• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Shule kutoka mataifa 8 zakongamana Juja kwa mashindano

Shule kutoka mataifa 8 zakongamana Juja kwa mashindano

Na LAWRENCE ONGARO

SHULE za Upili kutoka nchi tofauti zilikongamana Katika shule ya Upili ya Juja Preparatory and Senior School, kwa mashindano ya kujieleza ya The 4th Mwalimu Nyerere Debating Championship.

Mashindano ya aina hiyo ndiyo ya mwanzo kuendeshwa nchini na yalijumuisha nchi 8 kutoka bara la Afrika.

Baadhi ya nchi zilizohudhuria kongamano hilo la siku nne zilikuwa Tanzania, Uganda, Zimbabwe, Namibia, Botswana, Rwanda na Afrika Kusini.

Maswala muhimu wanafunzi walijihusisha kujadili ni maswala ya nchi kama uchumi, maisha na anasa za ulimwengu kwa jumla.

Mkurugenzi mkuu wa Kenya National Debates Council (KNDC), Bi Rose Ndichu, alisema mashindano hayo ni muhimu sana kwa wanafunzi kwa sababu inawapa msukumo wa kujieleza wazi katika umati bila kuwa na wasiwasi wowote.

“Tungetaka kuona mashindano ya aina hii yakiendeshwa mara moja kwa mwaka ili kuwapa wanafunzi mwongozo mzuri wa kuwa watu wa kutegemewa siku zijazo. Mwanafunzi akiwa mkakamavu katika kujieleza kwake bila shaka hata maisha yake ya badaye yataimarika,” alisema Bi Ndichu.

Alisema uongozi unapaliliwa katika umri mchanga kama wanafunzi hawa na kwa hivyo ni vyema walimu wao wawe katika mstari wa mbele kuwakuza ili wawe watu wa kujieleza bila wasiwasi.

Mara ya mwanzo kongamano hilo la Mwalimu Nyerere debating Championship, kuzinduliwa ilifanyika nchini Tanzania jijini Dar-es Salaam, mwaka wa 2018.

Mkurugenzi wa shule ya Juja Preparatory, Dkt Richard Muigai akihutubia walioshiriki katika kongamano hilo. Picha/ Lawrence Ongaro

“Mashindano ya aina hii ni muhimu kwa wanafunzi wa shule za upili ambapo wanapofika katika vyuo vya juu wanakuwa wamepevuka kimawazo na njinsi ya kujieleza bila wasiwasi,” alisema Bi Ndichu.

Alisema katika kikundi hicho ndiko tutapata wanasiasa na viongozi wenye maono ambao watakuwa tayari kujieleza kwa umma bila kuwa na tashwishi yoyote.

Naye Dkt Joseph Ng’ang’a alisema shule za upili zinastahili kuwapa wanafunzi mwongozo jinsi ya kuwa na weledi wa kujieleza mbele ya umati, ili wakijitosa katika ulimwengu wa ushindani mkali wanakuwa katika mstari wa mbele.

Kongamano hilo liliendelea kwa siku nne mfululizo huku likifunga milango zake mnamo Jumapili katika shule ya Juja Preparatory and Senior School Juja.

Dkt Ng’ang’a, alisema kuna haja ya walimu kuwanoa wanafunzi hao kuwa wasomi kama kina Mahatma Gandhi wa India, marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Martin Luther King.

“Tungetaka tuwe na wasomi waliosikika na kuenziwa na wengi kama hao waliotajwa na kwa hivyo wanafunzi wanastahili kujitia moyo kufikia kiwangto chao.”

Mwalimu mkuu wa shule ya Juja Preparatory Bw Joseph Irungu, alisema ni heshima kubwa sana kuzikaribisha nchi hizo katika shule hiyo kutokana na vifaa vya hali ya juu yaliyoko huko.

Alisema pia shule hiyo iko katika mstari wa mbele katika mtaala wa 8-4-4 na masomo ya IGCSE.

Ilidaiwa kuwa nchi zilizojizatiti na kufanya vyema zitapangiwa mashindano mengine katika nchi za nje ili wanafunzi wapate ujuzi zaidi jinsi wanavyostahili kujieleza mbele ya umati bila kubabaika.

You can share this post!

Wafanyakazi wa Sony Sugar wagoma kudai malipo

Auba alenga kumaliza msimu kwa mabao mengi zaidi

adminleo