI:  Wanafunzi wa TUM wamlilia Mutyambai awaokoe

UHALIFU KISAUNI: Wanafunzi wa TUM wamlilia Mutyambai awaokoe

Na STEVE MOKAYA

MTAA wa Kisauni, Mombasa huibua kumbukumbu za utovu wa usalama na uoga kila unapotajwa. Hili ni eneo ambalo limepata umaarufu jijini Mombasa kwa kuwa maficho na makazi makuu ya magenge ya vijana wasioogopa kuua wala kumjeruhi mtu yeyote, ilmradi wapate watakacho – pesa na mali ya thamani.

Waathiriwa wakuu wa uhuni wa magenge haya ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM), ambao wanaishi katika eneo hili.

Wengi wao wamekuwa waathiriwa wa ujambazi unaoendeshwa na makundi haya, na sasa ni dhahiri kwamba wanaishi kwa woga mkuu, wasijue siku yao ya kuporwa, kuumizwa au hata kuuawa na magenge haya itakuwa lini. Hii ni kwa sababu katika mwezi wa Machi pekee, wanafunzi kadhaa wamekumbana moja kwa moja na unyama unaosababishwa na magenge haya.

Kwa mfano, mnamo Machi 15 mwaka huu, Elikana Cheruiyot (pichani juu), mwanafunzi wa mwaka wa tatu alivamiwa na mwenziwe, Dennis Sigei, katika chumba chao huko Kisauni.

Ilikuwa ni asubuhi kama ya siku yoyote, tu, na Elikana alikuwa ameamka akiandaa staftahi kabla aelekee shuleni. Awali, asubuhi hiyo, alikuwa ametoka saa kumi na mbili kuenda kununua sukari kwa ajili hiyo, ila, aliporudi hakufunga kwa komeo lango la ploti wanamoishi. Sasa ikawa kwamba alipokuwa katika shughuli ya kutengeneza chai, akasikia sauti kuu ikifoka kutoka kwenye mlango.

“Nilikuwa nakoroga chai niliposikia watu wakisema kwa sauti ‘kila mtu lala chini!’ Elikana anafuta kumbukizi. “Mwanzo sikushtuka wala kupinduka kwa haraka kwa vile nilidhani kuwa walikuwa ni askari wanaopiga doria,” akasimulia Taifa Leo Dijitali. 

Pindi tu alipogeuka kuona hao ‘askari’, alipatana uso kwa macho na panga lenye makali kuwili likimkabili, pamoja na vijana barobaro watano wenye ukali nyusoni mwao.

“Hapo ndipo nilijua sasa leo tumekwisha,” Elikana anasema. Denniis Sigei aliyekuwa bado analala aliamshwa na akaamrishwa alale kwenye sakafu,” anaendelea.

Kilichofuatia ni kushuhudia mali yao yote yenye tahamani ikiporwa. Walichukua kipakatarishi pamoja na simu mbili aina ya smart-phones, pamoja na shanta lililokuwa na vitabu.

Hatimaye, walipokuwa wakitoka, mmoja wao alimkata Dennis Sigei kwa panga kwenye kichwa na damu ikaanza kutirirka. Majambazi hao watano walitokomea, wasijulikane waendako.

Katika kisa kingine, Andrew Kirathe, mwanafunzi wa mwaka wa mwaka wa pili katika chuo cha TUM, anasimulia aliposhuhudia wenziwe wakiporwa na kuumizwa.

“Ilikuwa ni saa kumi na mbili asubuhi, na wenzangu walikuwa wameamka wakatoka nje kwenda bafuni kuoga ili kujitayarisha kwenda shuleni,” Andrew anasimulia. “Hiyo siku nilikuwa nimelala kwa rafiki zangu, ila mimi sikuwa na darasa la asubuhi, hivyo sikuwa na haraka ya kuamka,” anaongeza.

Andrew Kirathe, mwanafunzi wa mwaka wa mwaka wa pili katika chuo cha TUM. Picha/ Steve Mokaya

Wenzake walipomaliza kujitayarisha alimka na kutoka na wao ili aende kwake, maana wenzake walikuwa wanaenda chuoni. Hata hivyo, walipotoka walimwacha mwenzao akilala.

Ikawa kwamba pindi tu walipokuwa wametoka, genge la majambazi lilifungua lango la ploti na kuingia kwenye chumba cha kuishi cha marafiki wa Andrew, na kumkata kijana huyo kwa panga kwenye kichwa, baada ya kupora simu aliyokuwa nayo. Baadaye wenzake walirudi na kumpeleka hospitali.

Katika kisa kingine, kilichotokea Jumaplili ya Machi 31, genge la majambazi wa Kisauni lilisimamisha gari la abiria mtaani humo na kuvamia abiria.

Walioshuhudia kisa hicho kilichotokea saa kumi na mbili asubuhi wanasema kwamba genge hilo lilisimamisha gari hilo kama msafiri yeyote.

