• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
IEBC yatuma wawakilishi katika uchaguzi wa wanachuo wa Egerton

IEBC yatuma wawakilishi katika uchaguzi wa wanachuo wa Egerton

NA RICHARD MAOSI

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton, Jumanne walishiriki katika shughuli ya kuchagua viongozi wao katika bewa kuu eneo la Njoro.

Katika operesheni hiyo Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), ililituma wawakilishi waliopata nafasi ya kushuhudia zoezi zima likiendelea.

Uchaguzi ulianza asubuhi mwendo wa saa 6.00, milolongo mirefu ikishuhudiwa katika kila kitivo, lakini hata hivyo masomo yaliendelea kama kawaida.

Kulingana na Profesa Julius Kipkemboi, mhadhiri anayesimamia zoezi la uchaguzi huru na wa haki, alisema wanafunzi walikuwa wamehamasishwa vya kutosha kabla ya kuchagua viongozi kwa mujibu wa katiba.

Alisema mchakato mzima unazingatia uwakilishaji wa kila dini ,jinsia na utendaji kazi bila kuingilia idara nyingineyo.

Karani akitayarisha orodha ya wapigakura. Picha/ Richard Maosi

Chuo hakikuingilia zoezi la uchaguzi,vinara wa wanafunzi pamoja na walinzi wakishika doria kuhakikisha usalama hali ya usalama inadumishwa.

“Wagombeaji kadhaa pia wako katika hatua za mwisho, kujipigia debe na kuwashawishi wapiga kura kuwachagua kama wasemaji wao,” akasema.

Aliongezea kuwa ameridhishwa na jinsi wanafunzi walidumisha hali ya utulivu,tangu waanze kampeni zao yapata wiki mbili zilizopita.

Baada ya uchaguzi walalamishi wanatakiwa kuwasilisha malalamishi yao kabla ya siku ya Jumatano saa 5.00 jioni lau sivyo washindi kutangazwa.

Baadhi ya wanafunzi wakishiriki zoezi la uchaguzi. Picha/ Richard Maosi

Hii ni mara ya kwanza katika Chuo cha Egerton uchaguzi kuendeshwa chini ya muungano wa wanafunzi yaani Egerton University Student Association.

“Wanafunzi walibuni tume yao na kujadiliana kwa kina.Wakaamua kuwakilisha kila kundi hata wale walemavu wana nafasi yao,” alisema.

Zoezi la uungwaji mkono linategemea ajenda za yule anayesimama,muradi ateke nyoyo za wafuasi wake.

Taifa Leo Dijitali ilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wagomeaji na haya hapa ni maoni yao.

Dennis Kirui anapania kuteuliwa kama rais, akiwa mwanafunzi wa somo la uhandisi mwaka wa tatu,alisema wafuasi wake ni wengi na anatarajia kuwabwaga .

Timu ya IEBC iliyotumwa kushuhudia zoezi la upigaji kura. Picha/ Richard Maosi

Alisema uchaguzi wa viongozi kwa misingi ya kabila na matabaka,ulikuwa umepitwa na wakati.

Hata hivyo alielezea kuwa hajakuwa akiridhishwa na jinsi uongozi wa chuo umekuwa ukilazimisha baadhi ya wagombea kuingia mamlakani.

“Mara hii nitahakikisha ninatimiza manifesto yangu kwa kuwatendea kazi wote watakaoniunga mkono na wale ambao hawatanichagua,” alisema.

Aliwarai wapinzani wake kuungana naye kwani hawakuwa na jipya la kuwatendea wanafunzi,ikilinganishwa na maono yake.

Kupitia msemaji wake Ngeno Kiplagat wamekuwa wakipatana na wafuasi wao,muda wa jioni uwanjani,madarasani na wakati mwingine katika sehemu za malazi.

Profesa Julius Kipkemboi msimamizi wa uchaguzi huru katika Chuo Kikuu Cha Egerton. Picha/ Richard Maosi

Dennis aliahidi kupigana na uhalifu,ambao umekuwa donda sugu katika baadhi ya maeneo Chuoni hasa Ngonde Centre na nje ya shule.

Angeungana na usimamamizi wa shule kushinikiza huduma bora zinamfikia kila mwanafunzi anayeishi Chuoni.

“Ikiwezekana nitashirikisha NTSA kukarabati miundo mbinu ambayo haijaleta manufaa yoyote Chuoni.Barabara ni mbaya na zile zilizopo ni duni,”alisema.

Chuo cha Egerton kimekuwa kikizungukwa na utata kutokana na uhaba wa raslimali kutosheleza mahitaji ya wasomi zaidi ya 14,000.

Dennis Kirui (kushoto) akizungumza na baadhi ya wafuasi wake katika mijengo ya Chuo kabla ya kushiriki zoezi la upigaji kura. Picha/ Richard Maosi

Patrick Shegu ni mwanafunzi wa Uhasibu lakini anaendesha biashara ya kuuza vitafunio nje ya Chuo,kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Alisema ana matumaini makubwa kwa uongozi unaokuja kwani hela za kuwasaidia wanafunzi wasiojiweza zimekuwa zikiwekewa masharti.

Wiki iliyopita Chuo Kikuu Cha Nairobi kiliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu,kwa kupata kiongozi wa kwanza wa kike tangu muungano wa wanafunzi kuanzishwa.

Pablo Shegu mwanafunzi anayefanya kazi ya kuuza vitafunio baada ya uongozi wa kwanza kukosa kumsaidia apate karo. Picha/ Richard Maosi

Kinyume na matarajio ya wengi wadhifa huo umekuwa ukichukuliwa na wanafunzi wa jinsia ya kiume miaka nenda miaka rudi.

Hili linaashiria jinsi uchaguzi katika muungano wa wanafunzi kote nchini unaendelea kupata ungwaji mkono kutokana na demokrasia yake.

You can share this post!

Shujaa yaomba kukwepa shoka Raga ya Dunia

Vipusa wa Kahawa United wawazima wenzao wa Kangemi

adminleo