• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
SHERIA: Wahitaji idhini ya mkeo kushiriki naye tendo la ndoa

SHERIA: Wahitaji idhini ya mkeo kushiriki naye tendo la ndoa

Na BENSON MATHEKA

JE, mume akishiriki tendo la ndoa na mkewe bila idhini yake inaweza kuchukuliwa kama tendo la ubakaji ? Na je, sheria inasema nini kuhusu ubakaji katika ndoa ? Hili ni swali la msomaji Jane akiwa Nakuru.

Nitaanza kwa kusema kuwa tendo la ndoa linapaswa kuwa kwa hiari hata kati ya wanandoa.

Hakuna anayepaswa kumlazimisha mtu kushiriki mapenzi naye. Mume akifanya mapenzi na mkewe kwa nguvu huwa anashiriki ubakaji na vilevile mke akimlazimisha mume kufanya mapenzi bila hiari huo ni ubakaji.

Hili ni tatizo kubwa miongoni mwa wanandoa kwa sababu watu wengi huchukulia ndoa kama leseni ya kufurahia tendo la ndoa wakati wowote wanaotaka.

Wengi wamekuwa wakidhulumiwa na wachumba wao na kuathirika kisaikolojia kwa sababu sheria ya dhuluma za kimapenzi ya Kenya haifafanui kuhusu ubakaji katika ndoa.

Inachukuliwa kuwa watu wakikubali kuoana huwa wanakubali kufanya mapenzi na wachumba wao na hawafai kuwanyima haki hii.

Hii ndiyo sababu mtu akidai alibakwa na mumewe huwa ni vigumu kuthibitisha ikiwa kweli alibakwa au mume alikuwa akipata haki yake ya ndoa.

Unyanyasaji

Hata hivyo, sheria hairuhusu unyanyasaji katika ndoa au dhuluma za aina yoyote ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kupata haki ya tendo la ndoa.

Kinachohitajika kwa wanandoa ni kuweka misingi ya ndoa yao kupitia mawasiliano ya hali ya juu kati yao ili kuepuka dhuluma katika ndoa ambazo zimefanya baadhi ya watu kupata majeraha au kuteseka kisaikolojia.

Haki katika ndoa haiwezi kupatikana kwa kukiuka haki ya mwingine.

Hapa ninamaanisha kuwa haki ya tendo la ndoa haifai kupatikana kwa kudhulumu mtu mwingine na kwa kufanya hivyo kumnyima nafasi ya kufurahia tendo la ndoa.

Japo sheria haifafanui jinsi ubakaji katika ndoa unavyopaswa kushughulikiwa na watu wengi hawajitokezi kulalamika, sheria hairuhusu mwanandoa kumshambulia na kudhulumu mwenzake.

You can share this post!

Kulikoni baadhi ya viongozi wa Jubilee walia eti...

MWANAMUME KAMILI: Ukipendwa pendeka, nayo macho ya pembeni...

adminleo