Gari liliposimama, watu wengine wa genge hilo walijitokeza na kuanza kupasua vyoo vya gari. Waliwaamrisha abiria washuke, huku wakiwatishia.

Katika harakati hizo, msichanana mmoja wa chuo cha TUM aliyekuwa akitoka katika mkesha wa sherehe za maonyesho ya kitamaduni chuoni TUM alikatwa mkono na majambazi hao. Msichana huyo alipelekwa hospitalini baadaye kwa matibabu. Askari walifika na kumwua kijana mmoja wa genge hilo kwa risasi, huku wengine wakitoroka.

Visa hivi vinatokea kila uchao, licha ya kuwa askari wanapiga doria katika mtaa wa Kisauni. Hata hivyo, magenge haya yamegundua nyakati za doria hizi na wakaamua kuchukua mtindo mpya wa mashambulizi.

“Askari wanapiga doria naam, ila magenge haya hushambulia watu nyakati za asubuhi, watu wanapooamka,” Elikana anaelezea. “Wao huja nyakati hizi kwa sababu wanajua kuwa mwanzo hakutakuwa na polisi, na pili, watapata mawindo yao wakiwa hawatarajii kushambulia, na hivyo kufanya shughuli yao iwe rahisi,” anasimulia.

Huku Elikana akisema kuwa askari hujaribu sana kuzuia mashambulizi hayo, Andrew anawalaumu maafisa hao wa poloisi kwa utepetevu na uzembe.

“Kuna siku walinishika usiku saa mbili nikitoka kutazama mechi,” Andrew anazungumza kuhusu askari. “Wakaanza kuniita jambazi na ,mkora anayewahangaisha wakazi wa Kisauni. Na hiyo ni kwa sababu sikuwa na kitambulisho. Nilijaribu kuwaelezea ila hawakusikia. Walikuwa wanatoka pesa. Nilipowaambia sina, wakatishia kwamba ningelala ndani,” anaongezea.

Hatimaye, Andrew alipiga simu nyumbani na kuomba atumiwe pesa za kuwapa hao polisi. Alipotumiwa, alienda na polisi hao hadi kwenye duka la Mpesa na kutoa shilingi mia tano na kuwapa, kasha wakamwachilia. Walikuwa watatu. Andrew anasema kuwa polisi ao hao hupatna na magenge ya vujana wavuta bangi na hawawanyii kitu.

Kwa upande wa Elikana, anasema kuwa walipoenda kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha Nyali kuhusu madhila yaliyowakumba, polisi waliwaambia wazi kwamba hawangefanya chochote kuokoa mali yao iliyoibwa.

“Walituambia kuwa wanawajua baadhi ya vijana hao, na kuwa siku zao zimehesabiwa. Ila wakasema bidhaa zetu hawangeweza kuziokoa,” Elikana anaeleza.

Magenge haya ya Kisauni yanafanya wizi wao kwa makundi, ili kufanya kazi ya kushikwa kwao iwe ngumu. Kwa mfano, Elikana anasema kwamaba kunao vijana wavuta bangi wanaokaa katika mitaa ya Kisauni, ambao hawajawahi kuwaibia. Anaamini kuwa ni vijana hawa ambao huyafanyia ujasusi magenge hayo na kujua mienendo ya wanafunzi. Kishaye vijana hwa hutumika kupanga njama ya kushambuliwa kwao.

“Ninaamini vijana hao wanaovuta bangi hapo mtaani ndio huto habari kutuhusu. Hakuna vile mtu ambaye hanijui anaweza kutoka mbali na ajue kwamba ninaishi mahali fulani na nina kitu fulani,” Elikana akasema.

Licha ya visa hivi vyote, Andrew na Elikana hawana haraka ya kuhama Kiasuni. Wanasema kuwa maisha huko ni rahisi kumudu, licha ya kodi ya ya chini ya nyumba. Wanasema kuwa maji pia hupatikana kwa urahisi na kwa bei ya chini, ikilinganishwa na maeneo mengine yaliyo karibu na chuo cha TUM.

“Huko Kisauni nyumba ya chumba kimoja unaweza ukapata kwa bei ya elfu tano kwa mwezi. Ukienda maeneo mengine kama Kaa Chonjo, nyumba kama hiyo utapata kwa bei kubwa sana, zaidi ya elfu kumi,” Elikana anaelezea.

Huku Inspekta Jenerali mpya wa polisi, Bw Hillary Mutyambai akitarajiwa kuchukua usukani hivi karibuni, wakazi wa Kisauni, na hasa wanafunzi wa chuo cha TUM wanamwomba aimarishe usalama eneo hilo.

You can share this post!

Hargreaves asema ndoto ya Arsenal kumaliza Nne Bora...

Ahadi za Rais bungeni bado hewa

adminleo