• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Finland kusaidia Kilifi kukomesha dhuluma

Finland kusaidia Kilifi kukomesha dhuluma

CHARLES LWANGA na KALUME KAZUNGU

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi, atashirikiana na serikali ya Finland kutatua dhuluma za kimapenzi pamoja na mimba za mapema katika kaunti yake.

Visa hivyo vimeripotiwa kuongezeka na kufikia 17, 850.

Haya yalijiri baada ya gavana huyo kukutana na Balozi wa Finland nchini, Erik Lundberg katika afisi yake mjini Kilifi, kujadiliana jinsi ya kukabiliana na kesi za dhuluma za kimapenzi na mimba za mapema.

Balozi huyo alitaja Kilifi kuwa miongoni mwa kaunti tatu ambazo zimechaguliwa kuzindua mradi huo wa kukabiliana na visa hivyo.

“Kaunti zingine ambazo zinanufaika na mradi huo ambao unafadhiliwa na serikali ya Finland ni Samburu na Bungoma,” alisema.

Mnamo Novemba mwaka jana, Gavana Kingi aliunda kamati maalum ya kuchunguza visa vya mimba za mapema ambavyo wakati huo viliripotiwa kufikia 13,624 na kuhusisha watoto wa umri wa kati ya miaka 15 hadi 19.

Kamati hiyo ambayo ilihusisha maafisa wa afya, elimu na jinsia ilitarajiwa kutoa mapendekezo jinsi shida hiyo itakavyotatuliwa baada ya kukamilisha uchunguzi wao.

Bw Kingi alieleza kuwa suala hilo linafaa kushughulikiwa kwa dharura ili kuzuia uwepo wa vizazi maskini.

Hali hiyo alisema ndiyo imefanya serikali yake kushirikiana na Finland kuona jinsi ya kukomesha dhuluma za kimapenzi na pia mimba za mapema.

Wiki iliyopita, gavana huyo alieleza kuwa mapendekezo ya ripoti hiyo yatatekelezwa vilivyo, na kwamba hawatalenga waathiriwa pekee yao bali pia wale wanaonajisi watoto ili wawasaidie kubadilisha mienendo yao.

“Pia tutaongeza vifaa na huduma za kusaidia wanaodhulumiwa kimapenzi katika hospitali zetu ili kusaidia waathiriwa ambao wamekuwa wakikosa kupata huduma kwa wakati unaofaa,” alisema.

Bw Kingi alisema kuwa waathiriwa wengi wa dhuluma za kimapenzi wamekuwa wakisafiri mbali hadi katika hospitali ya Malindi na Kilifi ambazo ndio hospitali za kipekee zinazotoa huduma hizo.

Hata hivyo, kaunti hiyo haijaeleza kiwango cha fedha ambacho mradi huo utagharimu.

Waziri wa Jinsi Kaunti, Bi Maureen Mwangovya, alisema wanatathmini gharama ya mpango huo.

“Bado tunatathmini mpango na tumeandika mapendekezo yanayatosaidia tupate fedha za kukabiliana na dhuluma za kimapenzi na mimba za mapema,” aliongeza.

Kwengineko, katika kaunti ya Lamu, waliofurushwa kutoka kwa ardhi zao wakati wa vita vya Shifta vya miaka ya 1960, wanataka serikali isimamishe usoroveya na ugavi wa ardhi zao.

Maskwota hao zaidi ya 5,000 waliilalamikia serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kwa kuwatelekeza.

Msemaji wao, Bw Mohamed Mbwana alisema wanataka serikali ya kitaifa ifichue ripoti ya Tume ya Haki, Ukweli na Maridhiano (TJRC), wanayoamini imeangazia mateso ya waathiriwa wa vita vya Shifta.

Bw Mbwana alisema pia kuna haja ya serikali kuwaomba msamaha maskwota wa vita vya Shifta, Kaunti ya Lamu.

You can share this post!

Mashambulio mapya bondeni yazima juhudi za amani

Mfungwa aonja uhuru kwa msamaha wa rais

adminleo