• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Magavana wataja njaa kuwa janga la kitaifa

Magavana wataja njaa kuwa janga la kitaifa

 Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA wametofautiana na serikali ya kitaifa kuhusu idadi ya waathiriwa wa baa la njaa huku wakisema kuwa watu milioni 6.5 wanahitaji chakula cha msaada kwa dharura.

Wakiongozwa na kiranja wa Baraza la Magavana (CoG), Prof Kivutha Kibwana, magavana hao; Charity Ngilu (Kitui), Martin Wambora (Embu) na Nderitu Muriithi (Laikipia), walimtaka Rais Kenyatta kutangaza baa la njaa kuwa janga la kitaifa.

Walisema hatua hiyo itasaidia kuwezesha wahisani na serikali kusaidia waathiriwa wa njaa, haswa katika kaunti 13 zilizoathirika zaidi.

Hii ni tofauti na idadi ya watu 1.1 milioni iliyotolewa na Waziri wa Ugatuzi , Eugene Wamalwa ambaye alisema serikali ina chakula cha kutosha na hakuna haja ya Wakenya kuwa na wasiwasi.

Bw Wamalwa alisema serikali inaendelea kusambaza chakula cha msaada katika kaunti za Turkana, Mandera, Marsabit, Garissa, Kilifi, Baringo, Pokot Magharibi, Isiolo, Wajir, Samburu, Kwale, Tana River, Kwale na Makueni.

“Hali ni mbaya zaidi katika kaunti 13 zinazokumbwa na ukame kwani kuna uhaba mkubwa wa chakula, maji na lishe kwa mifugo. Hii ndio maana tunaitaka serikali kutangaza hali hii kuwa janga la kitaifa ili mashiriki mengi yaweze kutoa misaada,” Prof Kibwana akasema jana.

Naye gavana Muriithi aliwataka viongozi wote kuweka kando masuala mengine na kuelekeza nguvu na juhudi zaidi katika mipango ya kukabiliana na baa la njaa inayosabishwa na makali ya ukame.

“Hitaji kuu nchini wakati huu ni chakula kwa watu wetu. Tunaomba viongozi kuweka kando masuala mengine kama siasa kando. Binafsi naungana na wenzangu kumsihi Rais atangaze changamoto hii kama janga la kitaifa,” akawaambia wanahabari katika makao makuu ya CoG, mtaani Westlands Nairobi.

Bi Ngilu na Bw Wambora nao walisema ukame unaoshuhudiwa nchini ndio umesababisha mkurupuko wa kipindupindu katika maeneo husika kufuatia uhaba wa maji.

“Kiangazi kinachoshuhudiwa nchini ndio chanzo cha mkurupuko wa kipindupindu katika maeneo mengi nchini. Hii ndio maana tunatoa wito kwa serikali ya kitaifa na mashirika ya kibinafsi kuingilia kati hali kwa kusambaza maji safi katika maeneo husika,” akasema Bi Ngilu.

Gavana Wambora alisema kaunti yake imepokea ufadhili wa Sh108 milioni kutoka kwa kampuni ya kuzalisha umeme nchini, KenGen kufanikisha mpango wa kusambaza maji kwa wakati wa Embu Kusini.

“Tunatoa wito kwa mashirika mengi kuiga mfano huu mzuri wa KenGen kama njia ya kuokoa watu wetu dhidi ya maambukizi ya kipindupindi,” akasema.

Magavana hao walisema baraza la magavana liko tayari kushirikiana na Serikali ya kitaifa kuanzisha miradi ya kilimo cha unyunyiziaji katika kaunti ambazo huathiriwa na kiangazi kila mara.

Idara ya hali ya anga pia imetangaza kuwa mvua haitanyesha msimu huu kama inavyotarajiwa, hali ambayo huenda ikaongeza makali ya njaa.

Tayari wakulima wengi waliopanda mahindi walilazimika kuyang’oa au kupanda upya, baada ya waliopanda kukosa kuota au kunyauka.

You can share this post!

NEMA yafunga viwanda vitatu

Wakenya wachemka kupinga ada ya ujenzi wa nyumba

adminleo