• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Nitafufua vipaji vya filamu nchini – Ruto

Nitafufua vipaji vya filamu nchini – Ruto

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amesema Serikali inalenga kustawisha sekta ya filamu nchini kama njia ya kuzalisha nafasi za ajira kwa Wakenya, haswa kwa vijana.

Alisema sekta hiyo ina uwezo mkubwa wa kukua na hivyo inapasa kuchukuliwa kama kichocheo cha maendeleo katika sekta mbalimbali ya uchumi nchini.

Akiongea alipokutana na waelekezi wa michezo katika makala ya 60 ya Tamasha ya Drama na Filamu miongoni mwa Shule na Vyuo afisini mwake Karen Jumanne, Dkt Ruto alisema mengi yanapasa kufanywa kuendeleza sekta ya filamu nchini.

“Nitaongoza juhudi za kimakusudi za kuhakikisha sekta ya filamu imefikia upeo wa maendeleo, sawa na michezo ya kuigiza na sanaa nyinginezo za kubuni,” akasema.

Aliwataka wadau wote katika sekta ya filamu kufanyakazi pamoja ili kuandaa sera itakayoweka mwongozo wa ufufuzi wa sekta hiyo katika kipindi kifupi kijacho.

“Sharti tuwe na mpango wa namna tunapanga kuendeleza sekta hii. Sharti tupalilie talanta, na ujuzi miongoni mwa vijana na ninawahakikishia usaidizi kutoka kwa serikali,” Dkt Ruto akasema.

Waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Elimu George Magoha, Katibu wa Wizara hiyo Belio Kipsang, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kuainisha Filamu Nchini (KFCB) Ezekiel Mutua, Mwenyekiti wa Tamasha za Kitaifa za Michezo ya Kuigiza kwa Shule na Vyuo Profesa Christopher Odhiambo, Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Mawasiliano Nchini (CA) Francis Wangusi, kati ya wengine.

Dkt Ruto aliwataka walimu na wazazi kuwatambua wanafunzi wenye talanta zao katika sanaa ya kuigizaji kwa kuwapa nafasi ya kushiriki tamasha mbalimbali za uigizaji.

“Kando na masomo ya darasani ni muhimu pia kuzingatia kuwa wanafunzi wanaweza kuwa weledi katika michezo, muziki na uigizaji fani ambazo zinaweza kuwasaidia maishani,” akasema Dkt Ruto.

You can share this post!

Vipusa wa Kahawa United wawazima wenzao wa Kangemi

Stars kufahamu Ijumaa wapinzani wake wa mechi za kirafiki

adminleo