• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
URODA KWA FOLENI: Je, ni rahisi kuacha ukahaba?

URODA KWA FOLENI: Je, ni rahisi kuacha ukahaba?

NA MWANDISHI WETU

SIO mara ya kwanza kwa mji wa Nakuru kugonga vichwa vya habari kutokana na biashara ya ukahaba inayoendeshwa na wasichana na wanawake.

Maeneo ambako utapata biashara hii ikifanywa waziwazi ni Gitwamba, Three Ways, Kanu Street, Baringo Lodge, Kiambuthia Lodge na Ndumu.

Katika barabara ya Kanu Street kwa mfano, utakuta foleni ya wanawake waliosimama na kuwaita baadhi wa wanaume wanaopita, wengine wakiwashika mkono na kuwavuta ili kuwauzia ‘huduma.’

Makahaba katika mitaa mingine mjini Nakuru hujiuza kimyakimya ndani ya giza, na wale wenye ujasiri hujianika hadharani mchana.

Makahaba katika eneo la Three Ways katikati ya mji wa Nakuru wakisaka ‘wateja’ gizani. Picha/ Richard Maosi

Wakiwa wamejipodoa, utawakuta wamepiga foleni ndefu mchana tena peupe ili kunasa windo kwa urahisi, huku wakivuta sigara.

Miaka ya nyuma, vidosho hawa wamekuwa wakikaangwa mtandaoni kwa kuchangia ndoa nyingi na mahusiano kusambaratika.

Biashara hii ya kuchuuza uroda imefanya jamii kuwatazama kwa jicho la dharau na kuwaona kama watu wazembe wasiopenda kupambana na maisha kupata riziki halali.

Je, hii ni kazi halisi?

Taifa Leo Dijitali ilipiga kambi katika ngome zao kung’amua ukweli wa mambo. Tulikutana na msemaji wao aliyekubali kuzungumza nasi, kwa masharti ya kubana jina lake.

Kulingana naye, ukahaba ni kazi kama nyinginezo muradi kuna kitu cha kutia mfukoni mwisho wa siku baada ya kuchuma gizani.

Alieleza kuwa bali na biashara yenyewe kunoga misimu fulani, kuna wakati kiwango cha mapato huenda chini na hata kudorora kabisa.

Mmoja wa makahaba akiwa amesimama karibu na Kiambuthia Lodge, Nakuru mchana. Picha/ Richard Maosi

Kwa upande mmoja, anachekesha anapowalaumu wanaume wanaojifanya mkono ngamu wakati wa wanaposaka huduma hizi, huku wengi wao wakiwa ni vijana. Pia anawalaani wanaume ambao hujifanya ‘wateja’ kisha kuwaibia hela zote walizopata usiku mzima.

Aliwasimanga baadhi yao waliozowea kutoroka pindi tu baada ya kurina asali bila kulipa pesa, na kutisha kuwaitia polisi.

Polisi wamekuwa wakiingilia kati na kutatiza ‘biashara’ yao kwa kuwakamata wateja wanaofika kuburudika katika barabara ya Gusii Road wakisingizia kushika doria.

“Wanaume wanaopatikana wamesimama karibu na gesti au baa, hasa wakati wa jioni wamekuwa wakinaswa na polisi bila hatia,” alisema.

Makahaba wamedhibiti vichochoro vya Threeways wakati wa mchana, na ifikapo husiku hujitokeza barabarani.

Sheria kali za manispaa ya kaunti kuwafurusha zimeonekana kugonga ukuta licha ya uhamasisho kuhusu kutafuta biashara mbadala. Polisi huwakamata baadhi yao na kuwaachilia huru siku chache baadaye.

Hivyo, hii si kazi ya kutegemea kwani huduma ni kati ya Sh100 na Sh300. “Kwa siku kila demu hapa hupata wateja wawili kwa wastani,” anafichua mmoja wao.

Wengi wa makahaba ni wa umri wa makamo, kama mwanamke huyu aliyejibanza katika barabara ya Kenyatta, Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Mbinu mpya

Kila wakati, makahaba wamekuwa wakibuni mbinu tofauti kuepuka mkono mrefu wa sheria na kuendeleza biashara yao haramu ndani ya vyumba vya kibinafsi wanavyokodisha mjini.

Wengi wao wameanika uchi wao na nambari zao za simu kwenye mitandao ya ngono kwenye intaneti, ili kuwanasa ‘wateja’ wasiopenda kwenda kuwatafuta vichochoroni kutokana na fedheha ya kuonekana wakiandamana na vimada.

Polisi wamekuwa wakishirikiana na wachuuzi kuwatimua, hasa pale wanapoanika sehemu za miili karibu na biashara zao, lakini bado wao hurejea barabarani ‘kusaka riziki.’

James Munywa ni mmoja wa wachuuzi hao na anafanya kazi ya kuuza viatu na nguo karibu na eneo la Three Ways. Anasema kwa miaka mitatu amekuwa akizozana na makahaba ambao huzuia wateja kununua bidhaa zake lakini siku hizi amewazoea.

Dada huyu katika barabara ya Gusii, Nakuru anajaribu kumuuzia mwanamume huduma. Picha/ Richard Maosi

Anaeleza jinsi siku za mbeleni wateja walikuwa wakitiliwa mchele ndani ya vinywaji na mashangingi hawa, na kuibiwa kila kitu.

