• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Shujaa yaning’inia pabaya Raga ya Dunia

Shujaa yaning’inia pabaya Raga ya Dunia

Na GEOFFREY ANENE

Kenya inaendelea kuning’inia pabaya kwenye Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 licha ya kufunga ziara ya Singapore Sevens kwa kuponda Uhispania 21-5 na kuambulia alama tatu kwenye duru hii ya nane, Jumapili.

Timu hiyo almaarufu kama Shujaa imesalia katika nafasi ya 13 duniani ikiwa na jumla ya alama 26, moja mbele ya Wales iliyojiongezea alama tano nchini Singapore.

Shujaa ya kocha Paul Murunga iliponea kumaliza ziara ya Singapore mkiani baada ya kutolewa kijasho chembamba na Japan kabla ya kuichapa 31-24 katika nusu-fainali ya kuorodheshwa kutoka nafasi ya 13 hadi 16. Japan sasa inashikilia nafasi ya kutemwa ya nambari 15 kwa alama 22 baada ya kubadilishana na Wales.

Msimu huu wote Kenya imekuwa ikishikilia mojawapo ya nafasi tatu za mwisho. Ikiwa na ufahamu kupoteza dhidi ya Japan katika nusu-fainali ya kutafuta timu nne za mwisho mjini Singapore kutaisukuma mkiani, Shujaa ilipigana kufa kupona na kuizamisha 31-24.

Nahodha Jeffrey Otieno pamoja na Daniel Taabu walichangia miguso miwili kila mmoja. Mguso wa Andrew Amonde na mguso na mkwaju kutoka kwa Taabu dakika tatu za kwanza ziliipa Kenya uongozi wa alama 12-0.

Japan ilipunguza mwanya huo kupitia mguso na mwakaju kutoka kwa Katsuyuki Sakai dakika mbili baadaye kabla ya Kenya kufurahia kuenda mapumzikoni kifua mbele 19-7 baada ya Taabu kuongeza mguso na mkwaju wake.

Hata hivyo, ilirejea kipindi cha pili mnyama tofauti ikisawazisha 24-24 baada ya kupata mguso kupitia Michael Toloke na kuongeza miguso mingine miwili kupitia kwa Siosifa Lisala na mkwaju kutoka kwa Sakai baada ya Otieno kufungia Shujaa mguso wa nne.

Otieno alihakikishia Kenya ushindi pale alipopachika mguso sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kulia, huku Taabu akiongeza mkwaju. Ilizamisha Uhispania kupitia miguso ya Vincent Onyala, Bush Mwale na Taabu, ambaye pia lifunga mikwaju ya miguso hiyo.

Uhispania ilijiliwaza na mguso bila mkwaju kutoka kwa Alejandro Alonso. Wakati mmoja wa mechi, Kenya ilikuwa chini wachezaji sita baada ya Mwale kuonyeshwa kadi ya njano, lakini ililinda ngome yake vyema na kujizolea ushindi huo muhimu.

Kenya italazimika kujikakamua vilivyo katika duru mbili za mwisho zitakazofanyika katika miji ya London nchini Uingereza (Mei 26-26) na Paris nchini Ufaransa (Juni 1-2).

You can share this post!

Kenya yapoteza mataji ya wanaume na wanawake Paris Marathon

Ugawaji usiofaa wa fedha kwa shule wasukuma walimu kufanya...

adminleo