• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Tabia za ushoga zaripotiwa Juja

Tabia za ushoga zaripotiwa Juja

Na LAWRENCE ONGARO

TABIA za ushoga zimeripotiwa kuenea kijijini Darasha, Juja, katika Kaunti Ndogo ya Thika.

Wakazi wa kijiji hicho tayari wameripoti mienendo hiyo kwa wakuu wa serikali, wakidai kuwa inahusisha baadhi ya wanaume.

Naibu kamishna wa Kaunti Ndogo ya Juja, Bw Charles Mureithi, alisema Jumatano tayari wameanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo ili hatua inayofaa ichukuliwe.

“Serikali haitakubali tabia kama hizo kuzagaa katika eneo la Juja na vitongoji vyake. Kwa hivyo, tunataka ushirikiano wenu ili tuwakamate washukiwa,” alisema Bw Mureithi.

Alisema nchi hii ya Kenya haitambui watu wawili wa jinsia moja kuendeleza tabia za ushoga, na yeyote atakayepatikana akitenda mambo kama hayo atachukuliwa hatua kali kisheria.

Malalamiko hayo yalitolewa na wakazi wa Juja, wakati wa mkutano wa baraza uliofanyika Juja mnamo Jumatano na naibu wa kamishna wa eneo hilo Bw Mureithi.

Alizidi kueleza ya kwamba ataanza kufanya msako kamili akishirikiana na machifu ili kuwanasa wale wanaojihusisha na tabia hiyo potovu.

Wakazi hao walisema tabia hiyo imeenea sana licha ya onyo kali kutolewa kwa washukiwa.

Ushoga watisha

Hata wengine walieleza ya kwamba wanaogopa kuwaacha vijana wao wa kiume peke yao ili wasije wakaingilia uraibu wa ushoga ambao unatisha maisha ya wakazi hao.

“Tumekuwa tukiwaona wanaume wawili wakiishi pamoja huku tabia zao zikitia shaka kwa wakazi wa eneo hilo. Ni vyema wawili hao wachunguzwe ili ibainike wazi ni kwa nini wanaishi sehemu mbali na wananchi,” alisema mchungaji Jackson Njoroge.

Alitaja mienendo hiyo kushamiri kwa sababu ya ukosefu wa kazi na utumiaji wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana wasio na ajira.

Alisema ni jukumu la serikali kuchukua hatua kali kwa watu wanaotekeleza tabia hizo zinazoharibu vijana wengi.

“Kizazi hiki cha sasa kinahitaji ushauri kuhusu maadili mema na jinsi ya kuheshimu miili yao. Ni aibu kubwa kupata vijana wa kiume wakishiriki ushoga. Ni jambo ambalo linahatarisha mwelekeo wa kuwa na kizazi kijacho,” alisema Njoroge, na kuwataka wakazi wawe macho kwa kuzungumza na wana wao wanaowalea majumbani.

Alisema iwapo tabia kama hizo zitazidi kuenea bila shaka wasichana wengi watakosa waume  wa kuwaoa mara wakifikisha umri wa kutaka kuanzisha familia na kizazi kijacho kitaangamia kabisa.

Aliitaka serikali na viongozi wa makanisa wajitokeze wazi na kuzungumzia jambo hilo kwa uwazi bila kuogopa.

You can share this post!

MAPISHI: Makaroni na nyama

KIZAAZAA: Fataki Emirates Arsenal wakitoana kijasho na...

adminleo