“Hususan wakitambua wewe sio mwenyeji wa hapa watatumia kila mbinu kuhakikisha huondoki bila kuacha kitu kidogo,” James alisema.

Aidha tuligundua kuwa biashara hii huendeshwa na wanawake wenye umri wa makamo pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Ushindani mkali kati ya makundi haya mawili umekuwa ukizua uhasama na kuleta zogo, na utawakuta wakirushiana cheche za matusi baada ya kunyang’anyana ‘mteja.’

Mbona wanajitosa kwa ukahaba?

Changudoa mwingine aliyekubali kuzungumza nasi ni Ann (sio jina lake kamili). Alitusimulia kwa kina jinsi alijikuta katika biashara ya ngono miaka mitatu iliyopita bila kupenda.

Akiwa mzaliwa wa Nyandarua, alikuja Nakuru kutafuta kibarua alipoahidiwa na mjomba wake kuwa angepata kazi.

“Wazazi wangu wanajua ninafanya kazi ya kuuza nguo mjini Nakuru. Kila mwezi huwa ninawatumia pesa za matumizi kwa sababu walinisukuma mjini kutafuta kibarua,” alifungukia Taifa Leo Dijitali.

Hapa swali ni: Mkunwa na mkunaji, muona raha ni nani? Picha/ Richard Maosi

Japo siku za mwanzoni ilikuwa vigumu kujikubali kwamba alikuwa anauza mwili wake, kufikia sasa ameridhia hali na anajaribu kupigana na unyanyapaa.

Alijifundisha kuvalia nguo fupi za kubana, kabla ya kubobea rasmi akaanza kutembea nusu uchi!

“Wateja wangu wengi ni wanaume walio kwenye ndoa,wanatumia fursa hii kujituliza moyo labda kutokana na usumbufu wa wake zao nyumbani,” aliongezea.

Aidha ananyooshea polisi kidole cha lawama, akisema ndio kikwazo kikubwa katika ‘kazi’ yake.

Anasema yeye hulazimika kugawana anachopata na maafisa hawa ili biashara iendelee, la sivyo waingie kizuizini siku kadha.

“Biashara hunoga msimu ambapo wakulima huwa wamevuna mahindi na ngano, au mwisho wa mwaka katika shamrashamra za kukaribisha Mwaka Mpya lakini sasa hali ni ngumu,” alisema.

Akiwa na watoto wawili katika shule ya upili na mmoja kwenye shule ya msingi, anategemea ukahaba kuliwalipia karo na kununua chakula.

Waendeshaji malori ya masafa marefu eneo la Pipeline, Nakuru wanaaminika kuwa wateja kwa huduma za makahaba. Picha/ Richard Maosi

Je, ni rahisi kuacha ‘kazi’ hii?

Jane (sio jina lake halisi) anatueleza jinsi alijaribu kuacha ukahaba lakini akashindwa. “Nilikuwa nimeamua kuacha kazi hii baada ya kupata kazi ya kuuza vyakula mjini. Lakini ule uchu wa kufanya ngono ulinirudisha tena kwa ukahaba. Kila mwanamume niliyemuuzia chakula nilitamani kulala naye. Wengi waliniitisha nambari ya simu, na baadaye nililala nao na kunilipa. Bosi wangu alipogundua alinitimua nami nikarudi vichochoroni,” anafichua.

Hata hivyo, Cate (sio jina lake) anatueleza jinsi yeye wakati ulitimia akaamu kujiondoa vichochoroni. “Ilikuwa baada ya kuhudhuria maombi ya kanisa ambapo niliungama dhambi zangu na kutubu. Niliahidi nafsi yangu kutofanya ukahaba tena,” anasema huku akiongeza kuwa baada ya maombi hayo alipata kazi ya kudumu inayolipa kuliko ukahaba.

“Kwa sasa nimeolewa kwa harusi na ndoa yangu ni ya raha. Siwezi kuchepuka hata kidogo nikikumbuka aliponitoa Mola,” anasema.

Kiongozi wa kidini akiwahutubu wakati katika hafla iliyowakutanisha na serikali ya kaunti kujadili namna ya kuzima ukahaba mjini Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Wakati mwingine makahaba hulazimika kusafiri hadi kaunti jirani za Uasin Gishu, Nairobi na Mombasa wateja wanapopungua.

Ni wazi hawara wengi hapa ni wake za watu, labda waliotengana, wajane au wanaoishi mbali na wapenzi wao kulingana na mahojiano yetu.

Kinyume na inavyotarajiwa, wateja wao wengi sio walevi wala watu hivihivi. Ufichuzi wetu uligundua pia wachungaji na mapasta wa kanisa ni wanunuzi wa huduma za ngono.

Serikali ya kaunti ya Nakuru imeweka mikakati kupunguza idadi ya vilabu na baa katika maeneo ya Kenlands na Section 58 ambapo vilabu ni vingi kuliko makanisa.

Naibu Kaunti Kamishna wa Nakuru Mashariki, Bw Herman Shambi alithibitisha haya mapema mwaka huu katika hafla iliyowakutanisha na viongozi wa kidini kujadili hali hii.

Na si ukahaba pekee, ufichuzi wetu ulibaini kuwa wanadada hawa pia hutumika kufanikisha biashara haramu ya bangi na mihadarati kwa kushirikiana na wanabodaboda.

You can share this post!

Handisheki yamuumiza ‘Baba’

‘Tangatanga’ sasa wajiita Yellow Movement

adminleo