• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
UMBEA: Dalili tosha za mwanamume atakayekufanya uchukie ndoa

UMBEA: Dalili tosha za mwanamume atakayekufanya uchukie ndoa

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA ni heri ukosee njia utaelekezwa, kuliko kukosea kuoa ama kuolewa.

Changamoto huwa zaidi pale mwanamke anapokosea kuolewa na halafu aolewe na mwanaume asiyejiamini.

Kuna starehe pale mwanamume anapojiamini na kuonyesha kwa matendo kwa yule ampendaye.

Hata hivyo, wapo akina kaka ambao wanashindwa kabisa kujiamini, ikiwa na sababu mbalimbali ikiwemo elimu, maumbile, muonekano wa nje, uwezo wa kiuchumi na hata yule mwanamke aliyemuoa iwapo amemzidi kwa hayo ambayo yeye hana.

Mwanamke kuishi na mwanamume ambaye hajiamini huwa ni shughuli nzito kwani hata maelewano huwa ni shida, hata pale anajaribu kujenga na kumsaidia mumewe, anaweza kuonekana ana dharau ama kama unashindana naye.

Hivyo humuwia vigumu mwanamke kuwa na furaha kwani wakati wote anakuwa anajishuku.

Kuna wakati unaweza uone ndoa yako haina furaha, unajiuliza ni kwa nini?

Unashindwa sababu inayofanya usielewane na mumeo? Unajiuliza ni sababu gani imemfanya asiendelee kuwajibika katika familia, anakuvurumishia matusi kila akipata nafasi.

Yawezekana kabisa kwamba mumeo ama huyo mwenzako hajiamini.

Iwapo ulikuwa unajiuliza na unashindwa kuelewa, hizi hapa ni dalili za mwanaume asiyejiamini na iwapo utaelewa unaweza kuchukua hatua muafaka:

Kuwa na wasiwasi kila mara

Mwanamume wa aina hii huwa anatia shaka kwa kila jambo unalofanya. Kwake hakuna kitu utakifanya aone kama umekifanya kwa nia nzuri, ukitafuta kazi anasema unatafuta wanaume wengine, ukihudumia watoto anasema sababu uonekane una pesa. Haamini kuwa unaweza kufanya kitu bila kuwa na nia ya kumsaliti, kumfanya aonekane mbaya au kuonekana una kiburi kwake yeye hakuna kitu kizuri, kila unachokifanya lazima atafute nia mbaya ndani yake.

Anahesabu na kutoa mfano kwa kila jambo unalofanya

Hapa sio mabaya tu, hata mazuri pia yamo, kila kitu unachokifanya atakilinganisha na alichokifanya yeye. Kauli zake zinaweza kuwa “wewe umetoa kiasi fulani nami nimetoa hiki, umeenda kwenu mara mbili mimi hata sijaenda, unafanya hiki mimi sijafanya.”
Kwake hata kufurahi, akikuona una furaha kuliko yeye basi hukasirika, ukiwa na marafiki wengi kuliko yeye basi ni shida pia, ndugu zako wakija kwenu mara nyingi ni maneno pia.

Hataki na hapendi kukubali makosa, kila afanyalo yeye ni sawa

Anaamini kuwa yeye hakosei na kila mtu hasa wewe ndiyo hukosea, kila akifanya kitu atahakikisha anakionyesha kama kitu kizuri, hakubali akakosea au kukiwa na tatizo alilolisababisha yeye hataki mkae na kulisuluhisha atajaribu kulitetea ili tu aonekane yeye yuko sawa.

Mara nyingi anaishia kukulaumu wewe hata kwa makosa ambayo hayakuhusu, hata kwa makosa ambayo alifanya yeye.

Hapa ndipo anaweza kusema alichepuka na mwanamke mwingine sababu umenenepa sana, mapishi yako sio mazuri tena ama labda humvutii tena.

Ana unafiki, wakija wageni anajidai mume bora

Mwanaume wa aina hii, pale mke anapokuwa na tatizo hawezi kusaidia na hata akisaidia ni kwa masimango lakini kwa majirani hata kama hajaombwa, kwa ndugu zake na watu kando atakua kimbelembele hata kama ndani alikuambia hana hela, kwa watu atataka kuonekana anacho, kuonekana mwanaume atatoa.

Anafurahia kuona huna furaha

Kwamba kila mara anataka kukuumiza, anataka ulalamike na kwakuwa yeye hana furaha basi atataka nawe usiwe na furaha.

[email protected]

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Ukipendwa pendeka, nayo macho ya pembeni...

AFCON: Kenya yatupwa katika chaka la simba

adminleo