• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Msikubali fedha za wizi makanisani na misikitini, Atwoli aonya

Msikubali fedha za wizi makanisani na misikitini, Atwoli aonya

NA KALUME KAZUNGU

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Francis Atwoli, amewakemea viongozi wa kidini wanaokubali kupokea fedha za wizi makanisani na misikitini, akisema hicho ni kinyume cha maadili ya kidini.

Akizungumza mjini Lamu, Bw Atwoli alisema haikubaliki kwa kiongozi wa kidini, iwe ni imamu msikitini, padre au pasta makanisani kukubali kupokea fedha za ufisadi na wizi na kuziombea kwenye madhabahu zao.

Alisema kufanya hivyo ni sawa na kujilaani, hivyo akawataka viongozi wa kidini kujiepusha na fedha hizo ambazo mara nyingi hutolewa na wanasiasa na viongozi wengine fisadi serikalini wakati wanapozuru misikitini na makanisani.

Alisema ni heri viongozi wa kidini kubaki vile walivyo na umaskini wao endapo ni lazima wao kupokea fedha zz wanasiasa, hasa wale ambao mara nyingi hutafuta pesa hizo kwa njia isiyo ya maadili yanayomridhisha Mwenyezi Mungu.

“Kuna baadhi ya viongozi hapa nchini ambao wamekuwa wakitangatanga makanisani na misikitini kufanya harambee au kutoa sadaka zao kwenye nyumba hizo za kidini. Ninawaambia maimamu na masheikh misikitini na mapadri na mapasta, iwe ni katoliki, protestanti au dini yoyote ile.

“Msikubali kupokea fedha za wizi na kuziombea kwenye nyumba zenu za ibada. Heri kubaki vile mlivyo kuliko kupokea fedha hizo ambazo zinatafutwa katika mazingira machafu yasiyomridhisha Mwenyezi Mungu,” akasema Bw Atwoli.

Katibu huyo wa COTU aidha alijigamba kwa kudai kuwa fedha zote ambazo yeye hutoa kama mchango kwenye hafla za harambee, kanisani na maeneo mengine huwa amezipata kupitia jasho lake.

“Mimi fedha zangu ni safi. Sijadhulumu mtu. Hii ndiyo sababu ikiwa unataka kunialika kwa mchango au harambee yoyote ile, lazima unijulishe mapema ili nijipange. Niweke fedha zangu polepole. Siibii mtu. Hata mke wangu mwenyewe huwa simwambii anipe fedha niende kutoa kwa harambee. Fedha zangu ni zangu na huzikusanya mwenyewe pole pole kwa muda wa kutosha kabla ya kuzitoa kwa harambee,” akasema Bw Atwoli.

Kauli yake iliungwa mkono na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, aliyemtaja Bw Atwoli kuwa mtu anayetambulika kwa kufanya mambo yake kwa njia ya haki na uwazi nchini kinyume na wengine.

“Huyu mzee ninampenda kwa tabia yake ya kusimama na ukweli. Yuko na fedha zake. Haibii au kudhulumu mtu. Fedha zake ni safi. Hapiganii kiti chochote cha uongozi, iwe ni Rais, Gavana, Mbunge, Seneta, Mwakilishi wa Wadi nakadhalika. Ni mtu anayetambulika kwa maadili yake mema nchini,” akasema Bw Joho.

You can share this post!

Auba alenga kumaliza msimu kwa mabao mengi zaidi

Barcelona wasema hawamtaki Griezmann

adminleo