• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Familia ya Ivy yaomba msaada kugharimia mazishi

Familia ya Ivy yaomba msaada kugharimia mazishi

MARY WAMBUI, JEREMIAH KIPLANG’AT na EDITH CHEPGENO

FAMILIA ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi aliyeuawa wiki jana wameomba msaada wa kifedha kutoka kwa umma ili kugharimia mahitaji wakati wa mazishi yake yanayotarajiwa kufanywa Alhamisi.

Msemaji wa familia hiyo, Bw John King’ori ambaye ni mjombake marehemu Ivy Wangechi, Jumapili alisema kuwa wanatarajia halaiki kubwa ya watu kwenye mazishi hayo na pia wangependa kumpa mazishi ya heshima, mahitaji ambayo yatagharimu pesa nyingi kutimiza.

“Kutokana na matukio yaliyozingira kifo chake, mazishi yake hayatakuwa ya kawaida. Tunawatarajia kati ya waombelezaji 1,500 hadi 2,000 hali ambayo inatuweka katika ulazima wa kutumia kiasi kikubwa cha fedha. Tunawaomba wahisani watume fedha kupitia nambari 855050 ili tusaidiwe kumpa mazishi ya heshima,” akasema Bw King’ori.

Mamake marehemu, Bi Winfred Waithera naye alishutumu wanaoeneza uvumi katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha mwanawe na kuwataka kukoma tabia hiyo mara moja kwa kuwa inaizidishia familia hiyo machungu.

“Punde tu baada ya marehemu kukata roho, hata kabla ya familia kupashwa habari, inasikitisha kuwa watu walivamia mitandao ya kijamii na kueneza uvumi kuhusu mtu wasiyemjua. Tunawaomba Wakenya wakomeshe tabia hiyo,” akasema Bi Waithera.

Wakati uo huo, mwanamume aliyemuua Bi Wagechi, Naftali Kinuthia, leo anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Eldoret baada ya makachero kurekodi taarifa kutoka kwa mashahidi wikendi.

Bw Kinuthia aliruhusiwa kuondoka katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi Ijumaa huku maafisa wa polisi wakiahidi kumfanyia uchunguzi kabla ya kumpeleka kortini leo.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Moi Bw Wilson Aruasa, Bw Kinuthia alikuwa amelazwa hospitalini humo tangu Jumanne wiki jana baada ya kupigwa na umati kutokana na hatua yake ya kumvamia Bi Wangechi na kumuua.

Siku ya Ijumaa Afisa Mkuu wa Polisi wa Eldoret Mashariki Lucy Kananu vile vile aliwaomba wenye habari muhimu zitakazosaidia katika uchunguzi kujitokeza na kuziwasilisha kwa polisi kabla ya Bw Kinuthia kupelekwa kortini.

Kati ya waliohojiwa wikendi ni marafikize marehemu na wapitanjia walioshuhudia tukio hilo katika kitengo cha kuwapokea wagonjwa kwenye hospitali ya Moi.

You can share this post!

Joho ametosha mboga kuongoza Kenya 2022, asema Atwoli

Hali ngumu zaidi baada ya bei ya mafuta kupanda tena

adminleo