• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Chansela mpya aahidi kulainisha Chuo Kikuu cha Egerton

Chansela mpya aahidi kulainisha Chuo Kikuu cha Egerton

RICHARD MAOSI NA FRANCIS MUREITHI

HATIMAYE Chuo Kikuu Cha Egerton kimepata chansela mpya baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua mfanyabiashara maarufu Narendra Raval kwa wadhifa huo.

Hii inajiri miezi michache tu baada ya wanafunzi kushinikiza chuo kufanya mabadiliko wakilalamikia kukosa huduma bora chuoni humo.

Tetesi zilizoibuka ni pamoja na miradi iliyoanzishwa na utawala wa hapo awali kusimama, huku wasimamizi wa chuo wakinyoshewa kidole cha lawama kwa kutumia fedha kiholela.

Baada ya kukaribishwa rasmi siku ya Ijumaa, Raval alisema ajenda yake kuu ni kurejesha hadhi ya Egerton, bali na kuwasaidia wanafunzi wanaotokchasea kwenye familia maskini wapate ujuzi wa kujiajiri.

Narendra Raval akichukuliwa futi za kofia na gauni la chansela kuvaliwa wakati wa mahafala. Picha/ Richard Maosi

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, alieleza alikuwa tayari kuleta maridhiano na kutatua mizozo ya uongozi inayotatiza uendeshaji kazi.

Alisema yuko katika mstari wa mbele kuleta suluhu ya kudumu ili kupunguza uhasama baina ya uongozi na wanafunzi.

Raval alisema rais alimteua akiwa na azma ya kuwapa wanafunzi matumaini na kwa upande mwingine aliwahimiza wajivunie chuo chao na kujijengea jina ndani na nje ya Kaunti ya Nakuru.

“Japo misukosuko ni mingi, ninaahidi kutengeneza taswira nzuri, vivyo tushikane mikono na kutekeleza mabadiliko,” alisema.

Chansela akipokezwa na afisa wa maktaba ya chuo nakala ya mojawapo ya vitabu alivyoandika. Picha/ Richard Maosi

Alisema hayuko tayari kuanzisha miradi mingine ila kuendeleza ile iliyoanzishwa lakini ikakwama.

Aliahidi kushirikiana na wafadhili wa kibinafsi na serikali ya kitaifa kukwamua miradi ambayo ilikuwa imesimama.

Baadaye alipata fursa ya kutangamana na Seneti ya Chuo ambapo aliwataka wahadhiri kubuni mbinu za kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatosheleza mahitaji ya wanafunzi.

Bw Raval anakuja wakati ambapo Chuo Cha Egerton kinakabiliwa na changamoto nyingi,hususan uhaba wa fedha.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza nasi walisema gharama ya maisha ndani ya Chuo ilikuwa imepanda, kiasi kwamba wengi walikuwa wameamua kupangisha vyumba nje.

Chansela Narendra Raval (kati) akikaribishwa rasmi na Naibu Chansela Profesa Rose Mwonya. Picha/ Richard Maosi

Hadi tukizungumza umeme katika baadhi ya vyumba vyao vya malazi ulikuwa umekatwa na kampuni ya Kenya Power kutokana na madeni.

Kiongozi wa wanafunzi Silas Makokha aliomba uongozi mpya kutatua swala la ukosefu wa umeme ulioadhiri sehemu kubwa ya Chuo.

“Hatutakubali kuona taasisi ya umma kiwango hiki ikiendelea kudorora kwa sababu ya mapungufu ya umeme,” aliongezea.

Alisema chuo hakijakuwa kikishirikiana na wanafunzi vilivyo huku tume ya mawasiliano ikiwa imefeli na ndio sababu rabsha zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

Seneti mpya ya Chuo Kikuu cha Egerton. Picha/ Richard Maosi

Katika hafla hiyo chansela aliwahimiza vijana wasitegemee mitandao ya kijamii kwani haitawasaidia kutatua matatizo yao.

“Katika maisha kitu cha msingi ni kuwa na malengo ya kukabili changamoto, jinsi zinavyokuja,” alisema.

Aliwatahadharisha wanafunzi kujiepusha na michezo ya kamari na badala yake wawekeze wakati wao mwingi katika masomo.

Alisema angesalimisha asilimia mia ya mshahara wake , kukidhi karo ya wanafunzi wasiweza kumudu gharama ya masomo.

Naibu Chansela Profesa Rose Mwonya alisema anatarajia chansela Raval ataleta mageuzi makubwa chuoni hasa ikizingatiwa kumekuwa na sintofahamu katika majukumu.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Egerton wakitagusana na familia ya chansela wao mpya. Picha/ Richard Maosi

Aidha akiwa mtaalam kwenye sekta ya viwanda, sio tu Kenya bali Afrika Mashariki, chansela huyo mpya anatarajiwa kuleta ujuzi wake wa ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi bali na kuwasaidia wapanue mawazo yao.

“Hakika familia ya Egerton inafurahia kupata chansela mpya mwenye tajiriba pana katika uwanja wa maisha,” akasema.

Miongoni mwa ajenda nyinginezo ni pamoja na ustawishaji wa miundo mbinu ya kisasa na kuwahakikishia wanafunzi usalama.

Chuo Kikuu Cha Egerton kilibuniwa na Lord Egerton miaka 75 iliyopita. Chansela Raval atadumu kwa kipindi cha miaka mitano.

You can share this post!

155 waliobobea katika KCSE 2018 kusomea udaktari

Idara lawamani baada ya mbegu kukosa kuota

adminleo