• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wagaragazana kuwania nyadhifa uchaguzi wa Chaukidu

KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wagaragazana kuwania nyadhifa uchaguzi wa Chaukidu

Na BITUGI MATUNDURA

JUMA lililopita, Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kilicho na makao makuu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin – Madison, Marekani kilifanya uchaguzi wa viongozi wake.

Hata hivyo, uchaguzi huo uliofanyika kwenye mtandao tangu Jumatatu, 1 hadi Ijumaa 5, 2019 uliongezwa muda wa kufanyika na ulikamilika Jumapili 7, 2019.

Kupitia taarifa kwa Taifa Leo, Dkt Elias J. Magembe alisema, hatua hiyo ilichukuliwa ili kuwapa muda wa kutosha wanachama kuenda kwenye sehemu zenye intaneti kutimiza wajibu na haki yao ya kupiga kura.

“Tume ya Katiba na Uchaguzi (KKU) inatangaza kwamba imeongeza muda wa kupiga kura kwa siku mbili – Jumamosi na Jumapili. Sababu kubwa ambayo imezingatiwa katika uamuzi huu ni ukweli kwamba muda uliokuwa umewekwa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa ni muda wa kazi na huenda baadhi ya wanachama hawakupata muda wa kuenda kwenye sehemu zenye intaneti kupiga kura,” akasema Dkt Magembe.

Nyadhifa zilizowaniwa ni pamoja na Urais, Makamu wa rais, Mkurugenzi, Naibu mkurugenzi, Mweka hazina, Katibu mwenezi na Wajumbe wa bodi. Wataalamu waliojitosa ulingoni kuwania nyadhifa hizo wanatoka katika vyuo mbalimbali ulimwenguni – ingawa wengi ni raia wa Kenya na Tanzania.

Waliowania urais ni pamoja na Dkt Dainess Maganda (Chuo Kikuu cha Georgia) na Dkt Leonard Muaka (Chuo Kikuu cha Washington DC).

Wadhifa wa makamu wa rais uliwavutia wagombea wawili – Dkt Hadija Jilala (Chuo Kikuu Huria cha Tanzania) na Dkt Musa Hans (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam). Dkt Hans pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wadhifa wa mkurugenzi ulimvutia mgombea mmoja – Dkt Filipo Lubua wa Chuo Kikuu cha Pittsburg kilichoko katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani. Kwa hivyo, hii inamaanisha kwamba atautwaa wadhifa huo bila kupingwa.
Kadhalika, wadhifa wa naibu mkurugenzi nao ulimvutia mgombea mmoja – Dkt David Wambua Kyeu ambaye ni msimamizi wa programu ya Lugha za Kiafrika Katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley.

Wadhifa wa mhazini uliwaniwa na Bi Happiness Patrick ambaye anafundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Cornrll kilichoko Ithaka New York, Marekani.

Kiti cha katibu mwenezi kiligombewa na Bi Beatrice Mkenda, ambaye anafundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Iowa.

Wanataaluma wanaopania kuhudumu kwenye Bodi ya Wajumbe ya CHAUKIDU ni pamoja na Bi Aida Mutenyo wa Chuo Kikuu cha Kyambogo – Uganda, Prof Aldin K. Mutembei – ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), na Bi Esther Martin Simba – ambaye ni mwalimu wa Kiswahili kwa wageni wanaotaka kujifunza Kiswahili kama lugha yao ya pili katika kampuni yake ya Experience Tanzania Co. Ltd nchini Tanzania.

Wengine ni Dkt Hadija Jilala, Dkt Musa Hans, Mwl Mwajuma Selemani Mohamedi wa Tanga, Prof Pacifique Malonga wa African Academy of Languages, mjini Kigali – Rwanda, Dkt Pendo Malangwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Zeinab Idd (Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar) na Bi Yusta Mganga anayefundishas Kiswahili mjini Arusha – Tanzania.

Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani kilianzishwa mnamo 2012. Madhumuni yake makuu yakiwa kuwaleta pamoja waendelezaji na watetezi wa Kiswahili kote duniani ili kukuza lugha hii na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kujivunia, kufaharia na kueneza Kiswahili.

Wasiliana na mwandishi kwa kutuma ujumbe kwa: [email protected]

You can share this post!

Faida za mapapai kiafya, kimapato na upanzi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya lugha rasmi katika...

adminleo