• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya Wingi Lugha

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya Wingi Lugha

Na MARY WANGARI

KWA kufafanua maana ya wingi lugha tunasema ni hali ambapo mwanajamii ana uwezo wa kutumia lugha zaidi ya mbili kwa ufasaha.

Sababu ya kuwepo kwa wingi lugha inatokana na mambo yafuatayo:

Sababu za sera ya elimu ambapo mwanafuni huhitaji kujifunza lugha.

Watu wa jamii mbalimbali kutangamana.

Lugha moja kuwa na hadhi na staha ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Sababu za kiuchumi: watalii hujifunza Kiswahili wanapozuru mwambao wa Afrika Mashariki.

Ukuruba wa lugha kimaeneo ambapo mzawa wa lugha huwa na nafasi ya kumiliki lugha ya eneo fulani.

Sababu ya utekelezi: ili kuweza kutekeleza kazi fulani.

Dhana ya Ujozi Lugha

Ujozi lugha ni hali ambapo mwanajamii ana uwezo wa kutumia lugha mbili tofauti kwa ufasaha kama wazawa wa lugha hizo.

Dhana ya Diglosia

Diglosia ni hali ambapo katika jamii moja lugha mbili tofauti zimepewa majukumu tofauti maalumu; moja imepewa hadhi ya juu na nyingine hadhi yachini. Kwa mfano, katika nchi moja kuna lugha mbili tu nazo ni Kiingereza na lugha yao ya mama. Lugha ya Kiingereza nayo ikawa lugha rasmi ilhali lugha yao ya mama ikasalia tu kwa matumizi ya nyumbani.

Dhana ya Triglosia

Triglosia nayo hurejelea hali ya kuwepo na lugha tatu zilizo na majukumu tofauti katika jamii, kwa mfano, kuwa na lugha rasmi, lugha ya taifa na lugha ya elimu pekee.

Lafudhi (accent)

Lafudhi ni matamshi ya mzungumzaji yanayojitokeza kutokana na athari za lugha yake ya kwanza, lugha zinazomzunguka au maumbile katika ala za sauti. Kwa maneno mengine, lafudhi ni upekee unaojitokeza kwa mtu binafsi na huleta tofauti baina ya wasemaji au jamii.

[email protected]

Marejeo

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.

Ndungo, C. Mwai, W.(1991). Kiswahili: Historical Modern Development in Kiswahili. Nairobi: Nairobi University Press.

Mbaabu, I. (1996). Language Policy in East Africa: A Dependency Theory Perspective. Nairobi: Educational Research and Publications.

  • Tags

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya lugha sanifu katika...

Kenya U-17 yacharazwa 5-1 na Algeria

adminleo