• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Joho ametosha mboga kuongoza Kenya 2022, asema Atwoli

Joho ametosha mboga kuongoza Kenya 2022, asema Atwoli

Na KALUME KAZUNGU

AZMA ya Gavana wa Mombasa, Hassan Joho kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 imeungwa mkono na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli.

Akihutubia umma katika eneo la Mkunguni kisiwani Lamu wakati alipoongoza hafla ya kuchangisha fedha kwa vikundi vya akina mama, Bw Atwoli alimtaja Joho kuwa mtu anayetosha kuongoza nchi hii.

Alisema tangu wanasiasa ambao ni vigogo wa Pwani, akiwemo Ronald Ngala na Shariff Nassir kufariki, Wapwani sasa wamebarikiwa na kiongozi shupavu ambaye ni Joho.

Aliwataka Wapwani na Kenya kwa jumla kusimama kidete ili kuona kwamba Bw Joho anashinda uchaguzi ujao na kuwa miongoni mwa watakaounda serikali ijayo.

Aliahidi kujitahidi kuhakikisha Bw Joho na viongozi wengine wote ambao wamekuwa wakisimamia haki nchini watashinda uchaguzini ili kuunda serikali ijayo.

“Wapwani nawataka muwe mkimsikiliza na ikiwa hamtafanya hivyo shauri yenu. Muislamu yeyote ana haki ya kutawala Kenya akiwa Mkenya. Kwa hivyo kwanza tubadilishe katiba na mkae mkijua kuwa uongozi wa serikali inayokuja Joho yuko ndani kabisa,” akasema Bw Atwoli.

Aidha alimtahadharisha Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Aden Duale kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais, akisisitiza kuwa ataanguka.

“Iwapo ni kiongozi mwenye nia ya kuwa Rais wa Kenya na sera zako zinapiga vita vyama vya wafanyakazi, ujue umepotoka na hupati kura yoyote. Namwambia Duale aendeleze ndoto yake ya kugombea urais lakini kupata ajue hapati,” akasema Bw Atwoli.

Kwa upande wake, Gavana Joho alisema hakuna lolote litakalomzuia kugombea urais ifikapo 2022.

Alisema nia yake ni kuongoza nchi hii ili kumaliza maovu yanayoendelea kuathiri taifa hili, ikiwemo janga la ufisadi.

“Nataka kuwaambia wazi leo hii kwamba sitishwi na yeyote. Mimi nitakuwa debeni kugombea urais ifikapo 2022. Ninajiamini pakubwa. Cha msingi hasa kwetu sisi wakazi wa Pwani ni kuwa na msimamo mmoja. Tusikubali kugawanywa kwani wengi watakuja na hata kumwaga pesa. Chukueni fedha hizo lakini mjue cha kufanya. Tunataka wale wanaotangatanga waachwe na mshangao,” akasema Bw Joho.

Nao viongozi walioandamana na Bw Atwoli na Bw Joho wakati wa ziara ya Lamu, ikiwemo Mbunge wa Kasipul Kabondo, Bi Eve Obara, Mishi Mboko (Likoni), Spika wa Bunge la Nairobi, Bi Beatrice Elachi, Mbunge Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo, Bi Elsie Muhanda wa Kakamega, Asha Hussein wa Mombasa na wengineo waliahidi kushirikiana ili kuona kwamba ndoto ya Joho ya kuongoza nchi hii inatimia.

“Joho ni mtoto wetu na ndugu yetu. Tutasimama na yeye katika hali zote zile. Tunataka awe mmoja wa watakaounda serikali ijayo ili Wapwani pia tuwe na cha kujivunia,” akasema Bi Mboko.

You can share this post!

Wanyamapori wetu ni zawadi kutoka kwa Mola, tuilinde...

Familia ya Ivy yaomba msaada kugharimia mazishi

adminleo