• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
AKILIMALI: Kilimo cha pilipili mboga kimemuinua kimapato na kimaisha

AKILIMALI: Kilimo cha pilipili mboga kimemuinua kimapato na kimaisha

Na SAMMY WAWERU

NYERI ni miongoni mwa kaunti zinazotegemewa nchini kwa kilimo cha kahawa na majanichai.

Pia, kaunti hii ni miongoni mwa kapu la mboga na matunda kwa sababu ya hali yake bora ya anga kukuza mazao hayo.

Thaithi, kijiji kilichoko karibu kilomita moja kutoka barabara kuu ya Karatina-Nyeri, kila migunda ya wakazi imesheheni kahawa.

Wengi wa wakulima wana matunda kama vile karakara, maparachichi, maembe na ndizi.

Bw David Karira Ndiritu, mkulima wa pilipili mboga aina ya Red night akiwa shambani eneo la Thaithi, Karatina kaunti ya Nyeri. Picha/ Sammy Waweru

Katika shamba la familia ya Bw David Karira Ndiritu, limepambwa kwa kahawa, maparachichi, maembe na ndizi. Hata hivyo, katika kipande cha Karira, anafanya kilimo cha kipekee.

Kwenye mikahawa na pembezoni mwake, anakuza matunda aina ya tomarillo-yanayoaminika kuongeza damu mwili.

Mkulima huyu na ambaye pia ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Kiarithaini, anakuza pilipili mboga katika kifungulio (greenhouse).

Alianza kilimo cha kiungo hiki cha mapishi 2011, kama njia moja ya kupiga jeki mapato yake. Anasema katika kaunti ya Nyeri ni wakulima wawili pekee waliokuza aina hii ya pilipili.

“Ilinigharimu mtaji wa Sh250,000 kuanzisha kilimo cha pilipili mboga. Nilianza na kifungulio chenye ukubwa wa futi 80 kwa 40, na ambacho nilijiundia,” anadokeza Bw Kariira.

Anafichua kuwa mtaji huo baada ya mwaka mmoja na nusu ulimpa mapato ya karibu Sh1 milioni, hii ikiwa na maana kuwa faida aliyotia kibindoni ni Sh750,000.

Upanzi

Kwa sababu ya upungufu wa shamba, mkulima huyu alilazimika kupunguza kifungulio alichotangulia nacho kikawa cha futi 50 kwa 28.

Juu, amekiezeka kwa karatasi za plastiki zinazoruhusu mwangaza na joto kupenyeza ndani. Kandokando, kiambazani, pia kimeundwa kwa karatasi za plastiki na neti zinazoruhusu hewa kuingia na kutoka.

Bw Kariira anasema pilipili mboga ni miongoni mwa mimea rahisi mno kupanda na kutunza. Maandalizi ya eneo la upanzi, huchimba futi mbili kuenda chini.

“Mbolea humwagwa na kuchanganywa na udongo sawasawa. Maji yanamwagiliwa na kulipa eneo la upanzi muda wa wiki mbili hivi,” anasema.

Huandaa makundi (beds) ya laini mbilimbili za mashimo.

Nafasi ya laini moja hadi nyingine ni futi moja. Mashimo anayochimba kwa kidole, baada ya kumwaga maji, yana nafasi ya kati ya futi moja na nusu hadi mbili.

Kutoka kundi moja hadi lingine, ameyapa kipimo cha futi moja na nusu.

Kuna njia mbili za kupanda pilipili mboga; kuandaa miche yake kitaluni au mbegu moja kwa moja mashimoni.

Kulingana na Karira ni kuwa upandaji wa mbegu moja kwa moja, ndio mbinu bora kwa kuwa miche huchipuka ikiwa yenye nguvu na haitapitishwa shughuli ya kuihamisha.

“Miche inapohamishwa kutoka kitalu hadi eneo la upanzi, hujikokota kushika kasi ya kumea,” anaeleza.

Hupanda pilipili mboga aina ya Red night, kutoka kwa kampuni ya Amiran.

Red night inadumu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu mkulima akiendelea kuvuna,” anasema.

Changamoto

Mbegu zichipukapo, changamoto kuu huwa ni shambulizi la wadudu kama vile vithiripi, viwavi na mende.

Mkulima huyu anasema wadudu hao hukata mimea ikiwa michanga.

Meshack Wachira, mtaalamu wa masuala ya kilimo anashauri mkulima kutumia dawa mbalimbali za kuwadhibiti.

“Ni vyema dawa ziwe zikibadilishwa ili kudhibiti wadudu hao waharibifu,” asema Bw Wachira.

Karira anasema siri ya kufanikisha kilimo cha pilipili mboga ni kuzilisha kwa mbolea, hasa ile hai na kuzinyunyizia maji ya kutosha. Mkulima anahimizwa kutumia mbolea iliyoiva sawasawa, na iliyo salama.

“Mbolea inapaswa kuchunguzwa kwa kuwa kuna zingine husambaza magonjwa na wadudu. Mimi hutumia ya mbuzi na kuku,” adokeza Karira.

Changamoto nyingine katika kilimo cha pilipili mboga ni ugonjwa wa Bacterial Wilt, ambao mkulima huyu anasema hauna dawa za kuudhibiti. Ili kuukabili, baada ya kung’oa mipilipili inapopunguza na kuisha mazao hukipa kifungulio muda wa miezi sita na kufunika eneo lote kwa karatasi za plastiki.

Kando na kusaidia kuondoa ugonjwa huo udongoni, anasema hatua hii pia huua wadudu waliomo udongoni.

Hupogoa matawi, ambapo husalia na matatu pekee.

Red night hurefuka hadi kimo cha futi sita, na huisimamisha kwa miti na kuifunga kwa nyuzi ili kustahimili uzito wa mazao.

Baada ya kati ya siku 75-85, huanza kuvuna pilipili.

Ingawa Karira anasema huanza kuzalisha kiduchu mwezi mmoja baada ya upanzi.

Huvuna kwa muda wa miezi mitatu mfululizo, kila wiki akipata zaidi ya kilo 240.

Kilo moja haipungui Sh100, wateja wake wakiwa wafanyabiashara wa masoko ya Karatina na Nyeri, wakijumuisha rejareja na wa kijumla.

Aidha, maduka ya bidhaa za kilimo ya Zucchini jijini Nairobi pia hununua mazao yake.

Kila baada ya miezi mitatu hukata mipilipili futi 3 au 4 kutoka ardhini. Matawi huchipuka wiki mbili baadaye, na kwa muda wa mwezi mmoja na nusu huzalisha pilipili.

Kwa mwaka huwa na misimu mitatu. Huing’oa baada ya mwaka mmoja na nusu ili kupanda mingine.

Pembezoni mwa kifungulio, mkulima huyu amechimba shimo lenye urefu wa zaidi ya futi 100 ambapo hutumia mfumo wa mifereji (Drip irrigation) kunyunyizia mimea ya maji.

Udongo wake ni tifutifu nyekundu, (red soil).

Kabla ya kuanza kukuza pilipili mboga, alipimiwa udongo wa shamba lake katika maabara ya kilimo, jambo analohimiza wakulima kutilia maanani.

You can share this post!

Mshindi wa EPL ni hadi siku ya mwisho – Klopp

Shujaa kupigania tiketi ya Olimpiki kwenye Kombe la Afrika

adminleo