• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Usajili wa Huduma Namba utaendelea baada ya siku 45 – Matiang’i

Usajili wa Huduma Namba utaendelea baada ya siku 45 – Matiang’i

Na PETER MBURU

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i amesema kuwa usajili wa watu kidijitali ili kupata Huduma Namba utaendelea hata baada ya siku 45 ambazo serikali ilikuwa imetangaza.

Dkt Matiang’i alisema kuwa watu ambao kwa sababu fulani hawatakuwa wamejisajili kufikia Mei 18, siku ya mwisho watapata huduma hizo katika afisi za manaibu chifu, kwani vifaa vya usajili vitasalia huko kuendelea kufanya kazi hiyo.

Akisifia zoezi hilo kuwa limechangamkiwa na Wakenya kiwango cha kusajili zaidi ya watu milioni nane kufikia Jumatatu, waziri huyo alisema watu wanafaa kujitokeza zaidi kwani ‘Huduma Namba’ itawasaidia kurahisishiwa huduma za serikali.

“Kufikia Mei 18, sidhani kutakuwa na sababu ya kusongesha tarehe ya mwisho mbele kwani Wakenya wote wanaotaka kujisajili watakuwa wamefanya hivyo.

“Lakini hata hivyo, Wakenya wanafaa kujua kuwa tulinunua vifaa hivyo vya usajili na vitasalia na manaibu chifu hata baada ya usajili kufanyika ili wale watu, kwa sababu fulani, hawataweza kujisajili wapate huduma hizo katika afisi hizo. Tunataka zoezi hili liwe likifanywa kila wakati, ili tuwe tukinakili habari za watu kila wakati,” akasema Dkt Matiang’i alipokuwa akihojiwa na runinga ya NTV.

Waziri huyo aidha alipuuza baadhi ya viongozi kutoka mrengo wa Naibu Rais William Ruto ambao wamelalamika kupokonywa walinzi, akiitaja kuwa hatua ya mageuzi ambayo inaendelea katika idara ya usalama na ambayo itaendelea kutekelezwa.

You can share this post!

Wabunge wadai muungano mpya wa kisiasa watokota 2022

NGILA: Teknolojia ya AI yahitaji sifa za binadamu

adminleo