• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
WAKILISHA: Mtetezi wa mabinti dhidi ya ukeketaji

WAKILISHA: Mtetezi wa mabinti dhidi ya ukeketaji

Na TOBBIE WEKESA

UKEKETAJI wa mtoto wa kike si suala geni nchini Kenya.

Kunazo baadhi ya jamii ambazo zingali zinaendeleza utamaduni huu potovu licha ya madhara yake kuonekana wazi.

Jamii zinazowakeketa mabinti wao zimeweza kutoa sababu mbalimbali za kuendeleza utamaduni huu.

Baadhi yao hudai ni njia mojawapo ya kumzuia msichana asiwe na macho ya nje katika ndoa na pia kuhifadhi ubikira yaani hatakuwa na hamu ya wanaume hadi atakapoolewa.

Soilan Kenana, 23, mwanaharakati dhidi ya ukeketaji. Picha/ Tobbie Wekesa

Jamii hizi mara nyingi huyafumbia macho madhara yatokanayo na tendo hili.

Kulingana na utafiti, ilibainika kwamba wasichana waliokeketwa huwa wanapata shida kubwa sana wakati wa kujifungua.

Ukeketaji huharibu tupu ya msichana kisha anapata matatizo wakati anakuwa mkubwa.

Inakuwa vigumu kwake kujifungua salama na vyema. Wengi wao huishia kufanyiwa upasuaji.

Pia, wakati wa ukeketaji, wasichana huvuja damu nyingi sana, suala ambalo huhatarisha maisha yao.

Madhara haya hubakia kumdhuru msichana huyo hadi uzeeni. Kutokana na madhara haya, wasichana wengi kutoka katika jamii hizi huishia kutorokea usalama wao.

Mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yameibukia kupigana dhidi ya utamaduni huu. Isitoshe, serikali vilevile iliamua kupiga marufuku suala zima la ukeketaji wa mtoto wa kike.

Licha ya juhudi hizi zote, bado utamaduni huu unaendelezwa na jamii fulani za humu nchini.

Soilan Kenana, 23, ni mwanadada aliyeamua kuenda kinyume na matarajio ya jamii yake.

Amekuwa mwokozi wa mabinti wengi ambao kwa mtazamo wa baadhi ya wanajamii, wamefikia umri wa kukeketwa.

Mzawa huyu wa kaunti ya Narok, hutembea kijiji baada ya kingine akijaribu kuwaelimisha wazee na akina mama kuhusu athari za ukeketaji wa wasichana.

Kulingana naye, aliamua kulivalia suala hili njuga baada ya kuona mateso na dhihaka waliyopitia wasichana waliokeketwa katika jamii yake.

Soilan ni binti wa Bw Tabula Kenana na Bi Catherine Kenana. Yeye ndiye kitinda mimba katika familia hiyo. Amesomea uanahabari katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret.

Anasema kwamba wengi wa wasichana hawa hulazimika kukeketwa kwa vile wazazi wao huwalazimisha.

“Nimezaliwa katika jamii ambayo bado inaamini katika ukeketaji wa mtoto wa kike. Wengi wa wasichana hulazimishwa kukatwa na wakikataa wao hufukuzwa,” anaeleza Soilan.

Vikao

Soilan aliona njia ya kipekee ya kumnusuru msichana wa jamii yake ni kuandaa vikao na wazee wa jamii pamoja na wazazi.

Kupitia kwa vikao hivi, yeye huwashauri kuhusu athari za ukeketaji na umuhimu wa kuachana na utamaduni huu potovu, ovu na uliopitwa na wakati.

Pia anasema kwamba yeye hutembelea shule mbalimbali akijaribu kuwashauri wasichana dhidi ya ukeketaji. Kwa wale waliokeketwa tayari, Soilan huandaa vikao vya pamoja na kuwapa ushauri nasaha na kuwaelekeza kuhusu njia mwafaka za kujilinda ili kuepuka madhara ya tendo hili waanzapo kuwa wazazi.

Licha ya juhudi zake kupata pingamizi kutoka kwa jamii, kipusa huyu anaamini kwamba penye nia pana njia. La mno kwake ni kuona mtoto msichana akipewa heshima yake.

“Kwangu ninaweza kusema nimefaulu kwa kiwango fulani licha ya pingamizi kuwa nyingi. Mtoto wa kike ana haki ya kuheshimiwa pasi kusukumwa kufanya tendo asilopenda,” anaeleza.

Anakiri kwamba wasichana wengi wameacha shule na kutorokea usalama wao baada ya kukaidi amri ya wazazi wao.

“Linalonikeketa maini zaidi ni kuona hata akina mama ambao wanafaa kuwalinda mabinti wao wakiwa kwenye mstari wa mbele wakiwadhulumu,” anasikitika.

Anayaomba mashirika mbalimbali ambayo yamezamia katika kuhakikisha tendo hili linatiwa katika kaburi la sahau kukaza kamba.

Asema hii ndiyo njia ya kipekee ambayo itamwezesha mtoto wa kike kurudisha hadhi yake katika jamii husika na kupata nafasi ya kujiendeleza na kuishi maisha yenye kupendeza kama wengine.

“Mimi mwenyewe sikupitia mikononi mwa ngariba. Ni jukumu langu kuhakikisha wengine nao hawakutani na adui huyo. Lazima nijaribu kuyaboresha maisha yao mapema iwezekanavyo kwani samaki hukunjwa angali mbichi,” akaeleza.

Soilan anapania kuanzisha shirika la kuwapa watoto wasichana hifadhi pamoja na usalama.

“Ni hela tu ndizo kizingiti kikubwa. Nikipata pesa nina imani nitafanya mambo mengi sana. Lakini namshukuru Mungu kwa yote,” anaeleza.

You can share this post!

MKU yafadhili ujenzi wa darasa nchini Rwanda

MAPOZI: Kidum

adminleo