• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Simo/ Misimu katika jamii ikiwemo uundaji na sifa zake

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Simo/ Misimu katika jamii ikiwemo uundaji na sifa zake

Na MARY WANGARI

HII ni lugha ya kisirisiri yenye mafumbo ambayo hutumiwa na kundi dogo la watu katika jamii.

Aghalabu huwa ni usemi wa muda tu na hutoweka baada ya muda mfupi na yale yanayobaki husanifiwa na kuwa msamiati rasmi wa lugha inayohusika.

Misimu ina sifa zifuatazo:

Misimu huzuka na kutoweka baada ya muda au majira fulani. Baadhi ya misimu hubadilika huku mingine ikidumu na kuingizwa katika lugha husika.

Ni lugha isiyokuwa sanifu. Aghalabu maneno ya misimu huzushwa na watu kutokana na hali zinazowapata kwa wakati huo.

Mara nyingi haifahamiki na watu wasio wa kundi hilo. Ni lugha ya mafumbo.

Wakati mwingine hubadilika na kuwa sehemu ya msamiati wa lugha husika.

Huweza kupotea na kufa.

Misimu huwa na chuku nyingi. Maneno mengi ya misimu huwa yanakejeli na yenye kutiwa chumvi.

Huweza kuwa na maana zaidi ya moja. Neno la misimu linalotumiwa sehemu moja linaweza kuwa na maana tofauti na linavyotumika mahali pengine.

Huhifadhi historia ya jamii hususa kuhusu maendeleo ya lugha (hasa pale inapoishia hata kukubaliwa katika lugha fulani).

Hupendeza sana miongoni mwa watumiaji wake. Hii ni kwa sababu ina mvuto mkubwa.

Wazee wakitumia misimu aina ya Sheng’ huonekana kama watovu wa nidhamu.

 

Misimu huundwa kwa namna ifuatavyo katika jamii:

Kuchanganya maneno ya lugha tofauti. Kwa mfano: Nilihata mat kwa maana ya Nilikosa daladala au matatu.

Kwa kuchanganya maneno kisha kuyasongoa. Kwa mfano: Mother  – masa.

Kutafsiri kijuujuu au kisisisi. Kwa mfano: Kudrive.

Kwa kutumia sauti za tanakali. Kwa mfano, Mtutu – bunduki (kutokana na mlio wake).

Kwa kutumia sitiari, kwa mfano: Ngoma – Ukimwi, golikipa – nyani.

Kufupisha maneno, kwa mfano, kompyuta –komp.

Kutokana na maneno ya kigeni, kwa mfano father kuwa fathe, brother – brathe.

Maneno kupewa maana mapya. Kwa mfano, chuma – gari mpya.

 

Sababu za kutumia misimu:

Hutumiwa kwa ajili ya kutaka mazungumzo yawe siri; yasieleweke kwa watu wengine.

Hutumiwa ili kufanya mambo mazito kuwa mepesi. Kwa mfano, mtu anapokusaidia kutenda jambo na atake kuhongwa anaweza kukuuliza, “Hata chai?” badala ya kukuuliza,”Mbona hunipi hongo?’’

[email protected]

Marejeo

Whiteley, W.H. (1969). Swahili: The Rise of a National Language. London: Methuen and Company Limited.

Chiraghdin, S., & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha ya kimataifa ikiwemo sifa...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Chimbuko na sababu za kutumia...

adminleo