• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
CHARLENE WANGUI: Nilikuwa mwoga sana lakini sasa nalenga Oscars

CHARLENE WANGUI: Nilikuwa mwoga sana lakini sasa nalenga Oscars

Na JOHN KIMWERE

ANAODHORESHWA miongoni mwa wasanii wanaolenga kutimiza makubwa katika sekta ya uigizaji hapa nchini.

Anasema tangu akiwa mdogo alitamani kuhitimu kuwa rubani ili kupata nafasi kupitia hewani kwenye shughuli za kikazi. Anadokeza kuwa amekusudia kujituma kisabuni kuhakikisha ametwaa Oscars Awards ambayo ni kati ya za hadhi tuzo za kimataifa.

Charlene Wangui ambaye licha ya kuhitimu kwa shahada ya digrii kama mwanahabari ni kati ya wasanii ambao huigiza kwenye kipindi cha Tahidi High akifahamika kama Mellisa ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.

Vilevile hushiriki matangazo ya kibiashara bila kusahau kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.

Binti huyu anashikilia kwamba waigizaji wanaokuja wanastahili kusoma maana bila elimu ni vigumu kwao kumakinika kwenye shughuli za maigizo.

Anajivunia kushiriki filamu nyingi tu tangu aanze shughuli za maigizo mwaka 2011. Kando na uigizaji dada huyu anamiliki lebo iitwayo ‘Charmay’ ambapo hushona mavazi mapya ya wanaume na wanawake.

”Nikiwa mdogo nilikuwa muoga sana singekubali kusimama mbele ya watu wengi lakini nilipata ujasiri mwaka 2010 wakati kundi la Mabingwa Player Theatre lilipozuru shuleni mwetu,” alisema na kuongeza kuwa viongozi wake ndio waliomtia motisha walipomweleza kwamba anazo vigezo vya kuwa mwigizaji.

Kando na Tahidi High, binti huyu anajivunia kuigiza filamu nyingi tu ikiwamo Waridi iliyokuwa ikionyeshwa kupitia KTN TV, Sumu la Penzi na Urembo (Maisha Magic) kati ya zingine.

Charlene Wangui mwigizaji anayelenga tuzo za Oscars. Picha/ John Kimwere

“Nakumbuka niliwahi shiriki filamu fupi nyingi tu chini ya Talent Shortfilms ambazo hadi muda huu hunifurahisha sana kwa jinsi nilivyoweza kujituma na kufanya yangu yote,” alisema.

Kwenye matangazo ya kibiashara amefanya kazi na kampuni ya simu za rununu ya Safaricom, Airtel bila kuweka katika kaburi la sahau Zuku.

Kipusa huyu amekusudia kumilika brandi yake miaka ijayo ili kutoa ajira kwa waigizaji wa kike wanaokuja.

”Hakika huwahurumia sana wasichana wenzangu ambao hujitokeza na kuniomba niwasaidie jinsi wanavyoweza kupata ajira ya uigizaji ilhali sina uwezo maana mimi siyo bosi popote,” alisema na kuongeza hali hiyo humtia ari na kutamani kumiliki brandi yake siku sijazo.

Anaamini kwamba kipaji chake kitamfikisha mbali hasa anakumbuka amepitia safari ndefu tangu aanze kujituma kwenye masuala ya maigizo.

Anasema huvutiwa na kazi yake staa wa maigizo mzawa wa Marekani Leonard Di Caprio ambaye ameigiza filamu kama ‘Titanic,’ ‘Inception,’ ‘Shutter,’ ‘The Beach,‘ na ‘Catch Me If You Can,’ kati ya zingine.

Katika mpango mzima anashauri waigizaji wa kike watambue dhamani yao na wakomeshe mtindo wa kujishusha kwa wanaume ndipo wapate nafasi za kuigiza.

You can share this post!

Bao tamu la Wanyama lachangamsha mitandao

Euronuts kutetea ubingwa Chapa Dimba Mkoa wa Kati

adminleo